Na. Dennis Gondwe -Misalaba
Blog, DODOMA
WATUMISHI wa afya katika Mkoa
wa Dodoma wametakiwa kuhakikisha dawa za tiba zenye asili ya kulevya
zinadhibitiwa ili kuondoa mianya ya dawa hizo kutumika tofauti ya lengo
lililokusudiwa na kusababisha uraibu wa dawa za kulevya katika jamii.
Rai hiyo ilitolewa na Kaimu
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dkt. Nelson Buruku wakati akifungua mafunzo ya
wasimamizi wa dawa za tiba zenye asili ya kulevya katika hospitali na vituo vya
afya vinavyotumia dawa hizo mkoani Dodoma yaliyofanyika katika ukumbi wa Chuo
Kikuu Huria Tanzania, Tawi la Dodoma.
Dkt. Buruku alisema “kwa
kutambua kuwa ninyi watumishi wa afya ni watu wa awali mnaokutana na wagonjwa
na kuwapa matibabu mna jukumu la kuhakikisha dawa za tiba zenye asili ya
kulevya zinadhibitiwa ipasavyo ili kuondoa mianya ya matumizi yasiyo sahihi ya
dawa hizo kwa jamii. Hivyo basi, ninawaomba kupitia mafunzo haya ambayo wengine
ni kwa mara ya kwanza lakini wapo ambao walishawahi kupata mafunzo haya siku za
nyuma kuhakikisha mnayaishi katika utendaji kazi wenu ili kuwezesha matumizi
sahihi ya dawa hizi”.
Alisema kuwa dawa hizo
zinatumika katika kutibu na kupunguza maumivi. “Hivyo, pamoja na faida hiyo,
dawa hizo zisipodhibitiwa vizuri huweza kuleta madhara kwa jamii hasa zikitua
katika mikono isiyo sahihi. Natoa rai kwenu watumishi mnaosimamia dawa hizi
kuepuka vishawishi vitakavyosababisha uchepushwaji wa dawa hizi na kupelekea
mzigo kwa nchi kutibu waraibu wa dawa za kulevya” alisema Dkt. Buruku.
Akiongelea matarajio yake kwa
washiriki, alisema kuwa mafunzo hayo yatatoa uelewa wa pamoja. Alisema kuwa
maazimio yatakayowekwa yatakuwa shirikishi na yatatekelezwa kwa ufanisi ili
kulinda afya ya jamii na kulipunguzia taifa janga la matumizi yasiyo sahihi ya
dawa za tiba zenye asili ya kulevya.
Kwa upande wake Kaimu Meneja
wa Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba (TMDA) Kanda ya Kati, Benedict Brashi alisema
kuwa mamlaka imetoa mafunzo kwa vituo vinavyotumia na kutunza za tiba zenye
asili ya kulevya.
“Mafunzo haya yanahusisha vituo 47, yakijumuisha
maeneo ya namna vituo vinavyoweza kununua dawa, kutunza na kutumia. Dawa hizi
zinaleta madhara na utegemezi. Mafunzo haya tunapitishana kwenye muongozo wa
TMDA unaoshughulikia udhibiti wa dawa hizi ili dawa hizi zisitumike ndivyo
sivyo na zinawafikia walengwa” alisema
Brashi.
Mamlaka ya Dawa na vifaa tiba
Kanda ya Kati inahudumia mikoa minne ya Dodoma, Morogoro, Iringa na Singida
ikiwa na jukumu la kudhibiti ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa za dawa, vifaa
tiba, vitendanishi, tumbaku na mazao yake.

Post a Comment