Na
Mapuli Misalaba, Shinyanga
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga imesema kwa Mwaka wa fedha 2023/2024 itaanza kupima maeneo ya wananchi ambao
tayari wameshalipia kwa ajili ya kupata hatimiliki zao pamoja na wananchi
wanaodai fidia kwenye utanuzi wa eneo la chuo cha afya Kolandoto.
Kauli hiyo imetolewa leo
na Kaimu Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga Bwana John Tesha kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la Halmashauri
hiyo wakati akijibu swali la diwani wa
kata ya Kolandoto Mhe. Mussa Elias aliyetaka kujua ni lini wananchi wa kata
hiyo watapimiwa maeneo yao ikiwa ni pamoja na kulipwa fidia kwa wananchi
watakaopisha utanuzi wa Chuo cha afya Kolandoto.
“Wananchi
wa kata ya Kolandoto wameshalipa fedha kwa ajili ya kupimiwa maeneo yao fedha
hizi zimelipwa imepita Miaka mitano sasa na hili swali nimekuwa nikiliuliza
mara kwa mara kwenye baraza na sasa kwa kuwa tunaingia kwenye Mwaka mwingine
tena naomba nipate majibu wananchi wa Kolandoto ni lini watakwenda kupimiwa
ardhi zao na kupata hati zao kwa ajili ya manufaa ya familia zao”.
“Kolandoto
tunahitaji kupanua chuo kuwa chuo kikuu wananchi wa maeneo yale
wamekwishakutwaliwa maeneo yao kwa ajili ya upanuzi wa chuo hicho swali langu
kwa sababu mchakato huu ulisimamiwa na Manispaa je ni lini sasa hao wananchi
wanakwenda kulipwa fidia zao kwa sababu ni muda mrefu sasa umepita toka
waahidiwe fidia zao hizi”.Amesema Mhe. Diwani Elias
Kaimu Mkurugenzi Bwana
Tesha amesema Halmashauri hiyo imepanga kuanza kupima maeneo ya wananchi ili kuwapatia
hatimiliki zao huku akibainisha zoezi la kulipa fidia wananchi watakaopisha kwa
ajili ya utanuzi wa eneo la chuo hicho.
“Ni
kweli wananchi wa Kolandoto walihamasishwa kufanya uchangiaji kwa ajili ya
kufanyiwa upimaji au urasimishaji wa maeneo yao sasa eneo lote la Kolandoto
limeingizwa kwenye mradi unaoitwa uboreshaji miliki salama Nchini na mradi huu
unafadhiriwa na Benki ya Dunia na utaanza rasmi Tarehe moja (1) kwezi wa saba
(7) Mwaka huu 2023”
“Mheshimiwa
Diwani ameuliza juu ya wananchi wanaozunguka chuo kile cha afya Kolandoto
ambapo eneo la wananchi wale limeshapimwa lakini wananchi wale hawajalipwa
fidia ni kweli zoezi hilo limeshafanyika na tayari taarifa za wananchi hao zimeshachukuliwa
taarifa hizo zimeingizwa kwenye vikao rasmi vya kamati ya mipango miji takwimu
ziko tayari na Mwaka wa fedha ujao wananchi wale wataanza kulipwa”.amesema
Bwana Tesha
Mstahiki Meya wa Manispaa
ya Shinyanga Bwana Elias Masumbuko pamoja na mambo mengine amekemea na kuagiza
watendaji wa kata kwenda kwenye shule mbalimbali ili kubaini michango
inayochangishwa bila kufuata utaratibu.
“Kuna
maeneo mawili yanasema ukaguzi wa shule ni kama kata tatu au mbili zinaonyesha
kama kuna shule zimekaguliwa kumbe katika kila robo hatuoni utendaji wa kazi
katika sekta hii kuna malalamiko mengi wazazi wanalalamika kwenye kata watoto
wanaambiwa kununua rimu kwenye kata huko watendaji mtusaidie kuna michango mia
tano mia tano mwalimu anaagiza za mitihani kwa nini hizo mia tano mia tano za
nini mwalimu anasema ni kwa ajili ya kuandalia mtihani watendaji wa kata
mtusaidie mtihani upi huo kama kuna
maelekezo hayo TAMISEMI mtuambie sasa na hawa wanaokagua kwenye shule wanakagua
majengo au wanakagua nini watendaji wa kata ndiyo wasaidizi wa mkurugenzi
fuatilieni hili jambo kuna malalamiko mengi sana kwa wazazi”.amesema Meya
Masumbuko
Mstahiki Meya huyo Mhe.
Masumbuko amewasihi madiwani wote wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga
kushirikiana na wazazi katika suala la kusimamia maadili mema ili kuzuia
mmomonyoko wa maadili.
Amewashauri wazazi na
walezi wa watoto katika shule mbalimbali za Manispaa ya Shinyanga kwenye vikao
vyao kuweka sheria na kanuni ndogondogo zitakazowaelekeza wazazi kuwajibika na
lishe ya watoto shuleni.
Leo Baraza la madiwani la
Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga limekaa kikao cha robo ya tatu kwa Mwaka
wa fedha 2022/2023.
Post a Comment