" TANZANIA YAFANYA MAPINDUZI AFYA MSINGI, VIFO VYA MAMA WANAOJIFUNGUA VYASHUKA.

TANZANIA YAFANYA MAPINDUZI AFYA MSINGI, VIFO VYA MAMA WANAOJIFUNGUA VYASHUKA.


Na, Egidia Vedasto, Misalaba Media, Arusha.Naibu Waziri TAMISEMI Festo Dugange amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika maboresho ya huduma za afya msingi, hatua ambayo imechangia kupunguza kwa kiasi kikubwa vifo vya wanawake vitokanavyo na uzazi.Akizungumza wakati akifunga Mkutano wa pili wa Kimataifa wa Afya ya Msingi  uliofanyika jijini  Arusha kwa siku tatu kutoka nchi za Afrika na Mabara mengine amesema, vifo vya wanawake wanaojifungua  vimepungua kutoka vifo 556 mwaka 2015/2016 hadi vifo 104 kwa kila vizazi hai laki Moja (100000). Aidha ameeleza kuwa, ni mafanikio makubwa yanayoonesha kuwa maazimio yaliyowekwa yamefanyiwa kazi.Ametaja mafanikio hayo kama picha bora ya jitihada zinazofanywa katika kuboresha huduma za afya nchini, hususan katika ngazi ya afya msingi."Maboresho hayo yamewezesha wananchi kupata huduma bora za afya kwa urahisi zaidi, na  kuchangia kuimarisha mfumo wa afya na kupunguza changamoto zinazowakabili wanawake wakati wa ujauzito na kujifungua" Dugange ameeleza kuwa hatua hizo pia zinaipa Tanzania mwanga wa kufikia malengo ya Ajenda ya Afrika 2063 pamoja na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050. Amebainisha  kuwa kuimarishwa kwa afya msingi ni nguzo muhimu katika kuhakikisha wananchi wanakuwa na afya bora na kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi na kijamii.Vilevile amezitaka nchi za Afrika kuendelea kugharamia huduma za afya, kushirikiana na kubadilishana uzoefu ili kupata mbinu bora za kukabiliana na changamoto zinazolikabili bara hilo katika sekta ya afya.Amehimiza nchi za Afrika kutekeleza kwa vitendo Azimio la Abuja linalozitaka nchi kutenga asilimia 15 ya mapato yake ya ndani kwa ajili ya sekta ya afya.Maazimio yaliyopendekezwa na washiriki wa mkutano  yametaka kuimarishwa kwa mfumo wa ufadhili wa afya unaozingatia utendaji (performance-based financing) barani Afrika, pamoja na kuharakisha utekelezaji wa ajenda ya uzalishaji wa dawa na bidhaa za afya barani Afrika, ili kupunguza utegemezi wa bidhaa kutoka nje ya bara.Azimio lingine ni utekelezaji wa ajenda ya Lusaka  kwa kuimarisha mifumo ya afya inayoongozwa na nchi husika, ikiwa na mipango, bajeti na mifumo ya taarifa inayoratibiwa kwa pamoja.Hata hivyo Katika mageuzi ya mifumo ya afya, azimio linatoa msisitizo kwenye matumizi ya teknolojia za kidijitali, mifumo inayoweza kuwasiliana na kubadilishana taarifa  usimamizi bora wa takwimu na upatikanaji wa taarifa sahihi katika ngazi ya kutolea huduma ili kusaidia kufanya maamuzi yanayotegemea ushahidi.Azimio la tatu kuimarishwa kwa ubora wa utoaji huduma za afya unaomuweka mwananchi katikati, maendeleo ya watumishi wa afya, upatikanaji na usalama wa dawa na bidhaa muhimu za afya, pamoja na kuimarisha mifumo ya afya kwa ujumla.Aidha, nchi za Afrika zimehimizwa kujenga mifumo ya afya inayostahimili mabadiliko ya tabianchi, sambamba na kuendeleza ajenda ya Three Zeros, inayolenga kuondoa vifo vinavyoweza kuzuilika vya mama na mtoto, kujifungua nyumbani na watoto kutopata