
Leo hii, Trashto Treasure hukusanya taka za plastiki kutoka kwenye jamii na kuzibadilisha kuwa vifaa vya kujifunzia vinavyobadilisha maisha ya watoto. Lakini safari hiyo haikuanza kwa urahisi.
Mwaka 2021, mwanzilishi wa Trashto Treasure alijiuliza swali moja:
“Vipi kama hiki kitu tunachokiita taka kinaweza kuwa fursa?”
Kwa mtoto mdogo aliyekulia katika familia ya kipato cha chini, mazingira ya kujifunzia hayakuwa rahisi. Vifaa vya kujifunzia vilikuwa vichache, na mara nyingi yeye na watoto wengine walitumia vijiti, vizibo vya soda na vitu vya kawaida vilivyopatikana mazingira ya karibu kama njia ya kujifunzia herufi na namba.
Lakini kulikuwa na jambo jingine lililomgusa zaidi.
Kila jioni baada ya shule, yeye na marafiki zake walikuwa wakielekea uwanjani kucheza mpira huku kila mmoja akiwa na ndoto ya kuwa kama Ronaldo. Karibu na uwanja huo kulikuwa na mtaro mdogo.
Kilamvua iliponyesha, maji yalifurika yakiwa yamebeba taka nyingi za plastiki. Maji hayo yaliingia mpaka uwanjani, yakiacha uchafu kila mahali.
Kwa mtoto mdogo, hiyo ilikuwa kero.Lakini miaka kadhaa baadaye, jambo lilelile ambalo lilionekana kuwa tatizo liligeuka kuwa mwanzo wa suluhisho kubwa.
Hapo ndipo ilipoanza safari ya Trashto Treasure iliyopo Sumbawanga, mkoani Rukwa.
Wazo halikuwa tu kuondoa taka kwenye mazingira. Wazo lilikuwa kuzibadilisha taka kuwa vitu vinavyoweza kubadili maisha ya watoto wengine.
“Taka ni mali.”
Hiyo si kaulimbiu tu kwa Trashto Treasure, bali ni maisha, ni imani, na ni safari iliyoanza kutoka kwenye kumbukumbu za utoto.
Kupitia ukusanyaji wa taka za plastiki kutoka maeneo mbalimbali, taka hizo huchambuliwa, kusafishwa na kuchakatwa, kisha kubadilishwa kuwa vifaa vya kujifunzia vinavyowasaidia watoto wa kawaida na wale wenye mahitaji maalum kujifunza na kucheza.
Miongoni mwa vifaa vinavyotengenezwa ni meno ya kujifunzia, fuvu la kichwa cha binadamu, mifupa ya mfano, herufi, namba pamoja na vifaa vingine vya elimu vinavyorahisisha elimu kwa vitendo.
Mpaka sasa, Trashto Treasure imefanikiwa kutengeneza katoni 320 za vifaa vya kujifunzia herufi na namba, pamoja na zaidi ya vifaa 400 vya mifano ya kujifunzia kama vile mifupa ya binadamu, meno, fuvu la kichwa na vifaa vingine vinavyomfanya mtoto afurahie kwenda shule.
Lakini safari haikuwa rahisi.
Mwanzoni, changamoto zilikuwa nyingi. Mfumo wa kazi ulikuwa wa kawaida, matokeo yalikuwa magumu kupima na mipango ya muda mrefu haikuwa imejengwa vizuri.
Kabla ya kushiriki katika programu ya Regenerative Economy Accelerator Tanzania (REAT), Trashto Treasure tayari ilikuwa ikifanya kazi nzuri kupitia ushirikiano wa jamii na hatua mbalimbali za mazingira. Hata hivyo, ukuaji wake ulikuwa na changamoto.
Kupitia REAT, mabadiliko makubwa hayakuwa tu kujifunza namna ya kuchakata taka.
Mabadiliko makubwa yalikuwa kubadilisha mtazamo.
Kutoka kujiuliza:
“Tunawezaje kuchakata taka?”
Kwenda kwenye swali kubwa zaidi:
“Tunawezaje kujenga mfumo unaobadilisha mazingira, elimu, uchumi na maisha ya watu kwa wakati mmoja?”
Hicho ndicho kinachoitwa kubadili tatizo kuwa suluhisho.
Baada ya kuimarisha mfumo wake wa biashara kupitia mtazamo wa uchumi rejeshi, Trashto Treasure imeweza kuongeza mara mbili uwezo wake wa kukusanya taka za plastiki.
Leo hii, kampuni inakusanya takriban tani 14 za plastiki kwa mwaka.
Kati ya Oktoba na Desemba 2025, kiwango cha plastiki kilichochakatwa kiliongezeka kwa kiasi kikubwa huku biashara ikizalisha zaidi ya shilingi milioni 28 kwa mwaka.
Matokeo yalianza kuonekana.
Lakini mafanikio makubwa zaidi hayakuonekana kwenye fedha. Yalionekana kwa watu.
Kupitia kampeni za mara kwa mara za kuokota taka katika mitaa mbalimbali, jamii ilianza kubadilika. Watu ambao zamani walikuwa wakipita pembeni ya taka bila kuziona, sasa wanaanza kuzikusanya na kuziuza kwa Trashto Treasure.
Leo hii, mfumo huu wa uchumi rejeshi umegeuka kuwa chanzo cha ajira na kipato kwa jamii.
Trashto Treasure inafanya kazi na wakusanyaji wa plastiki 20 wa Sumbawanga na Kigoma. Pia imeajiri wafanyakazi 12 wa kudumu pamoja na kutoa fursa kwa wanawake 10 wanaohusika maalumu na uchambuaji wa plastiki kabla ya kuingia kwenye hatua ya uchakataji.
Kwa baadhi yao, kitu kilichokuwa kikionekana kama taka leo kimekuwa sehemu ya kujenga maisha.
Kwa vijana na wanawake wengi, imekuwa fursa mpya.
Kwa shule, imekuwa njia ya kupata vifaa vya kujifunzia vya gharama nafuu vinavyodumu muda mrefu.
Mpaka sasa, Trashto Treasure imefikia shule 32 katika maeneo ya Iringa, Sumbawanga na Kigoma.
Lakini hii ni hatua ya mwanzo tu.
Tanzania ina zaidi ya shule 28,000, na bado shule nyingi zinahitaji vifaa bora vya kujifunzia, hasa kwa watoto wenye mahitaji maalum.
Mahitaji ni makubwa kuliko uwezo wa sasa wa uzalishaji.
Lakini ndani ya changamoto hiyo kuna ndoto kubwa.
Ndoto ya kuona watoto wa Kitanzania wakijifunza kwa kutumia vifaa vinavyowafanya waipende shule zaidi.
Ndoto ya kuona jamii zikiona taka si kama uchafu, bali kama rasilimali inayoweza kujenga maisha.
Kwa sababu mwisho wa siku, taka si mwisho wa hadithi.
Wakati mwingine, ndiyo mwanzo wa hadithi mpya kabisa.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment