Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, amewakaribisha wawekezaji kutumia fursa zinazoendelea kukua mkoani Kusini Unguja,kufuatia maendeleo ya miundombinu, huduma za jamii na shughuli za kiuchumi.
Akihutubia katika kilele cha Tamasha la Kizimkazi, 2026 leo tarehe 14 Agosti, 2026, Rais Dkt. Samia ameeleza kuwa Wilaya ya Kusini imebadilika kwa kasi katika miaka ya hivi karibuni, ikichochewa na ongezeko la uwekezaji na miradi ya maendeleo.
Rais Dkt. Samia amesema fursa hizo, pamoja na uwekezaji katika miundombinu, zimeendelea kuvutia shughuli mpya za kiuchumi, akisisitiza wajibu wa viongozi
kuhakikisha uwekezaji huo unaacha manufaa ya kudumu kwa wananchi.
Aidha, ametoa rai kwa wawekezaji kutumia fursa mpya zitakazoambatana na ujenzi wa uwanja wa michezo Kusini Unguja, unaotarajiwa kutumika katika mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Samia amewataka wananchi kuendelea kulinda amani, umoja, usalama na utulivu wa nchi, akibainisha kuwa shughuli za uwekezaji, utalii, biashara, ajira na huduma za jamii haziwezi kustawi katika mazingira ya vurugu.
“Amani ndiyo kila kitu katika maisha yetu,” amesema Rais Dkt. Samia, akiwataka Watanzania kudumisha umoja na kuuenzi Muungano kwa maslahi ya kizazi cha sasa na kijacho.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amelitaja tamasha hilo kuwa jukwaa muhimu la kutangaza Kizimkazi, kuhifadhi mila na utamaduni na kuchochea maendeleo.
Amesema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, itaendelea kusimamia utunzaji na uendelezaji wa miradi iliyotokana na Tamasha la Kizimkazi ili iweze kudumu na kutoa
huduma kwa wananchi.
Akiwasilisha salamu za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Mhe. Hamida Mussa Khamis, amesema uwekezaji uliofanyika katika miaka ya hivi karibuni umeibadilisha Kizimkazi, na kunufaisha makundi mbalimbali ya wananchi.
Ametaja sehemu ya mafanikio hayo kuwa elimu ya usimamizi na mitaji kwa Wajasiriamali wadogo kutoka taasisi za fedha nchini, fursa katika biashara ya utalii kwa vijana, pamoja na kupanuka kwa shughuli za uvuvi zilizoletwa na uwekezaji katika uchumi wa buluu.
Tamasha la Kizimkazi, lililoanzishwa mwaka 2016, limepanuka na kuwa jukwaa linalounganisha miradi ya maendeleo, biashara, uwekezaji, michezo, utalii na shughuli za kijamii Kusini Unguja.
Kupitia tamasha hilo, miradi mbalimbali ya maendeleo iliwekewa mawe ya msingi na kuzinduliwa, katika sekta za elimu, afya, maji, barabara, makazi, na burudani na michezo, huku shughuli zake zikivuta wafanyabiashara, wawekezaji na wageni kutoka Zanzibar, Tanzania Bara na nje ya nchi.
Sherehe hizo, sambamba na washiriki wengine, zilihudhuriwa pia na wageni kutoka nje ya nchi, akiwemo Rais wa Zamani wa Jamhuri ya Guinea-Bissau, Mheshimiwa Umaro Sissoco Embaló.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment