" WANANCHI SHINYANGA WATAKIWA KUFUATA TARATIBU ZA KISHERIA, MAADHIMISHO WIKI YA MSAADA WA KISHERIA

WANANCHI SHINYANGA WATAKIWA KUFUATA TARATIBU ZA KISHERIA, MAADHIMISHO WIKI YA MSAADA WA KISHERIA

 

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Wananchi wa Mkoa wa Shinyanga wametakiwa kufuata taratibu za kisheria wakati wote wanapotafuta  haki ama suluhu kwenye mashauri ya kijamii na kifamilia, ili kuondokana na migogoro ikiwemo migogoro ya ardhi, ndoa pamoja na masuala ya mirathi.

Hayo yamezungumza na Mwenyekiti wa kamati ya huduma ya msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga Bwana John Shija  kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma ya msaada wa kisheria ambayo kimkoa imefanyika katika kata ya Masanga Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga.

Mwenyekiti huyo amewasisitiza wananchi kuepuka migogoro na kwamba pale inapotokea wanapaswa kufuata taratibu za kisheria ili kupata haki zao.

“Ni kosa kisheria kuvunja ndoa nje ya mahakama chombo pekee kinachovunja ndoa ni mahakama ni kosa kisheria kugawana mali za mirathi bila kufika mahakamani unaweze kushtakiwa na ukatiwa hatiani na ukafungwa, kuna suala la migogoro ya ardhi tusigombane pale unapoona kuna mgongano mmeingiliana kwenye mpanga ama ardhi utaratibu wa kisheria unaeleweka nenda kwenye baraza la kata”

“Niwasihi kwamba tufuate taratibu za kisheria ili tutunze amani tuwe na upendo sheria zimekuja kwa ajili ya kutunza amani kunyosha njia ya migogoro ili watu waishi kwa amani badala ya kushikana mapanga na kuanza kupigana na nimarufuku mwanamke aliyefiwa na mume kuondolewa kwenye ardhi bila kufuata utaratibu wa kisheria”.amesema Mwenyekiti John Shija

Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Lydia Kwesigabo pamoja na mambo mengine amewataka wananchi kuepuka ukatili wa kijinsia huku akiwasisitiza wazazi na walezi kutimiza wajibu wao kwa watoto ili waweze kufikia ndoto zao.

Aidha afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Lydia Kwesigabo amesisitiza wananchi kutofumbia macho ukatili unaofanyika kwenye familia na kwamba wanapaswa kutoa taarifa za matukio ya ukatili ili hatua zaidi za kisheria ziweze kuchukuliwa.

“Ukatili  ni matendo yanayomzalilisha mtu, yapo matendo sisi wazazi tunawafanyia watoto tukiamini kwamba  ni adhabu kumbe tunawafanyia ukatili leo hii mototo kafanya kosa  unakwenda kuchukua chombo cha moto unamchoma sehemu za  mwili wake unasababisha majeraha hivi hapo harasa ni ya nani kwahiyo wazazi tuache kuwafanyika ukatili watoto tujitahidi kutimiza wajibu wetu kwa kuhakikisha tunamlinda mototo na kuwakagua mara kwa mara hasa watoto wa kike”.

“Upande wa madhara moja wapo ni mimba za utotoni tunaona kwamba watoto ambao wapo shule wanapoteza mwelekeo kwa sababu ya kupata mimba lakini madhara mengine ni ulemavu kama wanandoa watakatana mapanga mmoja wapo atapata ulemavu lakini pia vifo tunasikia hata kwenye vyombo vya habari mara nyingi tunasema unapokuwa na hasira usichukue maamuzi magumu unapaswa utulie kwanza mwisho wa siku utachukua maamuzi ambayo niya hekima lakini pia kuna kupata magonjwa kwa mfano mtu amebakwa huwezi kumjua aliyekubaka kama atakuwa salama anaweza kuwa ana maambukizi ya magonjwa”.amesema afisa ustawi wa jamii Lydia

“Tunaombeni ushirikiano kwa hao watu wanaofanya matukio ya ukatili wapo watu wanaona kabisa mtu anafanyiwa ukatili lakini wanaogopa kutoa taarifa kumbuka unakuwa unamkosesha haki mtu aliyefanyiwa ukatili yapo maeneo mengi ya kuripoti matukio ya ukatili kwa mfano kwa watoto shule unaweza kuripoti kwa mwalimu au ofisi za kata na ngazi zingine lakini pia ukiona huwezi au huwaamini piga simu sisi tunatunza siri yako ilikumuokoa yule mtu anayefanyiwa ukatili kwahiyo tusikae kimya tutoe taarifa kuna zile namba za serikali ambazo zinatumika bure kwahiyo na sisi kwenye ukatili tunatumia namba 116 piga hii namba ili kutoa taarifa ya ukatili”.amesema Lydia

 

Afisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kishapu Adam Mwihechi ametumia nafasi hiyo kuwaomba wananchi kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa na kwamba kila mwananchi anawajibu wa kushirika katika kuzuia na kupambana na rushwa.

