" SHIRIKA LA THUBUTU AFRICA LAWAOKOA WANAFUNZI WA KIKE 306 SHULE YA MSINGI LUBAGA - SHINYANGA

SHIRIKA LA THUBUTU AFRICA LAWAOKOA WANAFUNZI WA KIKE 306 SHULE YA MSINGI LUBAGA - SHINYANGA

Na Mapuli Misalaba, Shinyanga

Shirika  lisilo la kiserikali la Thubutu Africa Initiatives (TAI) limekabidhi choo cha wasichana katika shule ya msingi lubaga iliyopo katika Manispaa ya Shinyanga ili kupunguza msongamano wa wanafunzi kwenye matundu machache yaliyopo.

Shirika hilo ambalo limekuwa likitekeleza mradi wa Hisani katika jamii (Community Philanthropy) kwa kushirikiana na jamii pamoja na wadau mbalimbali wa Mkoa wa Shinyanga limekabidhi choo hicho leo Alhamisi Januari 26,2023 ambacho  mpaka sasa kimegharimu  zaidi ya shilingi Milioni 11.

Hafla hiyo imehudhuriwa na viongozi wa serikali, chama, wadau kutoka taasisi mbalimbali pamoja na wananchi.

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi mradi wa Hisani katika Jamii, Mkurugenzi wa shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI) Jonathan Manyama Kifunda ameeleza kuwa shirika hilo litaendelea kuboresha miundombinu kwa watoto wa kike katika taasisi za Elimu

“Shirika la Thubutu Africa  Initiatives (TAI) ni shirika linalofanya kazi katika Mkoa wa Shinyanga na moja ya miradi ya shirika hili ni kuboresha miundombinu kwa watoto wa kike katika taasisi za elimu katika shule za msingi na sekondari na tayari tumeshafanya kwa takribani shule nane za hapa Mkoa wa Shinyanga”. Amesema Mkurugenzi Jonathan

“Mradi huu wa hisani kwa jamii katika kata ya Old Shinyanga, Chibe na Mwamalili ilikuwa ni kupata tu mitazamo ya watu lakini kata hii ya Lubaga ilikuwa ni kufanya kwa vitendo kwa kuishirikisha jamii yenyewe tunashukuru jamii pamoja na wadau mbalimbali tumeshirikiana nao kwa asilimia mia moja”.amesema Mkurugenzi Jonathan

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga mgeni rasmi katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi amepongeza hatua ya ujenzi wa choo katika shule ya msingi Lubaga.

Kwanza nilishukuru shirika la Thubutu Africa kwa kuja na utaratibu huu mmeifungua jamii kwamba kumbe tunaweza kufanya sisi wenyewe niwaombe wajumbe mliopo kwenye kamati hii kwanza mjipongeze pili msikate tamaa, mimi nashauri baada ya kufikisha mradi huu kwenye hatua hii tuendeleze ili watu tuzoee kuchangia maendeleo yetu sisi wenyewe kwa sababu hiki kitu tunachofanya ni jambo jema kwahiyo niwaombe watu wengine ambao hawakushiriki tuunge mkono juhudi hizi tusisubiri wafadhiri kila wakati”.amesema katibu Chambi

Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa Hisani katika jamii (Community Philanthropy) Bwana Joseph Ndatala wakati akisoma taarifa ya ujenzi wa choo cha wasichana katika shule ya msingi Lubaga amesema ujenzi huo umetumia zaidi ya Milioni 11 huku akitoa ushauri na mapendekezo kwenye jamii ya mkoa wa Shinyanga.

“Kamati ya Hisani katika Jamii iliundwa na wadau wa Maendeleo katika Manispaa ya Shinyanga chini ya usimamizi wa Shirika lisilokuwa la Kiserikali (NGO,s) la Thubutu Africa. Wadau wa Maendeleo ambao walikuwa ni NGO,s pamoja watumishi wa Serikali ambao ni Maafisa Maendeleo ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata, Viongozi wengine wa Serikali ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata na Mitaa wakiwemo watendaji wa Mitaa na Kata walihudhuria Mkutano huo”.  

