Katibu Mkuu
wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa, ameitaka
tasnia ya habari nchini kuongeza uzalishaji wa habari zinazohusu maisha ya
wananchi wa vijijini, akieleza kuwa maeneo hayo yanahitaji kupewa nafasi kubwa
zaidi katika vyombo vya habari kutokana na idadi kubwa ya Watanzania wanaoishi
huko.
Msigwa
amesema takwimu za miaka mitano iliyopita zinaonesha kuwa zaidi ya asilimia 65
ya Watanzania wanaishi vijijini, wakati zaidi ya asilimia 80 ya vyombo vya
habari vimejikita mijini, hali inayodhihirisha umuhimu wa kuimarisha uandishi
wa habari unaowapa wananchi wa maeneo hayo uwakilishi unaostahili.
Ametoa wito
huo Oktoba 31, 2026, jijini Dodoma, wakati akifungua Mkutano Mkuu na Kongamano
la Mwaka la Tathmini ya Huduma za Habari na Mawasiliano Vijijini lililoandaliwa
na Chama cha Waandishi wa Habari Vijijini Tanzania (RUJAT).
Amesema
waandishi wa habari wanapaswa kwenda zaidi ya kuripoti mikutano na matamko ya
viongozi, badala yake kufanya utafiti na uchunguzi unaobaini changamoto
zinazowakabili wananchi na kuibua masuala yanayoweza kuchochea upatikanaji wa
ufumbuzi.
Katika hatua
nyingine, Msigwa amesisitiza kuwa waandishi wa habari wanapaswa kurejesha
nafasi yao katika kuhabarisha umma kwa kuzingatia weledi na maadili ya taaluma,
akieleza kuwa jukumu la kutoa taarifa kwa wananchi halipaswi kuachwa kwa
wanaharakati ambao wakati mwingine husimamia ajenda maalumu.
Amesema
taarifa zinazochapishwa au kurushwa na vyombo vya habari zinaweza kuwa na
mchango katika kujenga au kudhoofisha taifa, hivyo wanahabari wanapaswa kutumia
kalamu zao kwa uwajibikaji na kulinda maslahi ya nchi bila kujali tofauti
zilizopo.
Msigwa pia
ameitaka RUJAT kufanya utafiti kuhusu sababu zinazochangia kupungua kwa
ushawishi wa vyombo vya habari kwa wananchi ili kubaini namna bora ya kurejesha
imani na usikivu wa jamii kupitia habari zinazogusa maisha yao.
Ameeleza
kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta ya habari katika kuboresha
mazingira ya kazi kwa wanahabari, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha uchumi
wa vyombo vya habari na waandishi ili kulinda uhuru na weledi wa taaluma.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa RUJAT, Neville Meena, amesema chama hicho kinalenga
kubadilisha mwelekeo wa uandishi wa habari za vijijini kwa kuhakikisha wananchi
wanapewa nafasi ya kueleza changamoto, mahitaji na mafanikio yao, badala ya
habari nyingi kujikita katika mikutano na matamko ya viongozi.
Meena
amesema RUJAT pia imeweka mkazo katika kuimarisha uwezo wa wanachama wake
kupitia mafunzo yanayohusu uandishi wa habari za vijijini, matumizi ya
teknolojia na akili unde (AI), ili kuongeza ubora wa maudhui yanayozalishwa.
Naye Katibu
wa RUJAT, Prosper Kwigize, amesema chama hicho kilichoanzishwa mwaka 2020
kimekua kutoka wanachama waanzilishi 20 hadi kufikia wanachama 120, huku kikiwa
na maombi zaidi ya 60 kutoka kwa waandishi wanaotaka kujiunga.
Amesema
katika mikakati yake, RUJAT inalenga kuimarisha uwezo wa wanachama, kujenga
ushirikiano kati ya waandishi wa mikoa mbalimbali na kuongeza nafasi ya habari
za vijijini katika majukwaa ya habari.
Kwigize
ameongeza kuwa chama hicho kinapanga kuanzisha tuzo maalumu za uandishi wa
habari za vijijini mwaka 2027 kwa lengo la kutambua waandishi wanaozalisha
habari zenye kina na matokeo kwa jamii.
Katika kongamano hilo, Mbunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, ambaye pia ni mwandishi wa habari mwandamizi, amepongeza kuanzishwa kwa RUJAT akieleza kuwa chama hicho kina nafasi ya kusaidia kupaza sauti za wananchi wanaoishi vijijini.

PROFESSOR MGOKO EPISODE 07
🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA
Wasiliana nasi:
📍 East African Spirits (T) Ltd
📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254












































































































































Post a Comment