" KOREA KUSINI KUSHIRIKIANA NA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUKAMILISHA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

KOREA KUSINI KUSHIRIKIANA NA CHUO CHA UFUNDI ARUSHA KUKAMILISHA DIRA YA MAENDELEO YA TAIFA 2050

Na Seif Mangwangi, Arusha

SERIKALI ya Korea Kusini imesema itaendelea kushirikiana na chuo cha ufundi Arusha (ATC), katika nyanja ya ufadhili wa masomo kwa walimu na wanafunzi Ili kufanikisha malengo ya Serikali kupitia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Balozi wa Korea Kusini Nchini Tanzania,  Bi. Eunje Ahn ameyasema hayo Jana 31 Julai 2026, alipofanya ziara ya kikazi katika chuo cha ufundi Arusha yenye lengo la kukagua maendeleo ya programu inayofadhiliwa na Serikali yake ya Innovative Energy Education Program (IEEP).


Amesema programu hiyo ambayo imekuwa ikileta walimu kutoka nchini Korea Kusini kuja kufundisha walimu na wanafunzi katika chuo hicho imefanya vizuri sana na lengo lake lililokusudiwa limetimia ambapo vijana wengi wamepata ujuzi na ajira.

" Serikali ya Korea Kusini itaendelea kuendeleza ushirikiano na chuo cha ufundi Arusha (ATC), katika fani ya uhandisi wa mitambo na kuhakikisha malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 yanatekelezwa na yanafikiwa kupitia chuo cha ATC, " amesema.


Balozi Ahn amesema ameridhishwa na ushirikiano uliokuwepo kati ya Serikali ya Tanzania na Korea Kusini kupitia chuo hicho cha ufundi na kwamba ufadhili ilioutoa miaka saba iliyopita na kutarajiwa kumalizika mwakani umeleta mafanikio makubwa.


Amesema vijana wengi wa kitanzania wamepata ujuzi na ajira kupitia programu hiyo na kwamba amefurahishwa zaidi na ubunifu ambao umekuwa ukifanywa na vijana hao Kwa kubuni teknolojia mbalimbali.

" Chuo kikuu cha Hanyang na Seoul ni miongoni mwa vyuo ambavyo vimekuwa vikishirikiana na chuo hiki cha ufundi Arusha kwa walimu na wanafunzi wake kubadilishana ujuzi, na Leo tumefika hapa ATC kuona maendeleo ya programu tuliyokuwa tukiifadhili  kwa miaka saba kuanzia mwaka 2020 na inaelekea ukingoni kumalizika mwakani2027, nimefurahishwa sana na maendeleo mazuri ya programu hii," amesema.

Mkuu wa chuo cha ufundi Arusha (ATC), Profesa Chacha Mussa amesema Serikali ya Korea imekuwa msaada mkubwa chuoni hapo ambapo imekuwa ikifadhili walimu na wanafunzi wanaosomea kozi ya ufundi.

" Ushirikiano wetu na Korea Kusini kupitia vyuo vikuu viwili vya ufundi nchini huko ulipelekea sisi kuanzisha kozi ya Mechatronics and material engineering, ambayo ni ya kwanza nchini na Afrika Mashariki, ni kozi inayotoa waendesha mitambo kwenye viwanda," amesema.


Amesema kozi hiyo ilianzishwa baada ya serikali kuamua kujikita katika kuanzisha viwanda na hivyo chuo hicho kuanza mchakato wa kutayarisha vijana watakaoendesha mitambo viwandani.

Mkurugenzi wa kampuni ya I- tech Tanzania na Meneja programu ya Innovative Energy Education (IEEP), inayofadhiliwa na Serikali ya Korea Kusini, Dkt Wob Lee amesema Balozi amefurahishwa na mafanikio ya programu hiyo.

Balozi Ahn ametembelea madarasa, maabara na karakana zinanazotumiwa na wanafunzi wa programu hiyo na kuona bunifu mbalimbali zinazoendelea kufanywa, pamoja na karakana kubwa inayoendelea kujengwa ambayo itatumika Kwa kufundishia pamoja na uzalishaji.


Post a Comment

Previous Post Next Post