Mnamo tarehe 12.04.2015, Askofu wa Jimbo Katoliki Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu, aliwekwa wakfu na kusimikwa rasmi kuwa Askofu wa nne wa Jimbo la Shinyanga, kufuatia kifo cha aliyekuwa Askofu wa tatu wa Shinyanga hayati Aloysius Balina, aliyefariki mnamo mwaka 2012.
Askofu Sangu alipokelewa Jimboni Shinyanga mnamo tarehe 11.04.2015, katika mpaka wa Jimbo kuu la Tabora na Jimbo la Shinyanga, akitokea Jimboni Sumbawanga alikozaliwa.
Baada ya kuwasili Jimboni Shinyanga, alikiri Imani na kula viapo mbalimbali vya Kanisa ikiwemo, kuilinda Imani na kumtii Baba Mtakatifu, kupitia ibada ya Masifu ya Jioni iliyofanyika siku hiyo, ikiwa ni maandalizi ya utolewaji wa daraja la uaskofu siku inayofuatia.
Aliwekwa wakfu na kusimikwa na Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, akisaidiana na Maaskofu wengine, huku tukio hilo likishuhudiwa na Maaskofu kutoka maeneo mbalimbali ya ndani na nje ya nchi, rais wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Mapadre, watawa,waamini pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, taasisi na vyama vya siasa.
HISTORIA YAKE KWA UFUPI
Askofu Liberatus Sangu alizaliwa mnamo tarehe 19 Februari 1963, katika kijiji cha Mwanzye, Jimbo Katoliki la Sumbawanga, ambapo baada ya kumaliza elimu yake ya kidato cha sita na mafunzo ya Jeshi la kujenga taifa (JKT) kwa mujibu wa sheria, alijiunga na majiundo yake ya kikasisi kwenye Seminari kuu ya Kibosho iliyopo Jimbo Katoliki Moshi kwa masomo ya Falisafa na Segerea Jimbo kuu la Dar es Salaam kwa Masomo ya Teolojia.
Alipewa Daraja la Upadre mnamo tarehe 9 Julai 1994, katika Jimbo Katoliki Sumbawanga.
Katika maisha yake ya kipadre, Askofu Sangu amewahi kuwa Mlezi wa Seminari ndogo ya Kaengesa, iliyopo Jimboni Sumbawanga kuanzia mwaka 1994 hadi mwaka 1995 na baadaye akapangiwa kwenda kufanya kazi katika Parokia ya Matai kuanzia mwaka 1995 hadi mwaka 1996.
Kati ya Mwaka 1996 hadi mwaka 1999 alikwenda mjini Roma kwa masomo ya juu na kutunikiwa shahada ya uzamili katika taalimungu ya Sakramenti za Kanisa, kutoka katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Mtakatifu Anselmi, kilichoko mjini Roma.
Baada ya kurudi Jimboni mwaka 1999, aliteuliwa kuwa Msimamizi wa Parokia ya Mwanzye hadi mwaka 2000.
Kuanzia mwaka 2000 hadi mwaka 2007, akateuliwa kuwa Mkurugenzi wa miito Jimbo Katoliki la Sumbawanga, mlezi katika mwaka wa malezi na Mkurugenzi wa utume wa vijana wa Jimbo.
Mwaka 2007 aliteuliwa kuwa Paroko wa muda Parokiani Sopa hadi mwaka 2008 alipotumwa kwenda kutekeleza utume wake kama Afisa mwandamizi katika Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu mjini Vatican, mpaka alipoteuliwa kuwa Askofu wa Shinyanga.
BAADHI YA MAFANIKIO KATIKA MIAKA 8 YA UASKOFU
Katika miaka yake minane ya utumishi Jimboni Shinyanga, Askofu Sangu akiongozwa na kaulimbiu ya “TUNDA LA ROHO NI UPENDO” amekuwa karibu zaidi na waamini kwa kuzitemebelea Parokia kila mwaka ili kukoleza moyo wa imani pamoja na kuwajengea moyo wa majitoleo na kulitegemeza Kanisa lao.
Askofu Sangu amefanikiwa kuanzisha Parokia mpya zipatazo 11 na kulifanya Jimbo la Shinyanga kuwa na Jumla ya Parokia 37 badala ya 26 alizozikuta, hatua aliyoitaja kuwa imelenga kusogeza huduma za kiroho kwa waamini.
Pia ameanzisha Parokia teule kadhaa ambapo tatu kati yake ziko kwenye mchakato wa kuwa Parokia kamili, ambazo ni Ndembezi, Shishiyu na Lagangabilili.
Ameongeza idadi ya waseminari wakubwa kutoka chini ya 20 mwaka 2015, hadi kufikia zaidi ya sabini mwaka huu 2023, ambapo kwa mara ya kwanza katika historia ya Jimbo la Shinyanga, mwishoni mwa waka huu 2023, anatarajia kuwapatia daraja la ushemasi Mafrateri wapatao 11 wa Jimbo.
Ili kulistawisha Kanisa, Askofu Sangu pia ameanzisha Shirika la watawa wa kike la kijimbo la Mtakatifu Bikra Maria Mama wa Huruma.
Katika kukoleza moyo wa Imani, ameanzisha kituo cha hija ya Imani katika Kanisa la Mtakatifu Michael Parokia ya Sayusayu wilayani Maswa mkoani Simiyu, ambalo ni la kwanza katika historia ya Jimbo la Shinyanga.
Amefafanya uinjilishaji wa kina katika kijiji cha Gambosi (Gamboshi) eneo ambalo lilitengwa kwa muda mrefu kutokana na imani potofu zilizokuwa zimejengeka miongoni kwa jamii chini ya Parokia ya Ngulyati ambayo aliianzisha mara tu baada ya kuwekwa wakfu na kusimikwa kuwa Askofu wa Jimbo la Shinyanga.
Amefika na kupeleka habari njema katika eneo la jamii ya Wataturu huko wilayani Meatu mkoa Simiyu ambao wengi wao walikuwa hawajafikiwa na habari ya Injili.
Amejitahidi kuwapeleka masomoni Mapadre wengi zaidi pamoja na kuanzisha ujenzi wa Hostel maalum za Mapadre ambao uko katika hatua za mwisho.
Katika masuala ya huduma za kijamii ameendeleza na kuboresha mazingira ya kutolea huduma za afya katika vituo vya afya na zahanati zinazomilikiwa na Kanisa.
Aidha katika upande wa elimu ameboresha mazingira ya kujifunzia kwenye shule zinazomilikiwa na Kanisa pamoja na kuweka walimu wenye sifa ikiwemo Mapadre wenye taaluma ya ualimu.
Askofu Sangu pia amekuwa mstari wa mbele katika mapambano dhidi ya matendo maovu ikiwemo kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto, ushoga, usagaji na ndoa za jinsia moja.
Post a Comment