
NA DENIS MLOWE, IRINGA.
WAZIRI wa Ujenzi, Abdallah Ulega, amezindua rasmi Shule ya Sekondari Ugwachanya iliyopo Kata ya Mseke, Wilaya ya Iringa, huku akiipongeza Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuendelea kusogeza huduma za elimu karibu na wananchi na kuimarisha miundombinu ya maendeleo mkoani Iringa.
Akizungumza katika hafla hiyo, Ulega alisema ujio wake mkoani Iringa umetokana na maelekezo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuwafanya mawaziri kutembelea maeneo mbalimbali nchini ili kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo na kuhakikisha maelekezo ya serikali yanatekelezwa kwa ufanisi.
Alisema Rais Dr. Samia Suluhu Hassan amemtuma kuwafikishia wananchi wa Iringa salamu za upendo na shukrani kwa ushirikiano wanaoendelea kuonyesha katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo, huku akibainisha kuwa ameridhishwa na hatua kubwa iliyofikiwa katika sekta mbalimbali.
Ulega alisema ujenzi wa Shule ya Sekondari Ugwachanya ni ukombozi mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo kwani utapunguza umbali ambao wanafunzi walikuwa wakitembea kutafuta elimu ya sekondari, jambo litakaloongeza fursa za watoto wengi kuendelea na masomo.
Alisema mbali na elimu, serikali inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya kimkakati mkoani Iringa ikiwemo upanuzi wa Barabara ya Mlima Kitonga kutoka njia mbili hadi nne, ujenzi wa barabara ya mchepuo (Bypass) ya Iringa ili kupunguza msongamano wa magari, pamoja na ujenzi wa Uwanja wa Ndege wa Nduli ambao utapanua fursa za biashara, utalii na ajira.
“Wananchi wa Iringa wana kila sababu ya kujivunia maendeleo haya. Mkoa huu unaendelea kupaa kutokana na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alisema Ulega.
Aidha aliwataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja na mshikamano huku akisisitiza kuwa maendeleo yanaweza kudumu endapo kutakuwa na mazingira ya utulivu na ushirikiano.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, alisema ziara ya Waziri wa Ujenzi ni sehemu ya utaratibu wa serikali wa kufuatilia utekelezaji wa maagizo na maamuzi ya Rais katika sekta mbalimbali ikiwemo afya, elimu, maji na miundombinu.
Alisema serikali imeendelea kusimamia kwa karibu utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha fedha zinazotolewa na serikali zinatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwanufaisha wananchi.
Katika hafla hiyo, Waziri Ulega alimkabidhi cheti maalumu mwalimu aliyesimamia kwa karibu ujenzi wa shule hiyo, akieleza kuwa ni kutambua mchango wake mkubwa katika kuhakikisha mradi unakamilika kwa ubora na kwa wakati.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Iringa, Steven Mhapa, alisema ujenzi wa shule hiyo ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya viongozi wa halmashauri, madiwani na wataalamu, hali iliyowezesha mradi kukamilika bila changamoto kubwa.
Alisema shule hiyo imeleta ukombozi kwa watoto wa Ugwachanya na maeneo jirani ambao hapo awali walilazimika kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daud Yassin, alisema utekelezaji wa miradi mbalimbali unaonyesha kwa vitendo namna Ilani ya Uchaguzi ya CCM inavyoendelea kutekelezwa chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Alisema Kamati ya Siasa ya CCM Mkoa wa Iringa imeridhishwa na utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika wilaya zote za mkoa huo na kumpongeza Rais kwa kuendelea kuielekeza serikali kuwekeza katika sekta muhimu zinazogusa maisha ya wananchi.
Wananchi waliohudhuria uzinduzi huo walieleza kufurahishwa na kukamilika kwa shule hiyo, wakisema itasaidia kuongeza upatikanaji wa elimu, kupunguza gharama za usafiri kwa wanafunzi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika Kata ya Mseke na maeneo ya jirani.
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254.
Post a Comment