Na Beda Msimbe Bsky Media
Mwanachama wa Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) ana nafasi ya hiari ya kuamua iwapo anataka sehemu ya mkupuo wake igeuzwe na kuongezwa kwenye malipo yake ya kila mwezi badala ya kuchukua fedha taslimu za mkupuo kwa pamoja, kutegemeana na utaratibu unaomfaa zaidi.
Hayo yalielezwa na Afisa wa PSSSF, Bw.Mohammed Nyallo akijibu swali la Mwandishi wa gazeti la Mwananchi, Elizabeth Edward, aliyetaka ufafanuzi kama mwanachama anapofikia ukomo wa ajira ana uwezo wa kuchagua mfumo wa kulipwa mafao yake kati ya malipo ya kila mwezi na mkupuo.
Alisema pamoja na pamoja na ukweli kuwa malipo ya mwanachama aliyestaafu hufanyika kwa kuzingatia fomula maalum au kikokotoo kinachompa haki mwanachama kupata mkupuo pamoja na malipo ya kila mwezi hadi ukomo wa maisha yake, mwanachama anaweza kuamua kuongeza kiwango cha malipo ya mwezi kwa kuachia sehemu ya malipo yake ya mkupuo.
Awali Nyallo wakati akiwasilisha mada kuhusu mafao mbalimbali yanayotolewa na PSSSF na jinsi ya kuyaomba, wakati wa mafunzo ya siku mbili kwa waandishi wa habari yaliyoandaliwa na Mfuko huo na kufanyika kwenye jengo la PSSSF commercial complex barabara ya Sam Nujoma jijini Dar es salaam hivi karibuni, alisema pensheni ya mkupuo ya miezi 36, inatoa fursa kwa mwanachama anapofikia ukomo wa utumishi wake kulipwa kiasi maalum cha fedha za mkupuo kwa mpigo kinachokokotolewa kwa kuzingatia misingi na fomula rasmi ya mfuko.
Akifafanua kuhusu pensheni alisema:"Pensheni itakayotumika kulipia ni pensheni ya Mfuko peke yake iliyokokotolewa kwa kuzingatia kipindi au vipindi vyake vya utumishi. Aidha malipo yote ya pensheni yaliyolipwa baada mstaafu kufariki yatakatwa kwenye mkupuo wa pensheni ya miezi 36."
Malipo haya pia yanalenga kumpatia mstaafu mtaji au fedha za kuanzia maisha ya uraiani mara tu anapoacha kazi, jambo ambalo humwezesha kukabiliana na gharama za awali za maisha ya kustaafu huku akiendelea kupokea malipo yake ya kila mwezi.
Aidha katika mada yake alisisitiza dhamira ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) kendelea kuboresha ustawi wa wanachama kupitia utekelezaji rasmi wa huduma mpya nne za mafao zilizozinduliwa chini ya Waraka Namba 1 wa mwaka 2025 na kuhakikisha kuwa waajiri hawacheleweshi malipo ya wafanyakazi wao katika mfuko. .
Akifafanua Nyallo alisema maboresho hayo, yanayolenga kuleta tija kubwa na kupunguza changamoto za kiuchumi kwa wastaafu, yanajumuisha uhuishaji wa pensheni kwa asilimia mbili (2%), kuwekwa kwa kiwango cha chini cha pensheni cha Shilingi 250,000, pensheni ya mkupuo ya miezi 36, pamoja na kuanzishwa kwa fao la msaada wa mazishi.
Akizungumzia fao la msaada wa mazishi Nyallo amesema limekuja kama nguzo muhimu ya kutoa mkono wa pole na kupunguza mzigo mkubwa wa kifedha unaoweza kuikuta familia pale ambapo mwanachama anapopatwa na msiba.
"Fao hili linalipwa baada ya kupokea taarifa ya kifo cha mstaafu aliyekuwa akilipwa na Mfuko Pensheni ya Uzeeni au Ugonjwa.
Fao hili linatakiwa kuombwa ndani ya siku 30 tangu kufariki kwa mstaafu.Thamani ya fao ni shilingi 500,000 kwa familia ya mstaafu" anasema Nyallo.
Akizungumzia swali la udhibiti wa waajiri, mtoa mada alieleza kuwa mfuko una kikosi maalum cha wafanyakazi ambao hufanya ziara za mara kwa mara za ukaguzi kwa waajiri mbalimbali nchini. Kupitia ukaguzi huo, PSSSF inafanikiwa kuwabaini wafanyakazi waliopo katika kila ofisi na kuhakikisha kuwa wanaandikishwa rasmi ili wasikose haki zao za msingi za kisheria.
SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254
Post a Comment