" INASIKITISHA MTOTO WA MIAKA MITANO AFARIKI KWA KULIWA NA FISI JIONI WILAYANI SHINYANGA

INASIKITISHA MTOTO WA MIAKA MITANO AFARIKI KWA KULIWA NA FISI JIONI WILAYANI SHINYANGA


Na Moshi Ndugulile

Mtoto Mmoja mwenye umri wa Miaka Mitano Shamimu Tumaini Jumaissa mkazi wa kijiji cha Ibanza kata ya Mwamala Wilaya ya Shinyanga ameuawa kwa kushambuliwa na fisi wakati akiokota kuni jirani na nyumbani kwao.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa kijiji cha Ibanza  Bwana Hassan Issa Barabara amesema tukio hilo limetokea jana majira ya Saa kumi na mbili jioni wakati Mtoto huyo akiwa na mwenzake wakiokota kuni hatua chache kutoka nyumbani kwao,  ndipo fisi huyo alipomvamia na kumburuza Mtoto huyo na kisha kukimbia naye vichakani.

Amesema baada ya kutokea tukio hilo wanakijiji walianza kufuatilia michirizi ya damu na ndipo walipomkuta Mtoto huyo akiwa amepoteza maisha huku akiwa ameshambuliwa vibaya sehemu za uso na kichwani.

“Watoto hao wawili walikuwa wanaokota kuni kwenye muda wa saa kumi na mbili inaelekea saa moja ghafla akatokea Fisi kale katoto kana umri wa Miaka mitano harakati za kukimbia Yule mwenzake anaumri wa Miaka Tisa yeye alifanikiwa kukimbia na bahati nzuri kulikuwa na Mama jirani akakasikia kale katoto kanalia kuangalia akamuona Fisi amemny’ata sasa huyo mama akaanza kupiga kelele Fisi nayeye akawa anatokomea”.

“Baada ya hapo watu sasa tukajitokeza baada ya kusikia kelele usiku uliingia Fisi Yule alitokomea na mtoto tukaanza juhudi za kumsaka huku wasalama wanapiga penga tukakusanyikana kwenye tukio tukaendelea kusaka muda kama wa masaa matatu haonekani baadaye tukarudi sehemu ya tukio tukaanza tena kufuatilia damu mpaka alipo tukamkuta na Fisi anaendelea kumla huyo mtoto lakini Fisi alikimbia baada ya kutuona ikabidi tu tumchukue mtoto kumrudisha Nyumbani”.amesema Mwenyekiti Hassan

Misalaba Media imezungumza na Felista Elias Mkazi wa kijiji cha Ibanza ambaye  ameshuhudia tukio hilo  na hapa  ameeleza kuwa hakupata msaada wa haraka kumwokoa mtoto huyo kwa kuwa wakati huo wanaume wa kijiji hicho walikuwa mbali kwenye shughuli za Sungusungu.

“Mtoto aliyefanyiwa hilo tukio mimi ni jirani yao niliwaona wanaokota kuni baadaye walipeleka hizo kuni baada ya hapo wakaenda kurudi tena, waliporudi mara ya pili kidogo tu dakika kama moja hivi nikasikia wameanza kulia walikuwa wawili ndiyo nikasogea barabarani kuwauliza mnalilia nini sasa kale katoto kakubwa kakawa hakanisemeshi kanakimbia tu baada ya kukasikia kale kengine kanalia ndiyo nikageuka kuangalia nikaona Fisi amekabeba akawa anakaburuza mimi nilishindwa namna ya kufanya nikaanza kupiga tu kelele kwa bahati mbaya wanaume wote hawakuwepo ilikuwa imegongwa kengele ya Sungusungu walijitokeza tu wanawake ila badaye watu wakawa wengi na wanaume walikuja”.amesema Felista Elias

Afisa Mtendaji wa kijiji cha Ibanza Bi. Tausi Kabadi  amesema baada ya tukio hilo kutokea serikali ya kijiji imetoa taarifa kwa jeshi la polisi na kisha kuwasiliana na maafisa wa wanyamapoli na Maliasili na kwamba kwa hatua za awali Sungu sungu wameanza kumsaka mnyama huyo.

 

 

Post a Comment

Previous Post Next Post