" SHEHE BALILUSA AHAMASISHA UMOJA NA MARIDHIANO AWATAKA SUNGUSUNGU KULINDA AMANI

SHEHE BALILUSA AHAMASISHA UMOJA NA MARIDHIANO AWATAKA SUNGUSUNGU KULINDA AMANI

 


mwenyekiti wa JMAT Mkoa wa Shinyanga Shehe Balilusa Hamis 

Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga (JMAT), Shehe Balilusa Hamis, amewataka viongozi wa Sungusungu Wilaya ya Kahama kuendelea kutekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kwa kuzingatia sheria za nchi ili kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kutamalaki katika wilaya hiyo na Mkoa wa Shinyanga kwa ujumla.

Shehe Balilusa ametoa rai hiyo alipokuwa akizungumza na viongozi wa Sungusungu na Kamati ya maridhiano na amani Wilaya ya Kahama  katika kikao maalumu kilicholenga kujadili nafasi ya Sungusungu katika kuimarisha usalama wa wananchi, kuzuia migogoro ya kijamii pamoja na kuendeleza maridhiano miongoni mwa wananchi.

Amesema kuwa Sungusungu ni wadau muhimu katika kulinda usalama wa jamii kwa kushirikiana na vyombo vya dola, viongozi wa serikali na wananchi, hivyo wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia haki za binadamu, maadili na sheria za nchi, huku wakiepuka vitendo vinavyoweza kusababisha migogoro au uvunjifu wa amani.

"Ni wajibu wetu sote kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unaendelea kuwa wa amani na utulivu. Hilo linawezekana pale tutakaposhirikiana, kuheshimiana na kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria vya uhalifu au migogoro inayoweza kuhatarisha usalama wa wananchi," amesema Shehe Balilusa.

Aidha, amewataka viongozi hao kuendelea kutoa elimu kwa wananchi kuhusu umuhimu wa kuishi kwa upendo, mshikamano na kuvumiliana bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila, akisisitiza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wao, viongozi wa Sungusungu Wilaya ya Kahama wameleza kuwa wataendelea kushirikiana kwa karibu na Jeshi la Polisi, viongozi wa serikali za mitaa na wananchi katika kukabiliana na vitendo vya uhalifu pamoja na migogoro inayoweza kuvuruga utulivu wa jamii.

Aidha Wamemshukuru Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano na Amani Mkoa wa Shinyanga kwa kuandaa kikao hicho, wakisema kimewapa hamasa na mwelekeo mpya wa kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia sheria na maslahi ya wananchi.

Mkuu wa Polisi Jamii Wilaya ya Kahama ASP Emmanuel Rodgers  amesema ushirikiano kati ya Jeshi la Polisi, sungusungu na Kamati ya Amani ya Wilaya umeendelea kuimarika, jambo ambalo limechangia kudhibiti uhalifu na kuimarisha usalama wa wananchi.

Amesema sungusungu wamekuwa wakitoa taarifa muhimu za kiusalama na kushiriki doria za pamoja katika maeneo mbalimbali, huku Kamati ya Amani ikihamasisha wananchi kushiriki katika kulinda amani na kutatua migogoro kwa njia ya mazungumzo.


Post a Comment

Previous Post Next Post