Serikali
kupitia wakala wa taifa wa hifadhi ya chakula NFRA Kanda ya Shinyanga imetoa
msaada wa bure wa mahindi tani kumi kwa wananchi walioathirika na majitope ya
Mgodi wa Almasi wa Williamson Mwadui.
Msaada
huo umetolewa Novemba 23,2022 ambao pia umekabidhiwa kwa wananchi hao na Mbunge
wa viti maalum kupitia chama cha mapinduzi CCM Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga.
Akizungumza
mwakilishi wa NFRA Revocatus Bisama kwa niaba ya meneja wa NFRA kanda ya
Shinyanga amesema tani tano zimeshafikishwa kwa waathirika na tani tano
zitatolewa kwa awamu nyingine.
"Tulizungukia huku tukiwa na
Mbunge Lucy Mayenga tukaona hali halisi ilivyo hivyo Mbunge akaiomba serikali
iweze kuwasaidia wananchi walioathirika na kupoteza makazi yao"
Bisama Alisema.
" serikali kupitia wakala wa
taifa wa hifadhi ya chakula kanda ya shinyanga ikatoa msaada wa mahindi tani
kumi sawa na gunia 200, na leo tumeleta tani tano sawa na gunia 100, kwaajili
ya kuwasaidia waathirika wa Mwadui" Alisema Bisama.
Mbunge
wa Viti maalum Mkoa wa Shinyanga Lucy Mayenga amesema msaada huo umetolewa
baada ya kuiomba serikali iweze kuwasaidia wananchi waliokutwa na adha hiyo.
" Haya mahindi ilikuwa nitoe
pesa zangu mfukoni lakini baada ya kuongea na Waziri wa Kilimo Hussen Bashe
akanizuia akasema serikali itatoa ili kuwasaidia wananchi"
Alisema Lucy Mayenga.
"Tuishukuru serikali pamoja na
NFRA ambao wanahifadhi mahindi pamoja na uongozi wote wamekuwa tayari lakini
zaidi tumshukuru Rais Samia, na kwamba mtapata mgao wenu, lakini mumtangulize
Mungu kwa kila jambo" Lucy Mayenga alisema.
Kwa
upande wake Afisa Mahusiano katika Mgodi wa Almasi wa Williamson Mwadui WDL
Bernard Mihayo amesema Mgodi umeendelea kuweka mikakati mbalimbali na kwamba
unaendelea kuwahudumia wananchi wote walioathiriwa na tope.
"Kinachoendelea katika mgodi
huu tunafanya marekebisho mbalimbali kuzuia madhara yasiendelee kusamba, pia
kwa kushirikiana na Halmashauri ya Kishapu tunawatafutia mashamba mbadala
kwaajili ya kilimo" Alisema mihayo.
"Pia tutafuta ardhi kwaajili
ya kuwajengea nyumba lakini kwa sasa wapate sehemu za kupanga na kampuni
italipia kodi kwa miezi sita, tutaendelea kutoa msaada mingine kama chakula,
matibabu na kuhahikisha watoto wao wanasoma vizuri"
Alisema Mihayo
Baadhi
ya wananchi hao wameishukuru serikali kuendelea kutatua changamoto zao hususani
kuwaletea msaada wa mahindi.
"Tunaishukuru serikali kwa
kutuletea msaada wa mahindi mahindi ambayo yatatusaidia kwenda kuanzia maisha
maana vitu vyetu vyote viliharibika" Walisema
wananchi.
Novemba 7,2022 kingo za Bwawa la tope katika Mgodi wa Mwadui unaomilikiwa na Kampuni ya Petra Diamonds zilibomoka na tope kuvamia makazi ya wananchi katika kijiji cha Ng'wanh'olo kata ya Mwadui Luhumbo hivyo kusababisha uharibifu.
Post a Comment