Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, Jumatano tarehe 25.01.2023, amewapa daraja takatifu la Ushemasi Mafrateri watatu wa Jimbo, kupitia adhimisho la Misa takatifu ambayo imefanyika katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga.
Waliopewa daraja la Ushemasi ni Emmanuel Ndoma wa Parokia ya Nyalikungu Wilayani Maswa mkoani Simiyu, Sosthenes Ntemi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi mkoani Simiyu na James Furaha Mrema wa Parokia ya Mwadui Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Akizungumza katika Misa hiyo ya ushemasi, Askofu Sangu amewaomba Waamini kuendelea kuwaombea Mashemasi hao, ili hapo baadaye wafikie daraja la Upadre.
Ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wazazi wao kwa kuwalea katika misingi ya Imani na kuwaongoza mpaka kufikia daraja hilo, ambapo ameziomba familia za Kikristo kuendelea kuchochea miito ya Upadre na utawa kwa watoto wao.
Wakati huohuo, Askofu Sangu amewaapisha viongozi wanane wa Kamati tendaji ya Mawasiliano Jimbo, ambao wamechaguliwa hivi karibuni, huku watatu miongoni mwao wakiwa ni wa kuteuliwa.
Kamati hiyo pamoja na mambo mengine, itakuwa na Jukumu la kuratibu na kuhamasisha michango ya uenezaji wa Injili kupitia vyombo vya Mawasiliano Jimboni, hususani Redio Faraja.
Walioapishwa ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo Ndugu Sylivester Mpemba, Mwenyekiti msaidizi wa Kamti Juliana Paul, Katibu wa Kamati Ndugu Kenedy Malesa, Katibu msaidizi wa Kamati Monica Masesa na Mweka hazina wa Kamati Ndugu Ignatus Banyemaa.
Wengine ni wajumbe watatu wa kuteuliwa wa kamati ambao ni Eustace Mgawe, William Chami na James Msimbang’ombe.









Post a Comment