ibu Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Said Shaib Mussa ameshiriki Mkutano wa Tatu wa Tume ya Pamoja ya Kudumu (JPC) kati ya Tanzania na Angola utakaodumu kwa siku mbili, tarehe 29 na 30 Julai, 2026.

JPC hiyo imeanza katika ngazi ya Maafisa Waandamizi ambapo wajumbe kutoka pande zote mbili wamejadili utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa katika JPC iliyofanyika Zanzibar, Tanzania mwaka 2024, pamoja na kuweka mikakati mipya ya kuendeleza ushirikiano kwa manufaa ya nchi zote mbili.

Akizungumza wakati wa kufunga mkutano ngazi ya maafisa waandamizi, Balozi Mussa amesisitiza umuhimu wa pande zote mbili kuhakikisha yote yanayoafikiwa katika JPC hii yanatekelezwa.

Kupitia JPC hii, Tanzania na Angola zinatarajia kuimarisha na kukuza zaidi ushirikiano wa uwili katika maeneo mbalimbali ikiwemo diplomasia, ulinzi na usalama, biashara na uwekezaji, maendeleo ya jamii, afya, elimu, sayansi, teknolojia na ubunifu.

Mkutano wa ngazi ya Mawaziri unatarajiwa kufanyika tarehe 30 Julai, ambapo pande zote mbili zitapokea na kujadili taarifa ya wataalamu, kupitisha maazimio ya Mkutano wa Tatu wa JPC, pamoja na kuweka mwelekeo wa utekelezaji wa maeneo mapya ya ushirikiano kati ya Tanzania na Angola.