" ASKOFU SANGU AWATAKA WAAMINI KUITUNZA NA KUILINDA TUNU YA NDOA, MAPADRE WOTE WARUDIA VIAPO

ASKOFU SANGU AWATAKA WAAMINI KUITUNZA NA KUILINDA TUNU YA NDOA, MAPADRE WOTE WARUDIA VIAPO

Askofu wa Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, amewataka waamini Wakatoliki na watu wote wenye mapenzi mema kuitunza na kuilinda tunu ya ndoa, ambayo ndiyo chimbuko la miito na karama zote katika Kanisa, ikiwemo wito wa Upadre.
Askofu Sangu ameonya kuwa, kuruhusu vitendo vya ushoga na ndoa za jinsia moja ni kuua familia.
Ameziasa familia za Kikristo kuishi kwa kufuata misingi ya Imani na kumtegemea Mwenyezi Mungu, ili Kanisa liweze kupata Mapadre na watawa.
Wakati huohuo, Askofu Sangu amewakumbusha wakatoliki kuendelea kuwaombea Mapadre wao, ili waifanye kazi ya kuihubiri habari njema waliyokabidhiwa kwa upendo na uaminifu , wakionesha mfano kwa matendo na maneno yao.
Kupitia Misa hiyo, Mapadre wote wamerudia viapo vyao vya kipadre mbele ya Askofu wa Jimbo, na baadaye waamini wamepata nafasi ya kuwapongeza kwa majitoleo waliyoyafanya kupitia huduma za kiroho walizowapatia katika kipindi cha mwaka mzima.
Zaidi ya Shilingi Milioni 420 zimetolewa na waamini kwa ajili ya kuwategmeza Mapadre wao, huku Parokia ya Mwanhuzi ikiongoza kwa kutoa kiasi cha zaidi ya Shilingi milioni 36.
Kanisa Katoliki kote ulimwenguni, huweka wakfu mafuta ya Krisma takatifu na kubariki mafuta ya wagonjwa na wakatekumeni kupitia Maaskofu wa majimbo, mbele ya Mapadre na waamini, maadhimisho ambayo yanafanyika siku chache kabla ya Pasaka.
Mafuta ya Krisma takatifu hutumiwa na Kanisa kwa ajili ya kutakatifuza wakati wa utoaji wa Sakramenti mbalimbali za Kanisa, ambazo ni pamoja na Ubatizo, Kipaimara na Sakramenti ya Daraja (Ushemasi, Upadre na Uaskofu)
Mafuta hayo pia hutumika kutakatifuza vifaa mbalimbali vinavyotumika kwa kazi za ibada na Misa takatifu, ikiwemo Kanisa, Altare na Kalisi.
Kwa upande wa mafuta ya wagonjwa, wanapakwa ili kuwatia neema maalum, kuwapa nguvu na kuwafariji katika ugonjwa wao, pamoja na kuwaandaa kwa ajili ya kukutana na Mwenyezi Mungu.
Aidha, mafuta ya Wakatekumeni hupakwa wanafunzi wa dini kabla ya kupewa Sakramenti ya ubatizo, ili kuwaimarisha katika mapambano ya kiroho yanayodaiwa katika maisha ya Kikristo.

Post a Comment

Previous Post Next Post