“Kila mwananchi anajukumu la kutoa taarifa za vitendo vya rushwa kwa TAKUKURU au kwa vyombo vyingine vya sheria au dola, mwananchi unatakiwa kuichukia rushwa na kuepuka kushiriki vitendo vya rushwa kumbuka rushwa ni kikwazo kikubwa kwa demokrasia, utawala bora, haki za binadamu na ni tishio kwa amani, utulivu na usalama katika jamii wewe ndiye unayeathirika zaidi katika kila tendo la rushwa unaloshiriki hivyo amka acha mara moja rushwa”.amesema Adam Mwihechi

Wakili wa serikali ofisa ya Taifa ya mashtaka Mkoa wa Shinyanga Rose Kimaro amezungumzia suala la dhamana huku akiwasisitiza wananchi kutoa ushahidi kwa mtuhumiwa au mshtakiwa ili kuondoa changamoto.

“Dhamana hii huwa inatolewa kwa makosa ya jinai pale ambapo mtuhumiwa yupo katika kizuizi cha polisi au kizuizi cha mahakama na dhamana ni haki ya kikatiba  wala siyo upendeleo, katika kesi zetu tunazoendesha ni pamoja na kesi za ukatili wa kijinsia”

“kumekuwa na changamoto mbalimbali kwamba mashahidi hawafiki mahakamani kwahiyo hapo tunakuwa tunakosa ushahidi wa kuendeleza ile kesi na yule mhanga anashindwa kupatiwa haki yake kwahiyo mnatakiwa muonyeshe ushirikiano kuanzia kwenye upelelezi katika ngazi ya polisi na shauri linapofikishwa mahakamani basi muonyeshe ushirikiano kwetu kwa kuja mahakamani kutoa ushahidi ili tuweze kushinda kesi”.amesema wakili Rose Kimaro

 

 Kwa upande wake Mwanasheria wa kituo cha msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga Andrew Jeremiah ametoa elimu kwa wananchi,kuhusu namna bora ya kutafuta utatuzi wa migogoro ambapo amewasihi kufikisha changamoto ama migogoro sehemu husika ili ziweze kutatuliwa katika utaratibu mzuri uliowekwa.

Nao baadhi ya wananchi wa kata ya Masanga waliohudhuria kwenye kilele cha maadhimisho ya wiki ya huduma ya kisheria wamepongeza huku wakishukuru kwa kupata elimu hiyo.

Aidha baadhi ya wananchi waliohudhuria katika maadhimisho hayo wamepata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali wakitaka kuelewa zaidi juu ya masuala ya kisheria ambapo timu ya wataalam kutoka Mkoa na wilaya wamejibu maswali hayo papo kwa hapo.

Moja ya maswali yaliyoibuliwa katika maadhimisho hayo ni pamoja na migogoro ya ardhi, migogoro ya ndoa, umiliki wa ardhi, masuala ya mirathi, masuala ya dhamana mahakamani, upatikanaji na utoaji wa talaka, makosa ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji, ulawiti, vipigo pamoja na ushirikiana.

Wiki ya maadhimisho ya huduma ya msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga ilizinduliwa katika kata ya Mwakipoya Novemba 8,2022 na kilele chake kimefanyika kwenye kijiji cha Bulekela kata ya Masanga Novemba 12 ambapo mgeni rasmi katika kilele hicho alikuwa  afisa wa huduma za kisheria Wilaya ya Kishapu Bwana Benard Kadanda.

Maadhimisho ya wiki ya huduma za kisheria ni huduma inayotolewa kwa lengo la kuibua matatizo ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake, watoto, wazee, walemavu na wanaume Nchini.

Wiki ya huduma ya msaada wa kisheria hufanyika kila Mwaka kwa lengo la kutoa elimu kwenye jamii ili kuwa na uelewa kuhusu masuala ya kisheria ambapo kwa Mwaka huu 2022 maadhimisho ya wiki ya huduma za kisheria katika mkoa wa Shinyanga umefanyia maadhimisho hayo kwenye wilaya ya Kishapu kwa kauli mbio isemayo “UKATILI NA UDHALILISHAJI WA KIJINSIA NI KIKWAZO CHA MAENDELEO YA TAIFA WANANCHI WOTE TUSIMAME PAMOJA KUZUIA”

Mwenyekiti wa kamati ya huduma ya msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga Bwana John Shija akizungumza na wananchi kwenye kilele cha maadhimisho hayo

Aliyenyosha mikono juu ni Mwenyekiti wa kamati ya huduma ya msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga  John Shija akiwasisitiza wananchi kufuata utaratibu wa kisheria ili kuzuia migogoro mbalimbali

Mgeni rasmi katika kilele hicho  afisa wa huduma za kisheria Wilaya ya Kishapu Bwana Benard Kadanda akizungumza na wananchi

Afisa ustawi wa jamii Mkoa wa Shinyanga Lydia Kwesigabo akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo 

Afisa wa taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) Wilaya ya Kishapu Adam Mwihechi akitoa elimu kwa wananchi


Wakili wa serikali ofisa ya Taifa ya mashtaka Mkoa wa Shinyanga Rose Kimaro akitoa elimu kwa wananchi

Mwanasheria wa kituo cha msaada wa kisheria Mkoa wa Shinyanga Andrew Jeremiah akitoa elimu kwa wananchi

Diwani wa kata ya Masanga Mh: Enock Reuben akipongeza maadhimisho hayo kufanyika katika kata yake

                                        












































 

Post a Comment

Previous Post Next Post