" KATAMBI AONYA WANAODHULUMU MAFUNDI, MAGIC BUILDERS YAJA NA FURSA YA VYETI BURE VETA KWA MAFUNDI SHINYANGA

KATAMBI AONYA WANAODHULUMU MAFUNDI, MAGIC BUILDERS YAJA NA FURSA YA VYETI BURE VETA KWA MAFUNDI SHINYANGA

Na Mapuli Kitina Misalaba

Mafundi nchini wamehimizwa kuendelea kuwa mabalozi wa amani na mshikamano katika jamii, wakielezwa kuwa mazingira ya amani na utulivu ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta ya ujenzi na uchumi wa Taifa kwa ujumla.

Wito huo umetolewa katika semina maalumu iliyoandaliwa na kampuni ya MAGIC BUILDERS, iliyofanyika katika Ukumbi wa Lyakale, Manispaa ya Shinyanga, ambapo mgeni rasmi alikuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Paschal Patrobas Katambi.

Akizungumza katika semina hiyo, Waziri Katambi amesema Serikali haitakuwa tayari kuruhusu kundi dogo la watu wenye maslahi binafsi kuvuruga amani ya nchi kwa kujificha nyuma ya misingi ya haki za binadamu na demokrasia.

Amesema Serikali itaendelea kuhakikisha hali ya usalama na utulivu inaendelea kuimarika nchini ili Watanzania waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi kwa uhuru na amani.

Katika hatua nyingine, Katambi amewataka waajiri kuwathamini mafundi kwa kuwalipa stahiki zao kwa wakati na kwa mujibu wa makubaliano waliyoingia.

Amesema Serikali haitamvumilia mtu au taasisi yoyote itakayowadhulumu mafundi kwa kutowalipa fedha walizokubaliana baada ya kukamilisha kazi zao.

Pia amewahimiza mafundi kufanya kazi kwa uadilifu, kuzingatia viwango vya taaluma pamoja na kuhakikisha wanatumia mikataba rasmi wanapopewa kazi ili kulinda maslahi yao na ya waajiri.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa MAGIC BUILDERS, David Barongo, amesema kampuni hiyo imeamua kuandaa semina hiyo ikiwa ni sehemu ya kuwajengea uwezo mafundi na kuwapa elimu kuhusu haki zao, wajibu wao pamoja na namna ya kujenga kwa kuzingatia ubora na viwango vinavyokubalika.

Amesema mafundi ni nguzo muhimu katika maendeleo ya sekta ya ujenzi, hivyo wanapaswa kuendelea kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ujuzi na ushindani wao katika soko la ajira.

Barongo ameongeza kuwa kampuni hiyo, kwa kushirikiana na Serikali, imeandaa mpango maalumu wa kuwatambua na kuwarasimisha mafundi ambao bado hawana vyeti vya taaluma.

Amesema kupitia ushirikiano huo, mafundi hao watapatiwa mafunzo na fursa ya kupata vyeti vya taaluma bila malipo kupitia Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) Shinyanga.

Kwa mujibu wa Barongo, zoezi hilo la usajili, tathmini na utoaji wa mafunzo litafanyika kwa siku mbili kuanzia Jumanne, Julai 21, 2026, likiwa na lengo la kuongeza idadi ya mafundi wenye sifa na wanaotambulika rasmi nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, SACP Janeth Magomi, amewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kulinda na kudumisha amani, akisisitiza kuwa usalama ni jukumu la kila mwananchi.

Amesema kila mtu ana haki ya kufanya kazi, kuendesha biashara na kutekeleza shughuli zake za kila siku katika mazingira ya utulivu na usalama, hivyo ni muhimu kuepuka vitendo vinavyoweza kuvuruga amani.

Kuhusu masuala ya maandamano, Kamanda Magomi amesema shughuli hizo zinapaswa kufanyika kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni za nchi, huku akiwataka wananchi kutoshiriki vitendo vya uchochezi au uvunjifu wa sheria vinavyoweza kuhatarisha usalama wa watu na mali zao.

Ameongeza kuwa Jeshi la Polisi litaendelea kusimamia utekelezaji wa sheria kwa haki na weledi ili kuhakikisha Mkoa wa Shinyanga unaendelea kuwa salama na wananchi wanaendelea na shughuli zao za maendeleo bila hofu.

Baadhi ya mafundi walioshiriki semina hiyo wameishukuru kampuni ya MAGIC BUILDERS pamoja na Serikali kwa kuandaa mafunzo hayo, wakisema yatawaongezea ujuzi, kuimarisha taaluma zao na kuongeza fursa za ajira.

Wameahidi kuendelea kufanya kazi kwa weledi, uaminifu na kuzingatia maadili ya taaluma huku wakilinda amani ambayo ndiyo msingi wa maendeleo ya sekta ya ujenzi na Taifa kwa ujumla.

Semina hiyo ilihitimishwa kwa burudani kutoka kwa wasanii mbalimbali wakiwemo mchekeshaji Ndaro, pamoja na TX Dullah, Kidege na Azaboi, ambao wametoa burudani iliyowavutia washiriki wa semina hiyo.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhe. Patrobas Katambi, akizungumza na mafundi katika semina iliyoandaliwa na kampuni ya MAGIC BUILDERS mjini Shinyanga

 SHY TALENT FILMS - CONTENT YA MWISHO DRAMA

🥃🍶 TUMIA VINYWAJI BORA VYA KAMPUNI YA EAST AFRICAN SPIRITS – BEI RAFIKI, LADHA SAFI BILA HARUFU MBAYA

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post