" SERIKALI KUANZA AWAMU YA PILI YA CHANJO YA POLIO MEI 7–10; ZAIDI YA WATOTO 71,000 SHINYANGA KUNUFAIKA

SERIKALI KUANZA AWAMU YA PILI YA CHANJO YA POLIO MEI 7–10; ZAIDI YA WATOTO 71,000 SHINYANGA KUNUFAIKA

Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Elisha Robert, akitoa elimu kuhusu umuhimu wa chanjo ya polio kwa wadau na kuwahimiza wazazi kuhakikisha watoto wanapatiwa chanjo kwa wakati.

Serikali kupitia Wizara ya Afya inatarajia kuendesha zoezi la utoaji wa chanjo ya matone ya polio kuanzia Mei 7 hadi 10, 2026, likilenga watoto wote walio chini ya umri wa miaka 10. Hii ni awamu ya pili ya kampeni hiyo ya kitaifa, baada ya awamu ya kwanza kufanyika Machi mwaka huu.

Katika kujiandaa na utekelezaji wa zoezi hilo, serikali imeendesha mafunzo maalum kwa wadau mbalimbali wenye ushawishi katika jamii, yakiwemo viongozi wa kimila, dini na makundi ya kijamii, kwa lengo la kujenga uelewa wa pamoja na kuhakikisha ujumbe sahihi unawafikia wananchi.

Akizungumza wakati wa mafunzo hayo yaliyofanyika Mei 4, 2026, Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, Ramadhani Maneno, alisema lengo kuu ni kuhakikisha jamii inaelewa umuhimu wa chanjo hiyo na kushiriki kikamilifu katika kampeni hiyo inayotekelezwa katika mikoa saba ikiwemo Shinyanga, Geita, Mara, Singida, Simiyu, Kagera na Tabora.

Alisema katika Manispaa ya Shinyanga pekee, jumla ya watoto 71,966 wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo katika awamu ya pili, ikiwa ni jitihada za kuimarisha kinga dhidi ya ugonjwa wa polio ambao unaweza kusababisha kupooza kwa ghafla na ulemavu wa kudumu kwa watoto.

“Tumekamilisha maandalizi ya kutosha kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa chanjo. Tumeunda jumla ya timu 91, ambapo timu 83 zitafanya kazi ya kuwafikia watoto nyumba kwa nyumba, na timu 8 zitahudumu katika maeneo ya mikusanyiko kama masoko na vituo vya huduma za jamii,” alisema Maneno.

Kwa upande wake, mwakilishi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) Idara ya Afya, Linda Chatila, alisema kampeni hiyo siyo mpya bali ni mwendelezo wa juhudi za muda mrefu za serikali kudhibiti ugonjwa huo. Alifafanua kuwa uamuzi wa kuendesha kampeni maalum umetokana na kubainika kwa vimelea vya polio katika maji taka jijini Mwanza, hali iliyozua tahadhari ya kitaifa.

“Polio haina tiba, lakini inazuilika kwa chanjo. Ni wajibu wa kila mzazi kuhakikisha mtoto wake anapata chanjo kwa wakati ili kumkinga dhidi ya hatari ya kupooza,” alisema Chatila.

Aliongeza kuwa chanjo hiyo ni salama na imeidhinishwa na taasisi za kitaifa na kimataifa ikiwemo Shirika la Afya Duniani (WHO) pamoja na Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA). Alitoa rai kwa wazazi kupuuza taarifa potofu zinazosambazwa kuhusu chanjo hiyo na badala yake kufuata maelekezo ya wataalamu wa afya.

Akizungumza katika mafunzo hayo, Mganga Mkuu wa Manispaa ya Shinyanga, Dkt. Elisha Robert, alisema zoezi la chanjo ya polio ni muhimu katika kulinda afya za watoto na kuzuia madhara makubwa yanayoweza kusababishwa na ugonjwa huo.

 Alieleza kuwa polio ni ugonjwa hatari unaoweza kusababisha ulemavu wa kudumu kwa mtoto ndani ya muda mfupi, hivyo ni lazima jamii ichukue hatua za kinga mapema.

Dkt. Robert aliwahimiza wazazi na walezi kuhakikisha watoto wote walio chini ya umri wa miaka kumi wanapatiwa chanjo hiyo bila kukosa, akisisitiza kuwa chanjo ni salama, haina madhara na ndiyo njia bora ya kuzuia ugonjwa huo.

Aidha, alitoa wito kwa wadau na viongozi wa jamii kuendelea kutoa elimu sahihi kwa wananchi ili kuondoa hofu na imani potofu zinazoweza kuathiri mafanikio ya zoezi hilo.

Wadau mbalimbali waliohudhuria mafunzo hayo wameeleza kuunga mkono jitihada hizo za serikali. Kamanda Mkuu wa Sungusungu Mkoa wa Shinyanga, John Kadama, alisema watashirikiana kikamilifu kuhakikisha zoezi hilo linafanyika kwa ufanisi hadi kufikia kila mtoto anayelengwa.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Manispaa ya Shinyanga, Stephano Tano, aliwataka wazazi na walezi kutumia fursa hiyo kuhakikisha watoto wao wanapatiwa chanjo, akibainisha kuwa ni njia muhimu ya kuzuia ulemavu na vifo vinavyoweza kuepukika.

Serikali imeendelea kusisitiza kuwa mafanikio ya kampeni hiyo yanategemea ushirikiano wa wadau wote, hasa wazazi na walezi, katika kuhakikisha watoto wote walio chini ya miaka 10 wanapatiwa chanjo kwa wakati, ili kulinda afya ya kizazi cha sasa na kijacho.

Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, Ramadhani Manen. akielezea zoezi hilo. 

Mratibu wa Chanjo Manispaa ya Shinyanga, Ramadhani Maneno akielezea. 


 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

Post a Comment

Previous Post Next Post