Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Bw. Kisena Mabuba, amewaagiza watendaji wote wa Kata kwenda kuyahuisha madawati na mabaraza ya watoto katika shule zote za msingi na Sekondari zilizopo katika Halmashauri hiyo.
Kisena ametoa agizo hilo kufuatia hoja iliyotolewa na Mwenyekiti wa Baraza la watoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Amina Hamis, aliyeeleza kulegalega kwa mabaraza hayo pale wadu wanapoondoka.
Amina alitoa hoja hiyo kupitia Kikakao cha robo mwaka cha Kamati ya mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) kilichowakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo mashirika na taasisi zaidi ya 9, zinazotekeleza miradi ya kuzuia ukatili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kwa ufadhili wa mfuko wa ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T)
Kutokana na hoja hiyo ya Mwenyekiti wa baraza la watoto, Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga alibainisha kuwa, kwa kuwa madawati na mabaraza ya watoto katika shule za msingi na Sekondari yana umuhimu mkubwa katika kusaidia juhudi za kulinda haki na usalama wa watoto wawapo shuleni na nyumbani, haiwezekani kuona mabaraza hayo yanakufa kwa sababu tu ya wadau kumaliza miradi yao.
Amemtaka kila Mtendaji wa Kata kwenda kusimamia zoezi la kuhuishwa kwa mabaraza hayo kwenye eneo lake ili yawe endelevu na ameahidi kupita kila shule ili kujiridhisha kutekelezwa kwa agizo hilo.
SAUTI YA MKURUGENZI KISENA MABUBA KUHUSU KUHUISHA MABARAZA
Kisena amewataka watendaji wote wa Serikali kutambua kuwa, MTAKUWWA ni mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto, hivyo wanapaswa kushirikiana kwa karibu na wadau wanaosaidia mpango huo wa Serikali.
SAUTI YA MKURUGENZI KISENA MABUBA KUHUSU WATENDAJI KUSHIRIKIANA NA WADAU
Katika hatua nyingine, Mkurugenzi huyo amewaagiza Watendaji wa Kata kwa kushirikiana na maafisa Maafisa maendeleo na maafisa ustawi wa Jamii kwenda kuzisimamia Kamati za ulinzi zilizopo katika maeneo yao, ili na zenyewe sehemu ya kusaidia juhudi za kutokomeza vitendo vya Ukatili kwa wanawake na watoto, na wawe wanatoa mrejesho mara kwa mara wa utendaji wa kamati hizo.
SAUTI YA MKURUGENZI KUHUSU KUSIMAMIA KAMATI ZA ULINZI
Kwa upande wake Mratibu wa WFT-T wa mkoa wa Shinyanga Bi.Glory Mbia, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kupitia viongozi wake ikiwemo Mkurugenzi wa sasa Bw. Kisena Mabuba kwa kuvaa uhusika na kushirikiana kikamilifu na wadau katika kufanikisha juhudi za kutokomeza vitendo vya ukatili katika Halamshauri hiyo, hatua ambayo imewezesha mafanikio makubwa yaliyoleta matokeo chanya.
SAUTI YA GLORY MBIA
Mbia ametoa wito kwa Halmashauri hiyo kuendelea kuzitumia taarifa na tafiti mbalimbali zinazotolewa na wadau wa kupinga ukatili ikiwemo WFT-T ili kuleta mabadiliko, pamoja na kuendeleza utaratibu wa kukutana na wadau mara kwa mara hata pale wanapofikia mwisho wa utekelezaji wa miradi yao.
Kikakao cha robo mwaka cha Kamati ya mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, kimewakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo Kamati ya MTAKUWWA ngazi ya Halmashauri, wawakilishi wa wanawake na watoto, viongozi wa dini, watendaji wa Kata, Maafisa maendeleo ya Jamii pamoja na taasisi zinazotokeleza miradi ya kupinga ukatili katika Halmashauri hiyo akiwemo mdau mkuu WFT-T, Jeshi la Polisi dawati la Jinsia, Redio Faraja, Club ya waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga, TAI, YWL, GCI, YAWE, WEADO na RAFIKI SDO.

Wadu wakiwa kwenye kikao

Mdau akichangia namna ambavyo taasisi/ Mashirika mbalimbali ambayo yanatekeleza mradi wa kupinga ukatili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa ufadhili wa WFT-T hususani vyombo vya Habari ikiwemo Redio Faraja ambavyo wamesaidia kupeleka elimu ya kupinga ukatili kwa wananchi

Wawakilishi wa makundi mbalimbali ikiwemo watoto wakiwa kwenye kikao, kulia ni Mwenyekiti wa Baraza la Watoto katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Amina Hamis ambaye ni mwanafunzi katika shule ya Msingi Puni

Mwenyekiti wa Baraza la watoto wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Amina Hamis akiwasilisha hoja kwenye kikao

Veronica Massawe kutoka shirika la YWL akichangia hoja kwenye kikao

Mratibu wa WFT-T Mkoa wa Shinyanga Glory Mbia akichangia hoja kwenye kikao

Mratibu wa WFT-T Mkoa wa Shinyanga Glory Mbia akizungumza kwenye kikao kwa niaba ya WFT-T

Meneja Vipindi wa Redio Faraja Simeo Makoba akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili unaotekelezwa na chombo hicho

Mratibu wa Club ya waandishi wa Habari mkoa wa Shinyanga Estomine Henry akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kupinga ukatili unaotekelezwa na Club hiyo

Baadhi ya wadau wakiwasilisha taarifa zao

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu misalabamedia@gmail.com au Whatsapp namba 0745594231
Post a Comment