" SHUKRANI TRAINING COLLEGE YAJIVUNIA MAFANIKIO, YAAHIDI KUPANUA WIGO WA ELIMU MBEYA

SHUKRANI TRAINING COLLEGE YAJIVUNIA MAFANIKIO, YAAHIDI KUPANUA WIGO WA ELIMU MBEYA


Mgeni rasmi katika mahafali ya 21 ya chuo cha Shukrani Training college Soweto Mkoani Mbeya Colonel Mary Mkami (TPWM)



Na Lydia Lugakila- Misalaba Media,MBEYA

Chuo cha Shukrani Training College kilichopo Soweto jijini Mbeya, kimeendelea kupiga hatua katika utoaji wa elimu ya ufundi stadi na mafunzo ya kitaaluma, kikijivunia ongezeko la udahili wa wanafunzi kwa asilimia 20, uboreshaji wa miundombinu pamoja na upanuzi wa programu mbalimbali za mafunzo.


Mafanikio hayo yameelezwa katika Mahafali ya 21 ya chuo hicho yaliyofanyika jijini Mbeya, ambapo wahitimu 175 kati ya wanafunzi 180 walioanza mafunzo walihitimu katika ngazi na programu mbali mbali.

Akizungumza katika mahafali hayo yaliyofanyika Novemba 72026, Mgeni Rasmi, Colonel Mary Mkami, ambaye ni Territorial Commander wa Kanisa la Jeshi la Wokovu Tanzania Territory, ameipongeza menejimenti ya chuo kwa hatua inazopiga katika kuendeleza elimu na kuandaa vijana wenye maarifa na ujuzi unaoweza kuwasaidia kujitegemea.

Mkami amesema elimu wanayoipata vijana inapaswa kuambatana na nidhamu, uaminifu, bidii na hofu ya Mungu ili iweze kuwa msingi wa mafanikio yao katika maisha na maeneo ya kazi.

Amewataka wahitimu kutazama fursa zilizopo badala ya kukazia macho vikwazo, kuacha kulalamika na kuwa wabunifu katika kujitengenezea ajira, akisisitiza kuwa bidii ya kazi inaweza kumfikisha mtu kwenye mafanikio huku nidhamu ikimsaidia kuyadumisha.


Aidha, ameahidi kuhakikisha kunakuwepo na ushirikiano wa karibu kati ya uongozi wa Kanisa la Jeshi la Wokovu na chuo hicho ili kiendelee kutoa elimu bora na kukidhi mahitaji ya jamii.

Awali, Mkurugenzi na Mkuu wa Chuo hicho, Luteni Israel Wilson Mwalukani, amesema Shukrani Training College imeendelea kujenga msingi imara wa kutoa elimu inayozingatia maarifa, ujuzi, maadili, nidhamu, uwajibikaji na huduma kwa jamii.


Amesema chuo hicho kinatoa mafunzo katika ngazi za Stashahada (Diploma), Cheti (Certificate) na kozi fupi, zikiwemo Stashahada ya  Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (ICT), Utalii na Usimamizi wa Hoteli pamoja na kozi mbalimbali za ujuzi wa kujitegemea.

Akielezea mafanikio yaliyopatikana, Mwalukani amesema chuo kimeongeza udahili wa wanafunzi kwa asilimia 20 katika kozi zake, kuboresha majengo, maktaba na madarasa pamoja na kujenga darasa jipya la kisasa kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia.


Amesema pia kila idara imeendelea kupata vifaa vya kujifunzia, huku chuo kikitanua programu za mafunzo na kuimarisha ushirikiano na wadau mbalimbali wakiwemo Serikali, jamii na Kanisa la Jeshi la Wokovu.

Ameongeza kuwa chuo kimefanikiwa kujenga kisima cha kisasa kinachowezesha upatikanaji wa maji kwa saa 24, hatua ambayo imekuwa na manufaa si kwa wanafunzi na watumishi pekee bali pia kwa majirani wanaozunguka eneo hilo.

Akizungumzia dira ya maendeleo, Mwalukani amesema chuo kinalenga kupanua huduma zake za elimu kwa kuongeza na kuendeleza programu za mafunzo zinazokidhi mahitaji ya soko la ajira, kuongeza udahili wa wanafunzi katika ngazi mbalimbali ifikapo mwaka 2027 na kuboresha zaidi hadhi na muonekano wa chuo.


Amesema mipango mingine ni kuimarisha viwango vya kitaaluma, kuendeleza uwezo wa wahadhiri na wafanyakazi kupitia mafunzo ya kitaaluma pamoja na kupanua ushirikiano na taasisi za Serikali, sekta binafsi na wadau wa maendeleo.

Katika risala yao, wahitimu wameeleza kuwa chuo hicho kilianza kujengwa mwaka 1983 na Kanisa la Jeshi la Wokovu na kuanza kutoa mafunzo rasmi mwaka 1995 kikiwa na jina la Shukrani International College of Secretarial Studies.


Wamesema mwaka 2017 chuo kilifanya mabadiliko ya usajili na jina na kuanza kutambulika kama Shukrani Training College, jina ambalo kinatumia hadi sasa.

Wameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake, chuo hicho kimeendelea kukua kwa hatua mbalimbali kikiwa na dhamira ya kutoa elimu bora, maarifa, ujuzi na maadili yanayowawezesha wahitimu kuajirika, kujiajiri na kushiriki katika maendeleo ya taifa.


Aidha, wahitimu wamewashukuru wazazi na walezi kwa kujitoa kugharamia masomo yao hadi kufikia hatua ya kuhitimu, huku wakitoa pongezi kwa NACTVET, VETA, Serikali, wahadhiri, wafanyakazi na wadau mbalimbali kwa ushirikiano wao katika kuendeleza ubora wa elimu na mafunzo chuoni hapo.


Kwa upande wake, Mkaguzi wa Kata ya Ruanda, Inspector Fatma Hamdan, amewataka wahitimu kuwa raia wema, kudumisha maadili na kuwa mabalozi wa amani, utulivu na usalama katika jamii.

Amesisitiza umuhimu wa vijana kushiriki katika kupinga vitendo vya uhalifu kwa kutoa taarifa kwa vyombo husika wanapobaini matukio yanayoweza kuhatarisha usalama wa jamii.

Hata hivyo mahafali hayo ya 21 yamehitimishwa kwa wahitimu kusisitizwa kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuwa chachu ya maendeleo katika familia, jamii na taifa kwa ujumla.





PROFESSOR MGOKO EP 07

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254







Post a Comment

Previous Post Next Post