Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda leo Juni 25, 2026
imefanya Baraza lake la Kikanuni ambapo wajumbe walijadili masuala mbalimbali
yanayolenga kuimarisha uhai wa jumuiya, kuongeza wanachama, kuendeleza miradi
ya maendeleo pamoja na kufanya maandalizi ya ushiriki katika Maadhimisho ya
Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoani Mwanza.
Uongozi wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda
ulisisitiza umuhimu wa wanachama wote kuendelea kulipia ada za uanachama ili
kuhakikisha jumuiya inaendelea kuwa imara na kutekeleza majukumu yake kwa
ufanisi katika ngazi za matawi, kata na wilaya.
Baraza hilo pia lilijadili mikakati ya kuongeza idadi
ya wanachama kupitia kampeni za usajili katika maeneo mbalimbali ya wilaya.
Wajumbe walikubaliana kuwa elimu na hamasa ziongezwe ili kuwafikia wananchi
wengi zaidi na kuwahamasisha kujiunga na jumuiya pamoja na kutimiza wajibu wao
wa kulipia ada za uanachama.
Ili kurahisisha zoezi hilo, Jumuiya imepanga kutumia
maafisa wa TEHAMA kutembelea matawi na kata mbalimbali kwa lengo la kutoa elimu
kuhusu namna ya kujiunga na jumuiya na kufanya malipo kupitia simu, mawakala na
benki.
Moja ya ajenda kuu zilizojadiliwa katika baraza hilo
ni hatma ya Shule ya Sekondari na Ufundi Milala iliyopo Kijiji cha Milala, Kata
ya Misunkumilo, ambayo imekuwa haisomeshi kwa kipindi cha miaka mitano.
Wajumbe walieleza kuwa shule hiyo ni mali ya Jumuiya
ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na ina mchango mkubwa katika maendeleo ya elimu
endapo itafufuliwa na kuendelezwa. Kutokana na hali hiyo, baraza lilisisitiza
umuhimu wa kupima eneo la shule, kuboresha miundombinu na kuandaa mazingira
rafiki yatakayowezesha kuanza tena kwa shughuli za elimu na mafunzo ya ufundi.
Aidha, ilielezwa kuwa shule hiyo bado haina hati
miliki ya eneo lake, jambo ambalo limekuwa moja ya changamoto zinazochelewesha
maendeleo yake. Viongozi wa jumuiya wameahidi kushirikiana na wadau mbalimbali
kuhakikisha hati miliki inapatikana pamoja na kukamilisha upimaji wa eneo
husika.
Baraza lilieleza kuwa shule hiyo inahitaji kiasi cha
shilingi milioni 2.3 kwa ajili ya upimaji na upangaji wa eneo, huku
likibainisha kuwa taarifa zinazoeleza kuwepo kwa mgogoro kati ya shule hiyo na
kanisa si za kweli. Wajumbe walisisitiza kuwa shule hiyo ni mali halali ya
Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda na hakuna mgogoro wowote unaoendelea.
Kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya
Mpanda imetoa wito kwa wadau wa maendeleo, viongozi na wananchi wenye mapenzi
mema kujitokeza kusaidia juhudi za kuifufua shule hiyo ili iweze kutoa huduma
za elimu na mafunzo kwa vijana wa Mkoa wa Katavi na maeneo jirani.
Katika hatua nyingine, baraza lilijadili miradi
mbalimbali ya kiuchumi inayolenga kuimarisha uwezo wa kifedha wa jumuiya.
Wajumbe walihimizwa kubuni na kuanzisha miradi ya kimkakati katika matawi na
kata ili kuongeza mapato na kuifanya jumuiya kujitegemea zaidi katika
utekelezaji wa shughuli zake.
Baraza hilo pia lilipokea na kujadili taarifa ya
tathmini ya Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Wilaya ya Mpanda yaliyofanyika Mei 7,
2026 katika Hospitali ya Halmashauri ya Nsimbo, Kata ya Mtapenda. Wajumbe
walitoa pongezi kwa mafanikio ya maadhimisho hayo yaliyohusisha utoaji wa
misaada kwa wagonjwa pamoja na upandaji wa miti ya matunda na kivuli.
Maadhimisho hayo yalihudhuriwa na viongozi wa Chama
Cha Mapinduzi (CCM), Serikali pamoja na wananchi mbalimbali chini ya uongozi wa
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi Mkoa wa Katavi, Ndugu Evarist Simon Mnyele.
Baraza la Kikanuni la leo pia lilisisitiza umuhimu wa
viongozi kuendelea kufanya ziara katika matawi na kata kwa lengo la kutoa elimu
kuhusu malezi, mazingira na kuimarisha uhai wa Jumuiya ya Wazazi ndani ya
Wilaya ya Mpanda.
Sambamba na hilo, wajumbe walijadili maandalizi ya
ushiriki katika Maadhimisho ya Wiki ya Wazazi Kitaifa yatakayofanyika Mkoani
Mwanza kuanzia Juni 30 hadi Julai 4, 2026. Baraza lilieleza kuwa ushiriki wa
wanachama katika maadhimisho hayo ni muhimu kwa kuimarisha umoja, mshikamano na
kubadilishana uzoefu na wanachama kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Katibu wa Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda, Ndugu
Jimotoli Jilala Maduka, aliwahamasisha viongozi na wanachama kushiriki
kikamilifu katika maadhimisho hayo huku akisisitiza kuwa umoja na mshikamano ni
msingi wa mafanikio ya jumuiya na Chama Cha Mapinduzi.
Aidha, Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda ilitumia
fursa hiyo kutoa shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge, Madiwani pamoja na viongozi
mbalimbali wa CCM wanaoendelea kushirikiana na kuisaidia jumuiya katika
utekelezaji wa shughuli zake za maendeleo.
Baraza hilo lilihitimishwa kwa wito wa kuendelea
kuimarisha mshikamano, ushirikiano na kujitolea katika shughuli za maendeleo
kwa manufaa ya jamii na taifa kwa ujumla.
Ndugu Pius M. Buzumalle, Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, akifungua Baraza la Kikanuni la Jumuiya hiyo leo Juni 25, 2026. Katika baraza hilo, amesisitiza umuhimu wa umoja na mshikamano miongoni mwa wanachama na viongozi ili kuendelea kuimarisha na kuendeleza Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda. Aidha, aliwakaribisha wajumbe kushiriki kikamilifu katika kujadili agenda mbalimbali na kutoa mawazo yatakayochochea maendeleo ya jumuiya hiyo.
Ndugu Jimotoli Jilala Maduka, Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazazi Wilaya ya Mpanda wakati wa kikao kilichofanyika Juni 25, 2026. Katika salamu zake, aliwashukuru wajumbe kwa kujitokeza kushiriki baraza hilo na kuwaomba kuwa watulivu, makini na kushiriki kikamilifu katika kujadili agenda mbalimbali zilizowasilishwa kwa ajili ya maendeleo ya Jumuiya ya Wazazi Wilaya ya Mpanda.

Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa
ya Mpanda, Mheshimiwa Charles Venance Philipo, akizungumza katika Baraza la
Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda lililofanyika Juni 25, 2026 katika Ukumbi wa CCM
Wilaya ya Mpanda. Katika hotuba yake, alieleza mafanikio mbalimbali ya
maendeleo na utekelezaji wa miradi inayotekelezwa kupitia Ilani ya Chama Cha
Mapinduzi (CCM), huku akisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya viongozi,
Serikali na wananchi katika kuharakisha maendeleo ya Wilaya ya Mpanda.

Ndg. Pendo, Katibu wa Umoja wa Vijana Mkoa wa Katavi, ameshiriki kikamilifu kikao cha Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.
Akipata nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa kikao hicho, amewahimiza vijana pamoja na makundi mbalimbali ya jamii kutambua na kutumia fursa zilizopo ili kukabiliana na changamoto zinazowakabili, huku akisisitiza umuhimu wa ubunifu, ushirikiano na kujituma katika kuleta maendeleo ya jamii na taifa kwa ujumla.
Wajumbe wa Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda wakiwa katika kikao cha Baraza hilo, wakisikiliza kwa umakini mijadala na maamuzi yaliyokuwa yakiwasilishwa.
Ndg. Chasila, Mjumbe wa Kamati ya Utekelezaji ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, ameshiriki kikamilifu kikao cha Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.
Katika kikao hicho, amesisitiza umuhimu wa kila kiongozi kutambua nafasi na wajibu alionao katika kutekeleza majukumu yake kwa uadilifu, uwajibikaji na kwa kuzingatia maslahi ya Chama na wananchi kwa ujumla.
Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mheshimiwa Charles Venance Philipo, akizungumza na wajumbe wa Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda wakati wa kikao kilichofanyika Juni 25, 2026. Akitoa salamu zake, aliwashukuru na kuwapongeza wajumbe kwa kudumisha umoja na mshikamano ndani ya Jumuiya ya Wazazi, huku akieleza kufurahishwa na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jumuiya hiyo, Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Serikali katika kuwaletea wananchi maendeleo ya Wilaya ya Mpanda.
Ndugu Raymond Janda Nyogoto, Mjumbe wa Kamati Ndogo ya Uchumi, Mipango na Fedha ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, ameshiriki kikamilifu kikao cha Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.
Katika kikao hicho, amesisitiza umuhimu wa ubunifu katika kuanzisha na kuendeleza miradi mbalimbali ya Jumuiya, akibainisha kuwa hatua hiyo itaongeza nguvu ya kiuchumi na kuweka msingi imara wa maendeleo makubwa na endelevu ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.

Wajumbe wakiwa katika picha ya pamoja mara baada ya kikao cha Baraza la Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254






Post a Comment