" REA YAELEZA UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA NISHATI SAFI KWENYE TAMASHA LA KIZIMKAZI MWAKA 2026

REA YAELEZA UTEKELEZAJI WA MKAKATI WA NISHATI SAFI KWENYE TAMASHA LA KIZIMKAZI MWAKA 2026



Kizimkazi, Unguja 

Wakala wa Nishati Vijijini (REA) umefanikiwa kusambaza takribani mitungi laki saba ya gesi ya kupikia (LPG) nchini kote, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa kasi wa Mkakati wa Kitaifa wa Nishati Safi ya Kupikia.

Hayo yameelezwa na Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Jadidifu kutoka REA, Mhandisi, Advera Mwijage, wakati akizungumza kwenye mdaharo maalum uliofanyika katika Tamasha la Kizimkazi mkoani wa Kusini Unguja, Zanzibar; Mhandisi Advera alimwakilisha Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy.

Mhandisi Advera alieleza kuwa mafanikio hayo yametokana na uwezeshaji mkubwa kutoka kwa Serikali ya Awamu ya Sita, pamoja na uwepo wa vyanzo vingi vya nishati nchini. Alibainisha kuwa REA ilitumia majukwaa ya Waheshimiwa Wabunge kusambaza mitungi hiyo ili kuwafikia wananchi wa ngazi ya chini na kutoa elimu ya matumizi ya nishati hiyo.


"Miradi hii ikiwemo ya gesi ya kupikia (LPG) na majiko banifu inatolewa kwa njia ya ruzuku. Bila ruzuku kwa wananchi wa vijijini, mabadiliko ya kuelekea nishati safi yatachukua muda mrefu sana," alisema Mhandisi Advera.

Kuhusu utunzaji wa mazingira, Mhandisi Advera alisema REA imeanzisha mradi wa kusambaza majiko banifu ili kupunguza kasi ya uharibifu wa misitu. Inakadiriwa kuwa takribani hekta 470,000 za misitu hukatwa kila mwaka nchini kwa ajili ya kuni na mkaa.

Ili kukabiliana na changamoto hiyo, REA imeshirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kufungua viwanda vya kuzalisha mkaa mbadala maeneo ya vijijini, tofauti na hapo awali ambapo viwanda hivyo vilikuwa vimejificha mijini. Hatua hiyo imefanya mkaa mbadala kupatikana kwa gharama nafuu vijijini.


Katika hatua nyingine, REA kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), imefanikiwa kuunganisha jumla ya wateja 1,001 wa majumbani na taasisi kwenye mkuza wa mabomba ya Gesi Asilia katika mikoa ya Lindi na Pwani.

Mhandisi Advera alitoa wito kwa wananchi ambao bado hawajafikiwa na miradi hiyo kuendelea kuwa wavumilivu, kwani utekelezaji unaenda kwa awamu kulingana na ukomo wa bajeti ya serikali. Lengo kuu la serikali ni kuhakikisha zaidi ya asilimia 80 ya Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia.


Mdaharo huo ulihudhuriwa na viongozi waandamizi wa sekta ya nishati, akiwemo Waziri wa Nishati, Mhe. Deogratius Ndejembi, Naibu Waziri Mhe. Salome Makamba, na Katibu Mkuu (Umeme na Nishati Jadidifu) Mhandisi Felchesmi Mramba.

Viongozi wengine waliohudhuria na kushiriki ni pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa TANESCO, Bw. Lazaro Twange, huku mdaharo huo ukianzishwa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mstaafu, Mhe. Doto Biteko, Mbuge wa Jimbo la Bukombe.

SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post