" SMAUJATA SHINYANGA YAPANGA MIKAKATI MIPYA DHIDI YA UKATILI, YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU KUKABILI RUSHWA

SMAUJATA SHINYANGA YAPANGA MIKAKATI MIPYA DHIDI YA UKATILI, YAAHIDI KUSHIRIKIANA NA TAKUKURU KUKABILI RUSHWA


Na Mapuli Kitina Misalaba

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga, Bi. Nabila Kisendi, amewataka viongozi wa jumuiya hiyo katika Halmashauri zote za wilaya na mkoa kwa ujumla kuendelea kutoa elimu ya kupinga ukatili wa aina zote katika jamii wanazoishi.

Akizungumza leo Juni 26, 2025, kwenye kikao cha ndani kilichowakutanisha wenyeviti na makatibu wa wilaya zote za Mkoa wa Shinyanga, Bi. Kisendi amesema kuwa huu ni wakati muhimu kwa viongozi wa SMAUJATA kuongeza juhudi katika kutoa elimu ya ukatili kupitia mikutano ya hadhara, shule na taasisi za umma.

“Elimu ya ukatili haipaswi kuishia kwenye makongamano ya kitaifa pekee, bali inapaswa kushuka hadi ngazi ya familia. Kila kiongozi ni balozi wa mabadiliko katika eneo lake,” amesema Bi. Kisendi.

Amesisitiza kuwa jamii ya sasa inakabiliwa na changamoto nyingi za kijamii ikiwemo ukatili wa kijinsia, ndoa za utotoni, unyanyasaji wa watoto na wazee, hivyo ni jukumu la viongozi wa SMAUJATA kuwa mstari wa mbele katika kuelimisha umma na kuhamasisha mabadiliko ya kitabia.

Katika kikao hicho, viongozi wamekubaliana kubuni miradi ya kiuchumi itakayosaidia kuwawezesha wanachama wa SMAUJATA kujitegemea kifedha, sambamba na kusaidia jamii. Mwenyekiti huyo ameongeza kuwa kila mwanachama anapaswa kuwa tayari kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo, ili kuifanya jumuiya hiyo kuwa imara kiuchumi na kijamii.

Kwa upande wake Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea kushirikiana na taasisi za serikali, ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) katika kuelekea kipindi cha uchaguzi, kuhakikisha rushwa haitumiki kuwarubuni wananchi.

“Tunawahimiza wananchi kutoa taarifa za viashiria vyote vya rushwa. SMAUJATA tutasimama bega kwa bega na TAKUKURU kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na haki,” amesema Kapaya.

Kapaya ameongeza kuwa mikoa yote ya Kanda ya Ziwa ambayo ni Mwanza, Shinyanga, Geita, Simiyu, Mara na Kagera, inapaswa kuendelea kuwa chachu ya mabadiliko ya kijamii kwa kutoa elimu ya kupinga ukatili bila kuchoka.

Katibu wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga, George Ntemi, amesema kuwa jumuiya hiyo itaendelea kushikamana katika mapambano dhidi ya vitendo vyote vya ukatili vinavyoshamiri kwenye jamii.

Amesema maazimio yaliyofikiwa katika kikao hicho cha viongozi wa wilaya zote yatafanyiwa kazi kwa vitendo, huku akisisitiza kuwa SMAUJATA Shinyanga iko tayari kuyasimamia kwa nguvu zote ili kuhakikisha jamii inapata uelewa na kinga dhidi ya ukatili.

Aidha, Ntemi amewahimiza wanachama wote wa SMAUJATA ndani ya mkoa wa Shinyanga kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za jumuiya hiyo, zikiwemo kampeni za uelimishaji na utekelezaji wa miradi ya pamoja. Viongozi na taasisi za serikali pia wameombwa kuendelea kushirikiana kwa karibu na SMAUJATA ili kuongeza ufanisi katika kufikia lengo la jamii isiyo na ukatili.

SMAUJATA ni jumuiya inayotekeleza majukumu yake chini ya usimamizi wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, na imekuwa mstari wa mbele kupinga vitendo vya ukatili na kuhamasisha haki na usawa katika jamii ya Watanzania.

Mwenyekiti wa Jumuiya ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii Tanzania (SMAUJATA) Mkoa wa Shinyanga, Bi. Nabila Kisendi, akitoe maelekezo kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025. Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.Katibu wa SMAUJATA Kanda ya Ziwa, Bwana Daniel Kapaya, akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.

Makamu Mwenyekiti wa SMAUJATA Mkoa wa Shinyanga Mzee Mwarabu Akim, akizungumza kwenye kikao cha leo Juni 26, 2025 mjini Shinyanga.




Post a Comment

Previous Post Next Post