" GCI NA RESTLESS DEVELOPMENT WATOA MAFUNZO YA URAIA, UONGOZI, USHAWISHI NA UWAJIBIKAJI KWA VIJANA 50 SHINYANGA

GCI NA RESTLESS DEVELOPMENT WATOA MAFUNZO YA URAIA, UONGOZI, USHAWISHI NA UWAJIBIKAJI KWA VIJANA 50 SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Shirika la Green Community Initiatives (GCI), kwa kushirikiana na Restless Development, limetoa mafunzo ya uraia kwa vijana 50 kutoka kata mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa AU-EU Youth Voice Lab, unaolenga kuwajengea vijana uwezo wa kushiriki kikamilifu katika masuala ya kijamii, kiutawala na maendeleo ya jamii.

Katika mafunzo hayo, vijana wamefundishwa kuhusu dhana ya uongozi, aina za uongozi na sifa muhimu anazopaswa kuwa nazo kiongozi anayelenga kuleta mabadiliko chanya katika jamii.

Mwakilishi wa shirika la Restless Development Cecilia Msangwa kutoka shirika la YAWE ambaye alikuwa sehemu ya wawezeshaji katika mafunzo hayo ameeleza kuwa uongozi haupaswi kuhusishwa pekee na mtu anayeshika nafasi rasmi ya kisiasa au kiutawala, bali kila kijana ana nafasi ya kuwa kiongozi katika jamii yake kwa kuanzisha mawazo mapya, kuhamasisha wengine na kushiriki katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.

Vijana pia wamepewa uelewa kuhusu umuhimu wa kuwa na viongozi wenye maono, wanaowajibika na wanaoweza kusikiliza mahitaji ya wananchi huku wakihimizwa kutumia nafasi walizonazo kushiriki katika shughuli za maendeleo badala ya kusubiri kupewa nafasi za uongozi.

Peter Joseph kutoka Shirika la YAWE, ambaye naye alishiriki kwa niaba ya Restless Development amewasilisha mada mbalimbali ikiwemo uwajibikaji, ambapo vijana wameelezwa kuwa raia wana wajibu wa kufuatilia na kuelewa namna shughuli za maendeleo zinavyotekelezwa katika maeneo yao.

Katika sehemu ya utafiti, washiriki wamefundishwa umuhimu wa kukusanya taarifa sahihi kabla ya kufanya maamuzi au kutoa hoja kuhusu jambo lolote linalohusu jamii.

Mada ya ushawishi pia imepewa nafasi katika mafunzo hayo, ambapo vijana wamefundishwa namna ya kutumia hoja, ushahidi na njia mbalimbali za mawasiliano kushawishi mabadiliko chanya katika jamii.

Kwa upande wake, Afisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Salome Komba, ameyapongeza mashirika ya GCI na Restless Development kwa kuandaa mafunzo hayo, akisema kuwa vijana ni sehemu muhimu ya jamii na wanapaswa kupewa nafasi na maarifa yatakayowawezesha kushiriki katika maendeleo.

Salome amewasisitiza vijana kutumia elimu waliyoipata katika mafunzo hayo kwa vitendo, hususan kwa kushiriki katika shughuli za kijamii, kufuatilia masuala yanayowahusu na kutoa mawazo yanayoweza kusaidia kuboresha maisha ya wananchi.

Naye Afisa Vijana wa Manispaa ya Shinyanga, Enea Boniface, amesisitiza umuhimu wa vijana kutumia fursa za mafunzo kama hayo kujenga uwezo wao na kuongeza ushiriki wao katika masuala ya maendeleo.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo, Maryciana William kutoka Shirika la Green Community Initiatives (GCI), amesema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea vijana uelewa na uwezo wa kutumia maarifa waliyopewa katika kushiriki kwenye mijadala na shughuli mbalimbali zinazohusu maendeleo ya jamii.

Amesema GCI imekuwa ikitambua umuhimu wa vijana katika kujenga jamii yenye ushiriki, uwajibikaji na maendeleo, hivyo mafunzo hayo yameandaliwa ili kuwapa vijana maarifa ambayo wataweza kuyatumia katika maeneo yao.

Baadhi ya vijana walioshiriki katika mafunzo hayo, akiwemo Emmanuel Robert, Mhoja Ibengwe, Eliya Bahame na Neema Songela, wameyashukuru mashirika ya GCI na Restless Development kwa kuwapa nafasi ya kupata elimu zaidi kuhusu masuala ya uraia na uongozi.

Aidha, wameahidi kwenda kuwa mabalozi wazuri kwa kuwafikishia vijana wengine elimu waliyoipata, ili maarifa hayo yasiishie kwa washiriki 50 pekee, bali yaweze kuwafikia vijana wengi zaidi ndani ya Manispaa ya Shinyanga.

Mwakilishi wa Shirika la Restless Development, Cecilia Msangwa kutoka YAWE, akizungumza wakati wa mafunzo ya uraia mjini Shinyanga, akisisitiza kuwa uongozi si lazima uhusishwe na mtu anayeshika nafasi rasmi ya kisiasa au kiutawala, bali kila kijana ana nafasi ya kuwa kiongozi katika jamii yake.

Mwakilishi wa Shirika la Restless Development, Cecilia Msangwa kutoka YAWE, akizungumza wakati wa mafunzo ya uraia mjini Shinyanga, akisisitiza kuwa uongozi si lazima uhusishwe na mtu anayeshika nafasi rasmi ya kisiasa au kiutawala, bali kila kijana ana nafasi ya kuwa kiongozi katika jamii yake.Vijana 50 wakishiriki mafunzo ya uraia yaliyoandaliwa na GCI kwa kushirikiana na Restless Development, wakijengewa uwezo katika uongozi, uwajibikaji, utafiti na ushawishi.



 




Post a Comment

Previous Post Next Post