Na Daniel Sibu, Misalaba Media
Taasisi ya Flaviana Matata imekabidhi mradi wa uboreshaji wa miundombinu ya maji,
afya na usafi wa mazingira (WASH) katika Shule ya Sekondari Salawe, mkoani
Shinyanga, unaolenga kuboresha mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi, hususan
wasichana.
Makabidhiano ya mradi
huo yamefanyika Julai 23, 2025 yakiongozwa na mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya
Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro na kwamba mradi huo umetekelezwa na Taasisi ya
Flaviana Matata kwa ufadhili wa shirika la kimataifa la Diamonds
Do Good.
Meneja Miradi kutoka
Taasisi ya Flaviana Matata, Lineth Masala amesema kupitia mradi huo, shule
imenufaika na ujenzi wa matundu 12 ya vyoo vya kisasa, sehemu ya kunawia
mikono, chumba maalumu kwa wanafunzi wenye ulemavu, chumba cha wasichana
kujisitiri wakati wa hedhi pamoja na sehemu ya kuchomea taka, ikiwemo taulo za
kike zilizotumika.
Lineth Masala, amesema taasisi hiyo imekuwa mstari
wa mbele kusaidia watoto wa kike kupitia miradi ya elimu, huku lengo likiwa ni
kuhakikisha mazingira ya shule yanakuwa salama, safi na yenye staha kwa kila
mtoto.
Akizungumza wakati wa
hafla ya makabidhiano, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Wakili Julius Mtatiro amesema
mradi huo umeonyesha ushirikiano mzuri kati ya taasisi binafsi na serikali
katika kuleta maendeleo kwenye sekta ya elimu, huku akisisitiza umuhimu wa
kuweka mazingira bora kwa wanafunzi wa kike.
Baadhi ya wanafunzi wa
Shule ya Sekondari Salawe akiwemo Maryciana Juma wameeleza furaha yao kwa
kupatiwa miundombinu rafiki, hususan chumba cha kujisitiri wakati wa hedhi,
wakisema hatua hiyo itawasaidia kuhifadhi utu na kuongeza mahudhurio shuleni.
Post a Comment