Usafirishaji haramu wa binadamu umeendelea kuwa
changamoto kubwa nchini, huku wasichana kutoka maeneo ya vijijini wakiwa
miongoni mwa waathirika wakuu kutokana na ahadi za ajira, elimu na maisha bora
ambazo baadaye huishia kuwaingiza katika mazingira ya unyonyaji na unyanyasaji.
Akizungumza kwa niaba ya katibu Tawala wa Mkoa wa
Shinyanga ambaye pia ni Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, Rehema Edson, wakati
akifungua semina ya mafunzo kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji
salama kwa maafisa mbalimbali wa serikali.
Mafunzo hayo yamefanyika kupitia mradi wa EmPoWedeD II
unaotekelezwa na mashirika ya CVM na APA kwa ushirikiano na CHODAWU pamoja na Wote
Sawa, kwa ufadhili wa Italian Agency for Development Cooperation.
Rehema amesema watoto wengi, hususan wasichana balehe
ambao walipaswa kuwa shuleni, wamekuwa wakidanganywa kwa ahadi za ajira na
kusafirishwa kwenda kufanya kazi za nyumbani katika makazi binafsi, ambako
hukumbana na mazingira magumu ya kazi na ukiukwaji wa haki zao.
Ameeleza kuwa baadhi ya changamoto wanazokutana nazo
ni kufanya kazi kwa saa nyingi bila mapumziko, kulipwa mishahara midogo au
kutolipwa kabisa, kunyimwa haki ya kupata elimu, pamoja na kukumbana na
unyanyasaji wa kimwili, kisaikolojia na unyonyaji wa kiuchumi.
Kwa mujibu wa Rehema, changamoto hiyo ni ngumu zaidi
kubainika kwa kuwa kazi nyingi hufanyika ndani ya nyumba binafsi, hali
inayowafanya waathirika kutotambulika kwa urahisi.
Aidha, amesema bado kuna watoto wanaoajiriwa katika
shughuli za kilimo, ufugaji, uchimbaji mdogo wa madini, biashara zisizo rasmi
na uuzaji wa bidhaa mitaani.
Ameongeza kuwa wahalifu wanaojihusisha na usafirishaji
haramu wa binadamu wamebadili mbinu zao, ambapo mbali na kutumia madalali wa
kawaida, sasa wanatumia teknolojia, mitandao ya kijamii, matangazo ya ajira za
uongo pamoja na mifumo isiyo rasmi ya uajiri ili kuwavuta waathirika.
Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma
Ally, amesema mradi wa EmPoWedeD II umeanza awamu ya pili baada ya mafanikio
yaliyopatikana katika utekelezaji wa awamu ya kwanza.
Amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka
mitatu kuanzia mwaka 2026, ukiweka mkazo katika kuwawezesha wasichana
wanaofanya kazi za nyumbani kupata mafunzo ya stadi kupitia vyuo mbalimbali,
pamoja na kuhakikisha wanapatiwa mikataba ya ajira na waajiri wao ili kulinda
haki zao.
Naye mwezeshaji wa semina hiyo kutoka Wizara ya Mambo
ya Ndani ya Nchi, Providence Simbila, amesema usafirishaji haramu wa binadamu
ni kosa la jinai kwa mujibu wa sheria za Tanzania na kwamba vitendo hivyo vina
viashiria vinavyoweza kutambuliwa mapema.
Amevitaja baadhi ya viashiria hivyo kuwa ni matumizi
ya ahadi za uongo kuhusu mishahara mikubwa au ajira nzuri, udanganyifu
unaolenga kuwashawishi waathirika kukubali kusafirishwa, pamoja na vitisho au
shinikizo vinavyolenga kuwanufaisha wahusika wa uhalifu huo.
Washiriki wa semina hiyo wamehimizwa kuendelea kutoa elimu kwa jamii, kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali na kuwahamasisha wananchi kutoa taarifa mapema kuhusu viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu ili kulinda haki na usalama wa makundi yaliyo katika mazingira hatarishi, hususan wanawake na watoto.
Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa, Rehema Edson.
mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma Ally


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254














































Post a Comment