Msichana Winfrida Mandindile (17) mkazi wa Kihesa, Manispaa ya Iringa aliyekatisha masomo baada ya kupata mimba na kujifungua mwaka mmoja uliopita, amefariki dunia baada ya kujinyonga.
Inadaiwa kuwa msichana huyo aliyekuwa akisoma shule ya sekondari Kihesa, Manispaa ya Iringa alikuwa akilalamika kukosa mahitaji kwa ajili ya kumlea mwanae.
Hata hivyo baadhi ya majirani wamesema huenda mvutano uliokuwepo baina yake na familia ulisababisha msichana huyo kuamua kujinyonga kama njia ya kuukwepa.
Winfrida ambaye ameacha mtoto wa mwaka mmoja alikuwa akisoma kidato cha kwanza.
Akizungumza mama mzazi wa Winfrida, Agnes Donald amesema mwaka jana mwanaye alipata mimba aliyopewa na mwanafunzi mwenzake jambo lililosababisha akatishe masomo yake.
Hata hivyo, mama yake amesema siku ya tukio mwanaye aliaga nyumbani kwamba anakwenda kutembea na alipochelewa kurejea ilibidi amuulize huenda ikawa sababu ya kukasirika.
Amesema aliamua kuuliza sababu za kuchelewa kurudi nyumbani na huenda hiyo pia ikawa sababu za kuamua kupoteza
“Inawezekana ni kulingana na utoto alionao, sisi tulikuwa tunaishi naye vizuri na kama akikosea tulikuwa tunamuonya, sisi hatukuwa na ugomvi naye,” amesema Donald.
Baadhi ya majirani zao wamesema inawezekana mtoto huyo alikosa msaada wa ushauri baada ya kupata mimba na kukatisha masomo.
“Angepata msaada asingefanya uamizi wa kujiua, inasikitisha kuona msichana mdogo amepoteza maisha yake,” amesema Anitha Kissa, mkazi wa Semtema Manispaa ya Iringa.
Kwa upande wake, Mkuu wa kituo kidogo cha Polisi cha Semtema, Cosmas Ngai aliyekuwa eneo la tukio aliwataka wananchi na wafiwa kuwa wavumilivu katika kipindi hiki cha msiba.
Amewakumbusha wazazi kuwa karibu na watoto wao huku wakiangalia maendeleo yao ya masomo na maisha ya kawaida ili iwe rahisi kuwasaidia inapotokea changamoto.
“Kikubwa tuwashauri watoto wetu kama wanasoma wasome, kama kuna mambo mengine tuwasimamie. Huyu inaonekana alikosa ushauri. Tunaomba wazazi muwafuatilie sana watoto ndilo jukumu letu,” amesema.
Chanzo - Mwananchi
Post a Comment