" MSIGWA: MICHEZO NI DARAJA LA URAFIKI KATI YA TANZANIA NA CHINA

MSIGWA: MICHEZO NI DARAJA LA URAFIKI KATI YA TANZANIA NA CHINA

 

Na Mwandishi Wetu 
Dar es Salaam, Tanzania – Jumamosi, 1 Agosti 2026: Katibu Mkuu, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Gerson Msigwa amefungua rasmi Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Jamii ya Wachina nchini Tanzania, yaliyodhaminiwa na Stanbic Bank kwa Shilingi milioni 30.

Hafla ya ufunguzi ilifanyika katika Viwanja vya Don Bosco, Namanga, ambapo hundi ya udhamini ilikabidhiwa mbele ya Balozi wa Jamhuri ya Watu wa China nchini Tanzania, Mheshimiwa Chen Mingjian.

Mbali na kuwa mdhamini mkuu, Stanbic Bank pia imeshiriki kama mshindani kupitia timu yake ya mpira wa kikapu. Ushiriki huo unaonyesha namna uhusiano kati ya benki hiyo na jamii ya Wachina nchini ulivyoendelea kuimarika kwa miaka mingi, huku michezo ikitumika kama daraja la kuimarisha mahusiano ya kibiashara, mshikamano wa kijamii na kubadilishana tamaduni.

Mashindano hayo yameendelea kuwa jukwaa muhimu linalowaunganisha wafanyabiashara wa Kichina, viongozi wa jamii na wadau mbalimbali katika mazingira ya urafiki na ushirikiano kupitia michezo. Kwa Stanbic Bank, ni fursa ya kuimarisha mahusiano na wateja pamoja na kuwapa wafanyakazi wake nafasi ya kuiwakilisha benki kupitia timu yake.
Akizungumza kabla ya ufunguzi wa mashindano hayo, Mkuu wa Kitengo cha Uwekezaji (Corporate and Investment Banking) wa Stanbic Bank Tanzania, Ester Manase, alisema udhamini huo unaakisi dhamira ya benki ya kujenga ushirikiano wa kweli unaovuka huduma za kifedha pekee.

"Kwa miaka mingi, mashindano haya yamekuwa moja ya majukwaa muhimu kwetu katika kuimarisha mahusiano na jamii ya Wachina nchini Tanzania kwa sababu tunaamini ushirikiano imara hujengwa kupitia uzoefu wa pamoja, si miamala ya kifedha pekee. Dhamira hiyo ndiyo msingi wa kazi yetu kupitia Standard Bank Group, ushirikiano wetu na ICBC pamoja na dawati letu maalum la huduma kwa wafanyabiashara wa Kichina, ambalo linaunganisha biashara zao na fursa zilizopo Tanzania na barani Afrika," alisema.

Aliongeza kuwa: "Udhamini wetu wa Shilingi milioni 30 una maana kubwa zaidi ya kugharamia mashindano. Kwa kushiriki kama mdhamini na pia mshindani, tunaonyesha kuwa ushirikiano wetu ni wa dhati na wa muda mrefu. Tunaendelea kujizatiti kuunga mkono mipango inayokuza mshikamano wa jamii, kubadilishana tamaduni na maendeleo ya pamoja, na tunajivunia kushirikiana tena na jamii ya Wachina mwaka huu."

Kwa upande wake, Mgeni Rasmi Bw. Gerson Msigwa aliipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kuunga mkono mashindano hayo na kueleza kuwa michezo imeendelea kuwa daraja muhimu la kuimarisha urafiki kati ya Tanzania na China.

"Uhusiano kati ya China na Tanzania una historia ndefu na unaendelea kuimarika kupitia matukio kama haya ambapo michezo inatuunganisha katika roho ya urafiki na kuheshimiana. Naipongeza Stanbic Bank kwa kuendelea kudhamini mashindano haya kwa miaka mingi. Ushirikiano wa namna hii kati ya sekta binafsi na jamii unachangia kuimarisha mahusiano kati ya wananchi wa mataifa yetu mawili na kudhihirisha urafiki wa kudumu uliopo kati ya China na Tanzania," alisema.

Mashindano ya Mpira wa Kikapu ya Wachina yameendelea kuwa jukwaa muhimu la kujenga mitandao ya biashara, kuimarisha mahusiano na kukuza kubadilishana uzoefu wa kitamaduni kati ya wadau kutoka Tanzania na China. Kupitia ushiriki wake endelevu, Stanbic Bank inaendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuunga mkono mipango yenye manufaa ya kijamii na inayowaunganisha watu kupitia malengo ya pamoja.

Kadri ushirikiano huo unavyoendelea kukua, Stanbic Bank itaendelea kuimarisha uhusiano wake na jamii ya Wachina nchini Tanzania pamoja na kuunga mkono majukwaa yanayochochea ushirikiano, maelewano na maendeleo ya pamoja.

Post a Comment

Previous Post Next Post