“Tarehe 20/05/2022 Shirika la Thubutu Africa Initiatives lilizindua mradi wa hisani katika jamii katika ukumbi wa Vigmark hotel ambapo wajumbe mbalimbali kutoka serikalini pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali walihudhuria”. Amesema Mwenyekiti Ndatala

“Mkurugenzi wa Thubutu Africa Initiatives alitoa mafunzo kuhusu namna mradi wa hisani katika jamii unavyotekelezwa. Baada ya mafunzo hayo kati ya kata nne zilizokua na wajumbe walioziwakilisha kata moja (LUBAGA) ilichaguliwa ili kutekelezwa mradi wa hisani katika jamii ambapo kata tatu zilizobaki zilitumika kufanyiwa utafiti kuhusu uelewa na utayari wa wanajamii katika kuchangia maendeleo yao wenyewe”.

 “Kamati iliyoundwa ilikuwa na wajumbe kumi na mbili akiwemo Mwenyekiti, Katibu, Mratibu pamoja na wajumbe wengine ambao walikamilisha timu nzima ya wajumbe 12”amesema Ndatala

“Kamati ya Hisani ilianza kazi rasmi mnamo tarehe 07/07/2022 takribani miezi miwili baada ya kuchaguliwa ambapo zoezi la ukusanyaji wa rasilimali lilianza likiongozwa na Mwenyekiti wa kamati Ndugu Joseph Ndatala ambapo tarehe 17/07/2022 zoezi la ujenzi lilianza, siku kumi baada ya Kamati kuanza kazi, zoezi la ujenzi lilikamilika tarehe 12/12/2022 miezi mitano baada ya Kamati kuchaguliwa na kuanza kazi. Kamati ilitekeleza majukumu yake kwa weredi mkubwa kwa kuzingatia maazmio ya kikao cha wadau ambayo yalitumika kama hadidu rejea katika kutekeleza majukumu ya Kamati”. Amesema Ndatala

“Kwa mujibu wa Mchoro wa ujenzi na makadirio ya bajeti(BOQ) ujenzi wa choo cha Wasichana Lubaga ulikadiriwa kutumia kiasi cha Milioni ishirini na tatu laki tatu tisini na saba miatisa themanini na nne tu(Tsh 23,397,984) hata hivyo ujenzi huu umetumia kiasi cha Tsh 11,063,800/= ikiwa nipamoja na nguvu kazi kama ambavyo imeelezwa na kuchangunuliwa kwenye taarifa ya fedha ambayo nikiambatanisho cha taarifa hii”.

 “Kwa Taarifa hii Kamati inaujulisha umma wa wana Shinyanga na Tanzania kwa ujumla kuwa kiasi cha fedha kilichotumika kujenga choo hiki cha kisasa ni Tsh 11,063,800”.amesema Ndatala

“Kamati ya Hisani imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa matundu sita ya choo cha wasichana Lubaga pamoja na chumba maalumu cha wasichana kwa jili ya kujistiri hivyo, wasichana watasoma kwa utulivu na mahudhurio yao katika vipindi darasani kuongezeka na kuendeleza kiwango cha ufaulu kuwa juu na ubora wa elimu wanyoipata, Mafanikio haya hayakuwa mepesi kwa sababu miradi ya aina hii haijazoeleka katika maeno yetu na Tanzania hususani Manispaa ya Shinyanga hata hivyo umahiri na uvumilivu wa wajumbe wa Kamati umekuwa chanzo kikuu cha mafanikio ya kazi hii ya ujenzi wa choo hiki”.

“Pamoja na mafanikio makubwa yaliyopatikana kwa ujenzi wa choo kukamilika kwa asilimia 99.8 Kamati inatoa shukrani kwa kuaminiwa kuwa chombo cha kusimamia shughuli hii njema pamoja na kwamba ilikuwa na changamoto, Kamati kwa niaba ya Shirika la TAI inatoa shukrani kwa watu na Taasisi mbalimbali ambazo zimekuwa bega kwa bega katika kuhakikisha kuwa ujenzi wa choo cha wasichana Lubaga umekamilika”.