chanjo.Azimio la mwisho limependekeza kuendelezwa kwa African Union Champion Roadmap on Nurturing Care, kwa kuwekeza katika malezi na maendeleo ya mtoto tangu hatua za awali, huku likisisitiza matumizi ya tafiti na maarifa ya kitaalamu katika kuboresha sera na maamuzi ya afya.Kwa upande wakeMakamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge inayoshughulikia afya Zeyana Abdallah Hamid amesema Tanzania inapaswa kuendelea kuongeza uwekezaji katika huduma za afya ya msingi, akisisitiza umuhimu wa uhuru wa kiafya, kuongeza vyanzo vya mapato kupitia kodi za afya na kuhakikisha huduma hizo zinapata fedha za kutosha.Amesema afya ya msingi inahitaji ufadhili wa kutosha na kwamba Bunge lina wajibu wa kuendelea kuongoza na kusukuma mjadala huo, huku akieleza kuwa changamoto za ufadhili wa huduma hizo tayari zimeonekana na zinaendelea kushughulikiwa kama sehemu ya jitihada za kitaifa za kuhakikisha afya ya msingi inapata fedha zinazostahili.Amebainisha kuwa mkutano huo umewezesha washiriki kujadili mifumo, fursa, mafanikio na changamoto zilizopo katika sekta ya afya nchini Tanzania, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, taasisi, asasi za kiraia, wataalamu na washirika wa maendeleo katika kutafuta majibu ya changamoto hizo.Kwa mujibu huo amesema takribani asilimia 80 ya wananchi wanategemea huduma za afya ya msingi, hivyo uwekezaji katika eneo hilo ni muhimu, hasa kwa kuwa kinga ya magonjwa inaanzia katika ngazi ya huduma za afya ya msingi.Ameeleza kuwa matumizi ya mifumo mbalimbali ya kidijitali na kiteknolojia katika huduma za afya yana fursa kubwa ya kuboresha huduma, lakini ikiwa mifumo hiyo haitatumika ipasavyo inaweza kuongeza mzigo kwa watumishi wa afya badala ya kuwa suluhisho.Pia, amesema Serikali inapaswa kuweka mkazo katika kufadhili mifumo inayosaidia utoaji wa huduma badala ya kuanzisha mifumo inayoongeza mzigo kwa watoa huduma, huku akisisitiza kuwa washirika wa maendeleo wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali hadi ngazi ya utekelezaji ili kuhakikisha mifumo hiyo inatimiza malengo yaliyokusudiwa."Kamati ya Bunge imeona fursa mbalimbali za kupunguza gharama za utoaji wa huduma, mfano ubunifu wa usafiri wa wagonjwa kwa kutumia Bajaji, ambao unaweza kutumika nchini Tanzania na kusaidia kupunguza gharama bila kuathiri viwango vya huduma"Ameeleza kuwa Tanzania imeongeza bajeti ya afya kutoka asilimia saba ya bajeti ya Taifa mwaka uliopita hadi asilimia nane mwaka huu, lakini bado kuna lengo la kufikia asilimia 15, huku akisisitiza umuhimu wa kuweka vipaumbele sahihi katika matumizi ya rasilimali chache zilizopo.Zeyana amesema Kamati ya Bunge itaendelea kuimarisha ushirikiano na wataalamu, taasisi za Serikali, sekta binafsi, mashirika yasiyo ya kiserikali na asasi za kiraia ili kupata ushahidi unaoweza kusaidia Bunge kufanya maamuzi yenye tija kwa taifa.Pamoja na hayo amesema, Kamati hiyo itaendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), pamoja na Kamati nyingine za Bunge,  zinazoshughulikia elimu na bajeti, ili kuhakikisha ajenda za afya ya msingi zinapewa kipaumbele.

  PROFESSOR MGOKO SERIES (EP 1)

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post