Na Avitus Benedicto, MissenyiWananchi wa Kata ya Ruzinga, Wilaya ya Missenyi mkoani Kagera, wametakiwa kujikita katika shughuli za uzalishaji mali ili kuongeza kipato cha mtu mmoja mmoja na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa, huku wakihimizwa kuachana na makundi ya kisiasa kwa kuwa uchaguzi ulimalizika zamani.Rai hiyo imetolewa na Diwani wa Kata ya Ruzinga, Mhe. Aspon Mwijage, wakati akizungumza katika kikao cha wananchi kilichofanyika Kijiji cha Ruhija. Amesema maendeleo ya kata hiyo yanategemea mshikamano na juhudi za wananchi katika kufanya kazi kwa bidii badala ya kugawanyika kisiasa.Mhe. Mwijage amesema kuwa tangu alipoingia madarakani aliahidi kuhakikisha shule zote za msingi zilizopo katika kata hiyo zinapata huduma ya lishe kwa wanafunzi. Amesema ahadi hiyo tayari imetekelezwa, ambapo kila mwanafunzi hupata uji shuleni, huku akitumia zaidi ya shilingi milioni 3.6 kila mwaka kufanikisha mpango huo.Akizungumzia changamoto ya maji, diwani huyo amesema anaendelea kupambana kuhakikisha Kata ya Ruzinga inapata huduma ya maji ya uhakika. Ameeleza kuwa changamoto hiyo imedumu kwa miaka mingi kutokana na jiografia ya eneo hilo, huku chanzo kikuu cha maji kutokidhi mahitaji na miundombinu iliyopo kuendelea kuharibika na kuvuja.Aidha, amesema changamoto ya maji katika Shule ya Sekondari Ruzinga imepatiwa ufumbuzi kupitia ushirikiano wa wadau mbalimbali wa maendeleo. Amewashukuru Bw. Antimus Rwebangira na Dk. Aliphuns Tibaijuka kwa mchango wao wa kifedha uliowezesha ukarabati wa miundombinu ya maji shuleni hapo.Mhe. Mwijage pia amewapongeza wadau wa maendeleo wa Ruzinga Day (RD) kwa kuendelea kushirikiana na wananchi katika kutekeleza miradi ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo la OPD, hatua inayolenga kuboresha huduma za afya katika kata hiyo.Katika sekta ya kilimo, amewahimiza wananchi kuendelea kulima mazao ya biashara kama kahawa, vanilla na mazao mengine yenye tija. Amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan inaendelea kuboresha mazingira ya kilimo kupitia uimarishaji wa miundombinu na kuongezeka kwa bei za mazao, hali inayowapa wakulima fursa ya kuongeza kipato.Pia ameushukuru uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), pamoja na viongozi wa wilaya na mkoa, kwa ushirikiano wanaompa katika kusukuma mbele maendeleo ya Kata ya Ruzinga.Kwa upande wao, baadhi ya wananchi akiwemo Bw. Salvatory Anatory, Bi. Josephina Thomas na Bw. Salvatory Rutahiwa, wamempongeza Mhe. Aspon Mwijage kwa juhudi zake za kuwaletea maendeleo. Wamesema amekuwa kiongozi anayeshirikiana kwa karibu na wananchi tangu alipochaguliwa na ameendelea kutatua changamoto mbalimbali zinazowakabili.Naye Mtendaji wa Kijiji cha Ruhija, Bw. Abdalla Kaserwa, amesema hali ya ulinzi na usalama kijijini hapo ni nzuri. Amewataka vijana kujiepusha na vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani na badala yake wajikite katika shughuli za kujiongezea kipato.Pia amewahimiza wananchi kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya magonjwa ya mlipuko kwa kuzingatia usafi wa mazingira na kuwahi kufika katika vituo vya afya mara wanapoona dalili zisizo za kawaida.SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment