Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga Kisena Mabuba. amewaomba wadau wanaotekeleza miradi mbalimbali ya kupinga ukatili kwa wanawake na watoto katika Halmashauri hiyo, kuiangalia kwa namna ya pekee kata ya Lyamidati ambayo inakabiliwa na visa vingi vya Ukatili.
Kisena ametoa ombi hilo wakati akizungumza katika Kikakao cha robo mwaka cha Kamati ya mpango wa taifa wa kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA) kilichowakutanisha wadau mbalimbali ikiwemo mashirika na taasisi zaidi ya 9, zinazotekeleza miradi ya kuzuia ukatili katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga kwa ufadhili wa mfuko wa ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T)
Mkurugenzi huyo wa Halmashauri ya Shinyanga ameeleza kuwa, jamii ya watu wa Kata ya Lyamidati inahitaji kusaidiwa ili iondokane na maovu ambayo yanachangia kufanyika kwa ukatili, kutokana na matukio mengi ambayo yamekuwa yakitokea katika kata hiyo.
Amewaomba wadau washirikiane na Serikali na kuichukulia kata hiyo kama kanda maalum, ambayo inatakiwa kutupiwa jicho na kila mdau anayetekeleza mradi wa kupinga vitendo vya ukatili kwa wanawake na watoto.
SAUTI YA MKURUGENZI KISENA MABUBA KUHUSU WADAU KUISAIDIA LYAMIDATI
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ni moja ya maeneo ya nchi ambayo yananufaika na miradi mbalimbali ya kupinga ukatili inayofadhiliwa na Mfuko wa ruzuku kwa wanawake Tanzania (WFT-T) kupitia taasisi mbalimbali za serikali na zisizo za kiserikali zinazoshirikiana na Halmashauri hiyo katika kusaidia mpango wa Serikali wa kutokomeza Ukatili kwa wanawake na watoto (MTAKUWWA)
Licha ya changamoto hiyo, WFT-T inajivunia mafanikio makubwa kutokana na mabadiliko chanya ambayo yameanza kuonekana kupitia tafiti mbalimbali, tangu ilipoanza kutoa ruzuku kwa wadau wanaotekeleza miradi ya kutokomeza ukatili kwenye Halmashauri hiyo miaka mitano iliyopita.
Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ilikuwa ni moja ya maeneo ambayo yalikuwa na kiwango kikubwa cha ukatili kwa wanawake na watoto katika mkoa wa Shinyanga, hali inayochangiwa na mfumo dume uliorithiwa kutoka kwa mababu, kukosa elimu pamoja na mchanganyiko wa watu wa jamii mbalimbali ya wakulima, wafugaji na wachimbaji wadogo wa madini ya aina ya dhahamu yanayopatikana katika baadhi ya maeneo.
Visa vya ukatili ambavyo vilikuwa vinaripotiwa mara kwa mara katika Halmashauri hiyo ni pamoja mauaji ya wanawake vikongwe, ndoa na mimba za utotoni, ukatili wa kiuchumi, kimwili, kingono na kisaikolojia kwa wanawake, watoto wa kike kutopelekwa shule na ukatili wa aina mbalimbali ikiwemo wa kingono kwa watoto.
Hata hivyo juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau zinaelezwa kusaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza hali hiyo, kutokana na hatua mbalimbali zinazochukuliwa ikiwemo kupanua wigo wa kutoa elimu kwa jamii.

Wadau wakiwa kwenye kikao

Ikiwa unatukio lolote au jambo lolote tuma kupitia Barua pepe yetu misalabamedia@gmail.com au Whatsapp namba 0745594231
Post a Comment