Amesema mgeni rasmi siku ya ufunguzi anararajiwa Kuwa Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, ambaye pia atatembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo pamoja na kufanya mazungumzo na vijana wanaojishughulisha na kilimo, wakiwemo wanufaika wa programu ya BBT (Jenga Kesho Iliyo Bora).

Aidha, Waziri Chongolo amesema maboresho makubwa yamefanyika katika viwanja hivyo ili viweze kutumika mwaka mzima kwa ajili ya maonesho, utoaji wa mafunzo na huduma mbalimbali zinazohusiana na sekta ya kilimo.

Amebainisha kuwa tayari kimeanzishwa kituo cha huduma kwa wakulima kitakachopokea na kushughulikia taarifa kutoka kwa wakulima nchini, ikiwemo kutoa ufafanuzi kuhusu masuala ya mbegu na changamoto nyingine za kilimo.

Pia amesema Serikali imeanzisha kituo maalum cha kushughulikia dharura katika sekta ya kilimo ili kuhakikisha changamoto mbalimbali, ikiwemo uvamizi wa nzige na majanga mengine, zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati.

Ameongeza kuwa viwanja hivyo vitakuwa makao ya Wakala wa Huduma za Ugani, huku kituo maalum cha vijana kikiendelea kujengwa kwa lengo la kuwapatia mafunzo, taarifa za kilimo na huduma za teknolojia zitakazowawezesha kushiriki kikamilifu katika uzalishaji.

Kwa upande wa programu ya BBT, Mhe. Chongolo amesema Serikali inaendelea kuwawezesha vijana kwa kuwapatia miundombinu ya umwagiliaji, elimu ya afya ya udongo, mbegu bora na pembejeo ili kuongeza tija katika kilimo.

Amesema idadi ya washiriki imeongezeka kutoka takribani 800 mwaka jana hadi zaidi ya 1,000 mwaka huu, huku ushiriki wa nchi 24 ukithibitisha kuendelea kukua kwa hadhi ya kimataifa ya Maonesho ya Nane Nane.

Akizungumzia ushiriki wa vijana katika sekta hiyo, Chongolo amesema kilimo ni biashara yenye uwezo mkubwa wa kujenga mitaji na kuongeza kipato, akibainisha kuwa ongezeko la vijana wanaoingia kwenye uzalishaji, uchakataji na biashara ya mazao linaonesha umuhimu wa sekta hiyo katika ajira na maendeleo ya uchumi.

Akizungumzia ratiba ya Maonesho hayo, Waziri Chongolo amebainisha kuwa Agosti 2, Waziri Mkuu, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, atatembelea miradi inayotekelezwa na Wizara ya Kilimo pamoja na kuzungumza na vijana wanaoshiriki katika shughuli za kilimo.

Aidha,  Agosti 3 kutakuwa na shughuli za Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), zitakazoanza kwa mbio za marathon sambamba na maadhimisho ya ushirika, huku siku zinazofuata zikihusisha shughuli mbalimbali za sekta za mifugo na uvuvi.

Huku  kilele cha Maonesho ya Nane Nane 2026 kinatarajiwa kufanyika Agosti 8 mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.