
KATIKA hatua inayoashiria mabadiliko ya kimkakati katika usimamizi wa mazingira nchini, Serikali imeweka bayana mwelekeo mpya wa kuimarisha usafi wa mazingira kama nyenzo muhimu ya kupunguza magonjwa, kuongeza tija ya kiuchumi na kuharakisha maendeleo ya miji na vijiji.
Mkakati huo umeibuliwa jijini Dodoma leo July 2,2026 katika Kongamano la Kitaifa la Usafi wa Mazingira lililoambatana na uzinduzi wa mwongozo wa mpango jumuishi wa usimamizi wa huduma za usafi wa mazingira, ambalo limeweka msisitizo mpya wa kuunganisha huduma za usafi katika mfumo mmoja jumuishi unaolenga kuwafikia wananchi wote bila kuacha makundi yaliyo pembezoni.
Akizungumza katika kongamano hilo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu na Wenye Ulemavu), Profesa Palamagamba Kabudi,amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeweka mazingira kuwa agenda ya kimkakati inayohitaji utekelezaji wa kisera, kitaasisi na kijamii kwa pamoja.
Amesema usafi wa mazingira sasa hautazamwi tena kama shughuli za kawaida za kijamii, bali ni sekta yenye mchango wa moja kwa moja katika afya ya umma, ustahimilivu wa miji na ukuaji wa uchumi.
Prof.Kabudi amesisitiza kuwa mkakati wa sasa unalenga kuhakikisha huduma jumuishi za usafi wa mazingira zinaimarishwa ili kupunguza tofauti za upatikanaji kati ya mijini na vijijini, pamoja na kuongeza ufanisi wa mifumo ya ukusanyaji na utupaji taka.
“Tunajenga mfumo ambao unafanya usafi wa mazingira kuwa huduma ya msingi inayofika kwa kila Mtanzania,” amesema Kabudi.
Ameongeza kuwa mafanikio ya mkakati huo yanategemea mabadiliko ya tabia kwa wananchi sambamba na uwekezaji katika miundombinu ya kisasa ya usafi wa mazingira.
Aidha, ametumia kongamano hilo kumpongeza Rais Samia kwa kuendelea kuongoza ajenda ya nishati safi ya kupikia, akisema ni sehemu muhimu ya mkakati mpana wa kulinda mazingira na kupunguza uchafuzi unaotokana na nishati chafu.
Katika hoja ya kiufundi, Kabudi ameonya juu ya kuendelea kwa tabia ya utupaji taka kwenye mitaro ya maji ya mvua, akisema vitendo hivyo vinadhoofisha mifumo ya miji na kuongeza hatari ya mafuriko na magonjwa ya mlipuko.
Amesisitiza kuwa uwekezaji katika usafi wa mazingira ni sehemu ya mkakati wa taifa wa kulinda afya ya umma na kupunguza gharama za matibabu zinazotokana na magonjwa yanayohusiana na mazingira.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Fedha wa EWURA, Stanley Mahembe,aliyemwakilishi Mkurugenzi Mkuu amesema bado kuna pengo kubwa la kitaasisi katika usimamizi wa majitaka, akibainisha kuwa ni mamlaka 24 pekee kati ya 84 ndizo zilizo na mipango ya matibabu ya majitaka na tope la kinyesi.
Amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuharakisha utekelezaji wa mwongozo mpya wa usimamizi wa mazingira uliozinduliwa katika kongamano hilo.
Naye Naibu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya EWURA, Ngosi Mwihava, amesema kupitia bajeti ya shilingi trilioni 1.12 iliyopitishwa kwa ajili ya Wizara ya Maji, kuna matumaini makubwa ya kuimarisha ujenzi wa miundombinu ya maji taka na usafi wa mazingira, ili kuendana na lengo la Maendeleo Endelevu (SDG) namba 6 linalohusu upatikanaji wa maji safi na usafi wa mazingira kwa wote.
Kwa upande wake Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Maji na Mazingira, Kunti Majala, amesema changamoto za mazingira zinaendelea kuchangia vifo vinavyoweza kuzuilika, hivyo kuhitaji mkakati wa elimu na usimamizi kuimarishwa zaidi.
Awali Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Jabir Shekimweri, amesema ongezeko la kasi la watu katika mji wa Dodoma linahitaji mkakati madhubuti wa usafi wa mazingira unaoendana na ukuaji wa mji huo.
Kongamano hilo ni sehemu ya utekelezaji wa dira mpya ya taifa ya kuimarisha mifumo ya usafi wa mazingira, kwa lengo la kujenga miji salama, yenye afya na endelevu kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment