Na Mapuli Kitina Misalaba
Sekta ya uchimbaji mdogo wa dhahabu katika Mkoa wa
Shinyanga imeendelea kuwa tegemeo muhimu la uchumi wa wananchi wengi, hususan
katika migodi ya Mwakitolyo na Nyandolwa ambapo kupitia migodi hiyo, mamia ya
wakazi wamepata ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja, biashara
ndogondogo zimeimarika, na familia nyingi zimeanza kushuhudia mabadiliko ya
kiuchumi.
Hata hivyo, nyuma ya mchango huo wa kiuchumi kuna
hatari kubwa inayowakabili wachimbaji, inayochangiwa kwa kiasi kikubwa na
ukosefu wa elimu ya haki za msingi za mfanyakazi, kanuni za usalama kazini,
pamoja na uwajibikaji hafifu wa waajiri na mamlaka husika.
Uchunguzi uliofanywa na Misalaba Media unaonesha kuwa
idadi kubwa ya wachimbaji wadogo na vibarua wa migodini hawana uelewa wa
kutosha kuhusu haki zao pindi ajali zinapotokea na kwamba wengi hawajui
taratibu za fidia, bima, msaada wa dharura, wala namna ya kushirikiana na inspekta
wa migodi katika masuala ya usalama.
Katika kipindi cha mwaka 2022 hadi 2025, migodi ya
Nyandolwa na Mwakitolyo mkoani Shinyanga imerekodi jumla ya watu 72 waliokumbwa
na ajali kubwa migodini. Kati yao, watu 36 wamethibitishwa kufariki dunia,
mmoja (1) hajapatikana, na 11 wamejeruhiwa, huku 27 wakinusurika katika matukio
hayo.
Katika mgodi wa Nyandolwa uliopo kata ya Mwenge kwenye
leseni ya kikundi cha Wachapakazi Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, ajali ya
mwaka 2022 ilihusisha watu 30, ambapo watu sita (6) walifariki dunia sawa na
asilimia 20 ya waathirika wote, huku watu 24 wakinusurika.
Hata hivyo, ajali ya Agosti 11, 2025 katika mgodi huo
wa Nyandolwa ilihusisha watu 25, ambapo 21 walifariki dunia, watatu (3)
waliokolewa wakiwa hai na mmoja hajapatikana, ikiwa ni kiwango cha vifo cha
takribani asilimia 84 na kwamba Desemba 2025 kuliripotiwa kifo cha mtu mmoja
(1) katika ajali nyingine.
Katika mgodi wa Mwakitolyo, Mei 17, 2025 watu 17
waliathirika katika ajali Mwakitolyo namba 2, ambapo watu sita (6) walifariki
dunia na 11 kujeruhiwa, sawa na kiwango cha vifo cha asilimia 35. Tukio lingine
mwishoni mwa mwaka 2025 katika Kitalu namba 15 lilisababisha vifo vya watu
wawili (2) ambao miili yao haikupatikana.
Katika ajali hiyo, Samwel Makenzi Chembanya, kijana
mchimbaji mdogo, alipoteza maisha baada ya kuangukiwa na kifusi. Familia yake
ilieleza kuwa haikuwa na uelewa wa masuala ya fidia wala msaada wa dharura,
hali iliyowaacha katika changamoto kubwa za kiuchumi na kijamii.
Mchimbaji mdogo Kulwa Mpelwa alisema kuwa licha ya
kufanya kazi mgodini kwa muda mrefu, hajawahi kupatiwa mafunzo rasmi ya usalama
kazini, hali inayomfanya kufanya kazi bila uelewa wa nini cha kufanya endapo
atapata ajali au jeraha akiwa kazini.
Mchimbaji Bwana Mpiga Mhamal alisema baadhi ya duara
hazifungwi nguzo ipasavyo, huku wengine wakivamia duara bila kufuata taratibu
ili kupata dhahabu kwa haraka huku Kandya Ndutu akidai kuwa ukaguzi wa inspekta
haufanyiki mara kwa mara, na wakati mwingine taarifa za hatari hazifiki kwa wamiliki
wa migodi kwa wakati.
Kwa upande wake, Boniface Misong’oni, alieleza kuwa
hata elimu ya haki za mfanyakazi haijawahi kuwafikia wachimbaji wengi, jambo
linalowaacha katika hatari kubwa wanapopatwa na ajali.
Akizungumza na Misalaba Media, Mwenyekiti wa Kijiji
cha Mwakitolyo namba 2, Bwana Chongo Lutenganija, alieleza kuwa kumekuwepo na
ajali nyingine ambazo haziripotiwi rasmi kwa mamlaka husika, licha ya
kusababisha vifo vya wachimbaji mmoja mmoja au wawili, hali inayozuia hatua za
kudumu kuchukuliwa.
Alishauri kuwa ukaguzi wa mara kwa mara katika maduara
unapaswa kuwa wa lazima, huku hatua za haraka zikichukuliwa pale hatari
zinapobainika ili kuzuia ajali kabla hazijatokea.
Kwa upande wa Nyandolwa, Mwenyekiti wa Kijiji cha
Mwongozi, Bwana Mange Didas, alisema ajali migodini zimekuwa mzigo mkubwa kwa
jamii, hasa kwa familia zinazopoteza wapendwa wao bila fidia ya haraka wala
msaada wa kisaikolojia na kwamba alipendekeza elimu ya mara kwa mara kuhusu
usalama kazini pamoja na haki zao itolewe kwa vitendo.
Kwa upande wa wafanyakazi wa pembezoni, akina mama
wanaobonda mawe ya dhahabu walisema nao wanakabiliwa na hatari kubwa kutokana
na ukosefu wa elimu ya usalama na mazingira machafu ya kazi.
Christina alisema hafanyi kazi kwa kutumia mafunzo
rasmi ya usalama, bali hutegemea uzoefu wa muda mrefu na mbinu za jadi
kujilinda. Stella, anayefanya kazi ya kuponda mawe naye alisema ajali
ndogondogo zimekuwa zikimuathiri kiafya na kiuchumi kutokana na kukosekana kwa
elimu ya usalama kazini.
Mkazi wa Mwakitolyo, Esther Jackson, alisema ajali
migodini huathiri moja kwa moja biashara ndogondogo na ustawi wa familia nyingi
huku Mchungaji Paul James akisema vifo
na majeraha migodini huacha maumivu makubwa ya kijamii na kiuchumi pale msaada
wa dharura na fidia unapokosekana.
Inspekta wa migodi Samson Jelemiah alisema changamoto
kubwa ni kupuuzwa kwa maelekezo ya usalama wanayotoa kwa wamiliki wa migodi.
Dotto Seleman alisema baadhi ya inspekta hukumbana na vitisho wanapotekeleza
majukumu yao.
Clement Samson alisema mafunzo ya mara kwa mara kwa
inspekta bado hayatoshi, huku Mussa Bilia akieleza kuwa bila ulinzi wa
kisheria, inspekta hushindwa kusimamia usalama ipasavyo.
Mjiolojia kutoka Ofisi ya Afisa Madini Mkoa wa
Shinyanga, James Kibiti Muiko, alisema Tume ya Madini ina jukumu la kusimamia
shughuli zote za uchimbaji ikiwemo masuala ya usalama, lakini tofauti ya
uchimbaji mdogo na wa kati husababisha changamoto kubwa zaidi katika migodi
midogo.
Migodi ya Mwakitolyo na Nyandolwa imeendelea kuwa
mhimili wa uchumi wa Mkoa wa Shinyanga, lakini ajali za mara kwa mara
zinaonesha gharama kubwa ya maendeleo hayo kwa maisha ya wachimbaji.
Wachimbaji wagodo walipendekeza elimu ya mara kwa mara
kuhusu haki zao na kanuni za usalama itolewe, vifaa vya kujikinga vitolewe kwa
kila mfanyakazi, ukaguzi wa mara kwa mara ufanyike na upatikanaji wa fidia na
bima uboreshwe.
Mdau wa shughuli za uchimbaji madini kutoka kata ya
Salawe, Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, Hosea Marco, alitoa wito kwa
Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuongeza uwepo wake katika
maeneo ya migodi kwa kutoa elimu na kufanya ufuatiliaji wa karibu, hatua
itakayosaidia kupunguza vitendo vya rushwa na kuimarisha usalama kwa wachimbaji
wadogo.
Diwani wa Kata ya Mwenge Halmashauri ya Wilaya ya
Shinyanga, Mhe. Raphael Maharage alisema ili kupunguza ajali katika migodi ya
wachimbaji wadogo ni muhimu kwa inspekta wa migodi kufanya ukaguzi wa mara kwa
mara na kuchukua hatua kwa duara zinazobainika na dosari.
Katibu wa Wanawake Wachimbaji Taifa, kupitia Shirikisho
la Vyama vya Wachimbaji Wadogo wa Madini Tanzania (FEMATA), Evelyne Cleophace
Nzinza alisisitiza kuwa inspekta wanapaswa kufanya kazi kwa uadilifu na kuweka
mbele usalama wa wachimbaji ikiwemo kuchukua hatua stahiki pale hatari
inapobainika.
Mrakibu Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa
wa Shinyanga, ambaye pia ni Kaimu Kamanda wa jeshi hilo mkoani humo, Thomas
Majuto, alisema jeshi hilo linashauri uchimbaji ufanyike kwa mtindo wa mteremko
wa nyuzi 30 hadi 45 (horizontal angle), kwani njia hiyo hurahisisha
utengenezaji wa njia za pembeni kwa ajili ya kufikia eneo la tukio wakati wa
ajali, tofauti na mtindo wa kuchimba wima moja kwa moja chini ambao huongeza
hatari na kuathiri upatikanaji wa njia za uokoaji.
Amezikumbusha mamlaka za kisekta kuwasikiliza na
kuwasimamia kwa karibu wachimbaji wadogo, akieleza kuwa mara nyingi hutanguliza
tamaa ya kufikia madini bila kuzingatia usalama wa maisha yao, na wakati
mwingine hulazimisha kuingia maeneo yasiyo salama, jambo linaloweza kusababisha
ajali.
Majuto ametoa wito kwa wachimbaji kutambua kuwa
usalama huanza kabla ya shughuli za uchimbaji kuanza, na kusisitiza kuwa
mamlaka za usalama, ikiwemo OSHA, zinapaswa kuendelea kufanya ziara za mara kwa
mara migodini kwa ajili ya kutoa elimu na miongozo ya kitaalamu itakayosaidia
kupunguza ajali na madhara.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini Shinyanga,
Mhandisi Noel Baraka, alisema kwa mujibu wa kanuni za usalama, umbali kati ya
duara na duara haupaswi kupungua mita kumi ambapo Ofisi ya Madini itaendelea
kusimamia Kanuni za Usalama na Utunzaji wa Mazingira Mahali pa Kazi za mwaka
2010, ambazo zinataka umbali huo uzingatiwe.
Mhandisi Baraka alisema iwapo itabainika kuwa maduara
yapo karibu kuliko inavyotakiwa, hatua za kusimamisha leseni ya eneo husika
zitachukuliwa huku akieleza kuwa ukaguzi unaendelea katika maeneo mengine ili
kuzuia ajali kama iliyotokea Nyandolwa.
Akitoa wito kwa wachimbaji wadogo, alisema wanapaswa
kufuata sheria na kanuni za usalama bila shuruti, kuzingatia upangaji sahihi wa
maduara kwa mujibu wa maelekezo ya maafisa wa madini, na kutumia baruti kwa
kufuata taratibu. Pia aliwataka kutoa taarifa mapema pindi wanapobaini dalili
za hatari ili hatua stahiki zichukuliwe kabla ya kutokea kwa majanga makubwa.
MWISHO


SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254














































Post a Comment