" KATIBU TAWALA WA WILAYA YA KASULU AKERWA NA ONGEZEKO LA WATOTO WASIOENDA SHULE.

KATIBU TAWALA WA WILAYA YA KASULU AKERWA NA ONGEZEKO LA WATOTO WASIOENDA SHULE.

Anaripoti Respice Swetu, Misalaba Blog
Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Mughuha Titus, amewata walimu kushirikiana na viongozi wa serikali katika kuwarudisha shuleni watoto walioacha shule.

Mughuha ametoa wito huo alipokuwa akifungua mafunzo ya siku tano ya walimu wa MEMKWA wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu yanayofanyika kwenye chuo cha ualimu Kasulu. 

Amesema kuwa, kuendelea kuwepo kwa kundi hilo ni sawa na kuandaa bomu ambalo litakuja kulipuka baadaye.

Akitoa mfano Mughuha ambaye alikuwa amemwakilisha mkuu wa wilaya ya Kasulu kufungua mafunzo hayo amesema, matukio ya uhalifu yanayotokea hivi sasa  yamekuwa yakiwahusisha watoto hali ambayo ni hatari.

"Watoto hawa wamekuwa wakitumika kwenye vitendo vya uhalifu na matukio ya wizi, ukabaji, udokozi mpaka kwenye ugaidi, hali hii ni hatari na haikubaliki", amesema.

Ameongeza kuwa ili kufanikisha mpango huo, walimu wanapaswa kushirikiana na viongozi wa kata na vijiji kuwabaini watoto walioacha shule na kuweka mikakati ya kuwarudisha shuleni.

Akizungumza kwenye mafunzo hayo, kaimu mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya ya Kasulu Ndelekwa Vanika, amewataka washiriki kujituma wakati wa kuwatafuta watoto hao kwa kuzingatia ugumu wa kazi hiyo.

Mafunzo hayo yanayowasilishwa na wakufunzi kutoka Taasisi ya Elimu ya Watu Wazima, yanawashirikisha walimu wakuu, walimu wa MEMKWA na maafisa elimu wa kata tano za Kitanga, Heri Ushingo, Nyamidaho, Makere na Kagerankanda zenye madarasa ya mpango huo.Katibu tawala wa wilaya ya Kasulu Mughuha Titus akiwa kwenye picha ya pamoja na walimu.

Post a Comment

Previous Post Next Post