Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama Cha Mapinduzi (NEC) imefanya mabadiliko katika Sekretarieti ya Chama kwa kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali, baada ya kupokea na kupitisha mapendekezo ya Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao maalum cha NEC kilichofanyika leo Jumatano, Julai 29, 2026, Zanzibar, chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Laban Kihongosi, kikao hicho kilifanya uteuzi wa viongozi wafuatao:
Rahma Kassim Ali, ambaye ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM kutoka Mkoa wa Kusini Unguja, ameteuliwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa, akichukua nafasi ya Leilah Burhan Ngozi.
Katika Sekretarieti ya Chama, Aggrey Deaisile Joshua Mwanry ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Bara, akichukua nafasi ya John Mongela. Mwanry, amewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora na ni Balozi wa zao la Pamba nchini.
Kwa upande wa Zanzibar, Abdi Mahmood Abdi ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, akichukua nafasi ya Mohammed Said Mohammed (Dimwa). Kabla ya uteuzi huo alikuwa Naibu Katibu Mkuu wa UVCCM Zanzibar.
Aidha, Paul Matiko Chacha, ambaye ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora, ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa - Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni, akichukua nafasi ya Issa Haji Ussi Gavu.
Vilevile, Jamal Kassim Ali ameteuliwa kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa - Mkuu wa Idara ya Uchumi na Fedha, akichukua nafasi ya Joshua Chacha Mirumbe.
Wakati huo huo, wajumbe wengine wa Sekretarieti wanaendelea na nafasi zao kama awali. Hao ni Dkt. Asha Rose Migiro ambaye anaendelea kuwa Katibu Mkuu wa CCM, Kenani Laban Kihongosi ambaye anaendelea kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Idara ya Itikadi, Uenezi na Mafunzo, pamoja na Rabia Hamid ambaye anaendelea kuwa Katibu wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Idara ya Siasa na Uhusiano wa Kimataifa.
Mbali na uteuzi huo, kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM Taifa pia kilijadili na kupitisha mapendekezo ya Sheria ya Jinsia na Ujumuishaji ya CCM ya Mwaka 2026, Mwongozo wa Dawati la Jinsia la CCM na Jumuiya zake, pamoja na maandalizi ya Uchaguzi wa Chama na Jumuiya zake utakaofanyika mwaka 2027.
Mabadiliko hayo yamefanyika ikiwa ni sehemu ya maamuzi ya NEC ya kuimarisha uongozi wa Chama kuelekea utekelezaji wa majukumu yake na maandalizi ya uchaguzi wa ndani wa mwaka 2027.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254


Post a Comment