Ticker

6/recent/ticker-posts

KANISA KATOLIKI JIMBO LA SHINYANGA LAPATA MAPADRE WAPYA 11

Kanisa Katoliki Jimbo la Shinyanga, limepata jumla ya Mapadre wapya 11 kwa wakati mmoja, kufuatia waliokuwa Mashemasi wa Jimbo kupewa Daraja la Upadre na Askofu wa Jimbo la Shinyanga Mhashamu Liberatus Sangu hii leo.
Misa ya utolewaji wa Daraja la Upadre imefanyika katika uwanja wa Kanisa la Mtakatifu Bikra Maria Mwombezi wa neema zote (Maria Mediatrix) Buhangija mjini Shinyanga, na imehudhuriwa na Mapadre, Mashemasi, Watawa, Mafrateri na waamini kutoka sehemu mbalimbali za ndani na nje ya Jimbo la Shinyanga.
Mapadre hao wapya ni Paschal Masunga wa Parokia ya Gula ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Lubaga mjini Shinyanga, Paschal Mahalagu wa Parokia ya Mwanangi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi mkoani Simiyu, Paschal Ntungulu wa Parokia ya Shishiyu ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Maganzo Wilayani Kishapu mkoani Shinyanga, Paschal Salyungu wa Parokia ya Mwamapalala ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mwanangi wilayani Busega mkoani Simiyu na Peter Sayi wa Parokia ya Mtakatifu John-Bariadi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mhunze wilayani Kishapu mkoani Shinyanga.
Wengine ni Japhet Nyarobi wa Parokia ya Mtakatifu Luka-Bariadi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Kitangili mjini Shinyanga, Philemon Nkuba wa Parokia ya Buhangija ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mwanhuzi Wilayani Meatu mkoani Simiyu, Musa Majura wa Parokia ya Gula ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko Msaidizi wa Parokia ya Ndala mjini Shinyanga, James Chingila wa Parokia ya Mipa ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Kilulu Wilayani Bariadi mkoani Simiyu, James kija wa Parokia ya Chamugasa ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Mtakatifu John-Bariadi mkoani Simiyu na Osward Nkelege wa Parokia ya Bugisi ambaye ametumwa kwenda kuwa Paroko msaidizi wa Parokia ya Salawe iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga (Vijijini)
Awali kabla ya kuwatuma, Askofu Sangu aliwataka Mapadre hao kuendelea kupokea malezi kutoka kwa Mapadre wenzao, ambapo pia ametumia nafasi hiyo kuwashukuru wale wote waliochangia na kuwawezesha kufikia daraja hilo wakiwemo wazazi wao, Mapadre wa Jimbo na wa Seminari walizopita, pamoja na waamini.
Askofu Sangu amemshukuru Mungu kwa neema na baraka ambazo anaendelea kulijalia Jimbo Katoliki Shinyanga ikiwemo kwa zawadi hiyo ya Mapadre wapya, ambapo amewaomba waamini kuendelea kusali kuombea miito ili Kanisa liendelee kupata Mapadre.
Pia amewakumbusha waamini wajibu walionao wa kutunza na kulinda tunu ya ndoa na famila ambayo ndiyo chimbuko la miito yote ndani ya Kanisa, ikiwemo kuwalea watoto wao kwa kuzingatia misingi ya Imani na maadili mema.
Ni mara ya kwanza kwa Jimbo Katoliki Shinyanga kupata idadi kubwa ya Mapadre kwa wakati mmoja, tangu kuanzishwa kwake mwaka 1956.



























Post a Comment

0 Comments