“Kamati pia inatoa shukrani za dhati kwa ofisi ya Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga kwa ushirikiano mkubwa waliotoa kwa Kamati wakati tulipohitaji ushauri wa kitaalamu, mchango wa mawazo na fedha kwa ajili ya ujenzi, ni ukweli uliokuwa wazi Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga alipokea simu zetu kwa wakati wote na hata tulipotaka kukutana naye alitoa ushirikiano wa kutosha”.

“Aidha Kamati inashukuru sana Shirika la Thubutu Africa kwa kuja na mpango ambao umeleta matokeo chanya kwa wanafunzi wa Shule ya Msingi Lubaga tunawashukuru pia walimu na wazazi wa Shule ya Msingi Lubaga kwa ushirikiano wao waliotupatia lakini pia Kamati inawashukuru wote walitoa ushirikiano na kushiriki kwa namna moja ama nyingine kufanikisha ujenzi huu”.

“Kamati ya hisani katika utekelezaji wa mradi huu imebaini kuwa upo uwezekano mkubwa wajamii kushiriki katika shughuli za maendeleo katika kusaidia jamii yao wao wenyewe, hivyo tunapendekeza mradi huu utekelezwe mahali pengine katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga”. Ameeleza Mwenyekiti wa kamati Bwana Ndatala

Mkuu wa shule ya msingi Lubanga Stella Lucas Halimoja amesema shule hiyo inajumla ya wanafunzi 605 kata yao wavulana 297 na wasichana 306 huku akilishukuru shirika la Thubutu Africa kwa kupunguza changamoto ya choo.

“Katika shule yetu tulikuwa na changamoto ya vyoo lakini changamoto kubwa ilikuwa kwa wasichana tulipaswa kuwa na matundu ya choo 15 lakini  tulikuwa na matundu cha choo manne tu kwahiyo kutokana na huu mradi ambao tumekabidhiwa leo tumeponguza changamoto kwa kiasi kikubwa”.amesema Mkuu wa shule Stella

Misalaba Blog imezungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Lubaga nao wamelishukuru shirika la Thubutu Africa kwa kutatua changamoto ya vyoo ambapo wamesema kitawaondolea adha ya kupanga foleni wakati  wa kujisaidia lakini pia  kujiepusha na magonjwa mbalimbali ikiwemo Kichocho.

Mkurugenzi wa shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI) Jonathan Manyama Kifunda akizungumza leo kwenye hafla hiyo iliyofanyika katika uwanja wa shule ya msingi Lubaga Manispaa ya Shinyanga.

Mkurugenzi wa shirika la Thubutu Africa Initiatives (TAI) Jonathan Manyama Kifunda akizungumza leo kwenye hafla ya kukabidhi mradi wa Hisani katika jamii.

Mgeni rasmi katibu tawala wa Wilaya ya Shinyanga Boniphace Chambi  akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mradi wa hisani katika jamii shule ya msingi Lubaga kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.

Mwenyekiti wa kamati ya mradi wa Hisani katika jamii (Community Philanthropy) Bwana Joseph Ndatala akisoma taarifa ya ujenzi wa choo cha wasichana katika shule ya msingi Lubaga kata ya Lubaga Manispaa ya Shinyanga.

Naibu Meya wa Manispaa ya Shinyanga Esther Makune akizungumza katika hafla ya shirika la Thubutu Africa kukabidhi mradi wa choo cha kisasa katika shule ya msingi Lubaga Manispaa ya Shinyanga.Mwenyekiti wa chama cha mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Anord Makombe akizungumza katika hafla hiyo.Diwani wa kata ya Lubaga Reuben Dotto akizungumza katika hafla hiyo.









Post a Comment

Previous Post Next Post