Na Mapuli Kitina Misalaba
Chama Cha Mapinduzi CCM Wilaya ya Shinyanga mjini leo
Februari 2,2024 kimeadhimisha Miaka 47 ya kuzaliwa kwa Chama hicho ambapo Shughuli hiyo imefanyika sanjari na
zoezi la kupanda miti, kutolewa elimu ya madarasa ya itikadi kwa wanachama na
viongozi wa ngazi za matawi na baadaye Mkutano wa hadhara.
Maadhimisho hayo yamefanyika katika viwanja vya Shule
ya Sekondari Kolandoto Manispaa ya
Shinyanga ambapo Chama hicho kimepanda miti zaidi ya Mia tano kama sehemu ya
kuunga mkono kampeni ya upandaji miti Nchini.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi CCM Wlaya ya
Shinyanga Mjini Mhe. Anord Makombe
akizungumza baada ya zoezi la upandaji miti amehimiza uongozi wa shule hiyo
kutunza miti yote iliyopandwa leo ili iweze kustawi vizuri ambapo hatua hiyo
itasaidia kufikia melengo yaliyokusudiwa katika kupambana na mabadiliko ya
tabia nchi.
Mwenyekiti huyo wakati akizungumza kwenye mkutano wa
hadhara, amesema kuelekea uchaguzi wa Serikali za Mitaa Chama hicho kitachagua
safu ya viongozi bora wenye uwezo, sifa,
utashi na maono, ambao wanakubalika
kwa wananchi.
Pamoja na mambo mengine amesisitiza mchakato wa kuwapata
wenyeviti wa serikali za Mitaa,vijiji na vitongoji pamoja na wajumbe wao
ufanyike kwa kuzingatia maslahi ya wananchi.
“Tutakapochagua
viongozi wabovu tutakapochagua viongozi kwa sababu tu amekuja amekuletea Sukari
amekuletea Chumvi amekuletea Kitenge lakini unajua kabisa mtu huyu uwezo wake
ni mdogo tutakwenda pasipo, kwahiyo
tunachokitaka ninyi wenyewe mkafanye tathimini kwanza mtuletee watu ambao
mnajua kwamba wanakubalika kwa wananchi”.amesema Mwenyekiti
Makombe
Aidha Mwenyekiti Makombe amewakumbusha wazazi na walezi kuhusu
umuhimu wa kupeleka watoto shule kwa kuwa serikali imeweka mazingira wezeshi ya
watoto kujifunzia.
“Ndugu
zangu na wazazi wenzangu niwaombe itakuwa ni aibu tunavyoona shule zimejengwa
vizuri na shule za msingi zipo halafu bado watoto hawaendi shule ni jambo la
aibu mno utakuwa ni mtu wa ajabu mno kushindwa kumpeleka mtoto shule wakati
elimu ni bure kuanzia chekechea mpaka kidato cha sita ni bure kabisa sasa shida
ni nini niwaombe kila mtu awe kiongozi kwa jirani yake ukiona mtoto haendi
shule mripoti haraka sana jirani yako usimuonee aibu tunataka Taifa la watu
wenye weledi haiwezekani mtu anakaa nyumbani hajui kusoma na kuandika yaani
hajui Dunia inakwendaje ni muhimu kila mtu kupata elimu hasa kizazi cha sasa”.amesema
Makombe
Kwa upande wake Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga
Mhe. Elias Ramadhan Masumbuko wakati akizungumza kwenye maadhimisho hayo naye amewakumbusha
wazazi kuendelea kusimamia jukumu la malezi na makuzi bora ya watoto,huku
akisisitiza watoto kupelekwa shule hasa waliochaguliwa kuingia kidato cha
kwanza.
Wakati huo huo amewakumbusha wakazi wa Manispaa ya
Shinyanga kuendelea kuchukua tahadhari ya kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu
ikiwemo kuzingatia usafi katika maisha ya kila siku.
Maadhimisho hayo ya Miaka 47 ya kuzaliwa kwa CCM,
katika Wilaya ya Shinyanga mjini yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Chama
hicho wakiwemo madiwani wa kutoka kwenye kata zote 17 za Halmashauri ya
Manispaa ya Shinyanga.
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga mjini Mhe. Anord Makombe akizungumza kwenye maadhimisho ya miaka 47 ya CCM ambayo yamefanyika katika kata ya Kolandoto.
Post a Comment