" KAMATI YA UTEKELEZAJI WAZAZI CCM MPANDA YAPANGA KUFUFUA SHULE YA SEKONDARI NA UFUNDI MILALA

KAMATI YA UTEKELEZAJI WAZAZI CCM MPANDA YAPANGA KUFUFUA SHULE YA SEKONDARI NA UFUNDI MILALA

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Mkoa wa Katavi na Mjumbe wa Kamati ya Siasa ya Mkoa huo, Ndg. Evarist Simon Mnyere, akiunga mkono juhudi zinazoendelea kufanyika kuhakikisha eneo la Shule ya Sekondari na Ufundi Milala, iliyopo Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, linapimwa na kupatiwa hati miliki. Hatua hiyo ni sehemu ya mikakati ya kurejesha shule hiyo katika hali ya kutoa mafunzo ya sekondari na ufundi kupitia eneo linalomilikiwa na Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda.


Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda imefanya kikao maalumu cha tathmini ya maendeleo ya juhudi za kufufua Shule ya Sekondari na Ufundi Milala iliyopo Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, mkoani Katavi, ambayo kwa mujibu wa taarifa zilizowasilishwa katika kikao hicho haijafanya kazi kwa zaidi ya miaka mitano.

Kikao hicho kilichofanyika Oktoba 29, 2026, kimeongozwa na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndg. Pius M. Buzumalle, ambapo pamoja na mambo mengine, wajumbe wamejadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kurejesha shughuli za shule hiyo na kuiwezesha kutoa elimu ya sekondari na mafunzo ya ufundi kwa vijana.

Katika majadiliano hayo, wajumbe wameeleza umuhimu wa kufanya tathmini ya hali ya shule, kuboresha miundombinu na kupanga eneo lake ili kuweka mazingira yatakayowezesha kurejesha shughuli za utoaji wa elimu na mafunzo ya ufundi.

Mojawapo ya changamoto zilizobainishwa ni kutokuwepo kwa hati miliki ya eneo la shule hiyo, hali ambayo imeelezwa kuhitaji hatua za haraka ili kuhakikisha umiliki wa eneo unalindwa na mali ya Jumuiya ya Wazazi inakuwa salama.

Wajumbe pia wameeleza kuwa miongoni mwa mahitaji muhimu katika hatua za kufufua shule hiyo ni fedha kiasi cha Shilingi milioni 2.333 kwa ajili ya upimaji na upangaji wa eneo. Aidha, wameeleza umuhimu wa mshikamano na ushirikiano wa pamoja katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazoikabili shule hiyo.

Kutokana na hali hiyo, Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda imetoa wito kwa wadau mbalimbali wenye nia ya kusaidia maendeleo ya elimu kujitokeza kushirikiana katika upimaji wa eneo, uboreshaji wa miundombinu na mazingira ya shule hiyo.

Katika hatua nyingine, kikao hicho kimejadili mikakati ya kuimarisha uhai wa Jumuiya ya Wazazi kupitia kuongeza idadi ya wanachama, kuhamasisha ulipaji wa ada za uanachama kwa wakati na kuongeza ushiriki wa wanachama katika shughuli za jumuiya.

Ili kutekeleza mikakati hiyo, maafisa wa jumuiya kwa kushirikiana na maafisa wa TEHAMA wamepangwa kutembelea matawi na kata, huku zoezi la uandikishaji likitarajiwa kufanyika kwa utaratibu wa duka kwa duka na nyumba kwa nyumba ili kutoa elimu kuhusu uanachama na mifumo ya usajili.

Vilevile, wajumbe wamejadili umuhimu wa kuanzisha na kuimarisha miradi ya kiuchumi katika ngazi za matawi na kata ili kuongeza mapato ya jumuiya na kupunguza utegemezi wa michango katika kugharamia shughuli zake.

Kikao hicho pia kimesisitiza umuhimu wa viongozi kutembelea matawi na kata kwa ajili ya kutoa elimu kwa wanachama na wananchi kuhusu masuala ya malezi, elimu, mazingira, afya na utamaduni, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utekelezaji wa majukumu ya Jumuiya ya Wazazi katika Wilaya ya Mpanda.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndg. Pius M. Buzumalle, akiongoza kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, kilichofanyika Oktoba 29, 2026.

Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, Ndg. Jimotoli Jilala Maduka, akishiriki kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda, kilichofanyika Oktoba 29, 2026, kwa lengo la kujadili mikakati ya maendeleo na ufufuaji wa Shule ya Sekondari na Ufundi Milala.

Majengo, madarasa na uwanja wa Shule ya Sekondari na Ufundi Milala, iliyopo Kijiji cha Milala, Kata ya Misunkumilo, Halmashauri ya Manispaa ya Mpanda, Mkoa wa Katavi. Kupitia kikao cha Kamati ya Utekelezaji ya Jumuiya ya Wazazi CCM Wilaya ya Mpanda kilichofanyika Oktoba 29, 2026, wadau mbalimbali wenye mapenzi mema na shule hiyo wameombwa kujitokeza kuchangia hali na mali ili kuwezesha eneo la shule kupimwa na kupatiwa hati miliki. Hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kurejesha shule katika hali yake ya awali ya kutoa mafunzo na kuwezesha vijana kunufaika na elimu kupitia eneo hilo.



PROFESSOR MGOKO EPISODE 07

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

 

Post a Comment

Previous Post Next Post