Na Mapuli Kitina Misalaba
Jitihada za kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu
wa binadamu zimeendelea kuimarishwa mkoani Shinyanga kupitia utoaji wa elimu
kuhusu uhamiaji salama, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda haki za wanawake,
watoto, vijana na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.
Hayo yameelezwa na Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa
Shinyanga ambaye pia ni Ofisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, Rehema Edson, wakati wa
semina ya mafunzo kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji salama kwa
maafisa wa serikali.
Edson amesema usafirishaji haramu wa binadamu ni moja
ya changamoto zinazohitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali ili kuzuia wananchi,
hususan wasichana na wanawake, kutumbukia katika mikono ya wahalifu wanaotumia
ahadi za ajira na maisha bora kuwashawishi.
Amesema elimu ya uhamiaji salama ni nyenzo muhimu ya
kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi wanapotafuta ajira au fursa za
maisha, hivyo kupunguza uwezekano wa kudanganywa na kusafirishwa kinyume cha
sheria.
Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma
Ally, amesema mradi unaotekelezwa unalenga kuwainua wafanyakazi wa majumbani,
hasa wasichana, kwa kuwapa maarifa kuhusu haki zao pamoja na kuwaunganisha na
fursa za mafunzo na ajira zenye staha.
Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, wafanyakazi wa
majumbani wanawezeshwa kupata elimu kuhusu haki zao, mafunzo ya ujuzi kupitia
VETA, ajira zenye staha pamoja na elimu ya uhamiaji salama ili kupunguza
uwezekano wa kudhurumiwa au kuingia katika mazingira ya usafirishaji haramu wa
binadamu.
Mafunzo hayo yamewakutanisha maafisa wa serikali na
wadau mbalimbali kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu namna ya kutambua
viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu, kuimarisha ulinzi wa makundi
yaliyo katika mazingira hatarishi na kuongeza ushirikiano katika kuzuia uhalifu
huo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment