" FURSA ZA UJUZI KWA VIJANA: VETA SHINYANGA YAPANUA MILANGO YA AJIRA NA KUJIAJIRI

FURSA ZA UJUZI KWA VIJANA: VETA SHINYANGA YAPANUA MILANGO YA AJIRA NA KUJIAJIRI


Na Mapuli Kitina Misalaba

Katika kukabiliana na changamoto ya ajira kwa vijana, Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) kupitia Chuo cha Ufundi Stadi Shinyanga imeendelea kupanua wigo wa mafunzo ya ufundi stadi ili kuwawezesha vijana kujiajiri na kuajiriwa katika sekta mbalimbali za uzalishaji.

Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Richard Mbughuni amesema Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan imeweka msisitizo mkubwa katika elimu ya ujuzi kama nyenzo muhimu ya kukuza ajira na uchumi wa taifa.

Amesema katika hotuba yake ya Bunge ya Novemba 14, 2025, Rais alisisitiza umuhimu wa kuunganisha mafunzo ya ufundi stadi na miradi mikakati ya kitaifa ikiwemo reli ya kisasa (SGR), bandari, uchumi wa buluu, madini na gesi, hatua inayofungua fursa pana kwa wahitimu wa vyuo vya ufundi stadi.

Mbughuni ameeleza kuwa VETA ni wakala wa Serikali ulioanzishwa kwa Sheria ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi, Sura ya 82, ukiwa na jukumu la kuratibu, kugharamia na kutoa mafunzo ya ufundi stadi nchini.

“Kwa lugha rahisi, VETA ndiyo inazalisha watu wanaojenga Tanzania kwa vitendo. Nyumba, barabara, umeme, mashine viwandani na hata huduma za utalii zinategemea mafundi stadi,” amesema.

Ameongeza kuwa dira ya VETA ni kuona Tanzania yenye mafundi stadi mahiri na wa kutosha, huku kaulimbiu ikiwa ni ‘Ufundi Stadi, Fursa Kama Zote, Kwa Watu Wote’.

Katika kupanua fursa kwa vijana mkoani Shinyanga, chuo hicho kimeongeza uwezo wa udahili kufuatia upanuzi wa miundombinu uliofanyika kupitia mradi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB).

Kabla ya upanuzi huo, chuo kilikuwa na uwezo wa kudahili wanafunzi 400 wa kozi za muda mrefu na chini ya 1,200 wa kozi za muda mfupi kwa mwaka. Hivi sasa, uwezo umeongezeka hadi wanafunzi 545 wa muda mrefu na zaidi ya 3,000 wa muda mfupi kwa mwaka.

Kutokana na ubora wa mafunzo, chuo hicho hupokea pia wanafunzi wa kozi za muda mfupi kutoka nchi za Afrika Mashariki na Kati, hatua inayochochea ajira ndani na nje ya nchi.

Mbughuni amesema VETA Shinyanga imeendelea kuboresha na kuanzisha kozi mpya zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira, zikiwemo umeme wa majumbani na viwandani, uashi, useremala, ushonaji na ubunifu wa mavazi, uchomeleaji na uundaji vyuma, ufundi bomba, pamoja na ukataji na ung’arishaji wa madini vito.

Aidha, chuo kimeanzisha kozi mpya za ufundi magari, umeme wa magari na utengenezaji pamoja na ukarabati wa barabara ili kukidhi mahitaji ya sekta ya ujenzi na miundombinu.

Katika kuhakikisha hakuna kijana anayeachwa nyuma, VETA Shinyanga imetoa mafunzo kwa makundi maalumu wakiwemo vijana wasio na ajira, wanawake na vikundi vya ujasiriamali.

Programu ya Wanawake na Samia ilinufaisha washiriki 368, huku mradi wa bomba la mafuta wa EACOP ukitoa mafunzo kwa washiriki 20 (wanaume 16 na wanawake 4), wote wakipatiwa ujuzi wa kuwawezesha kujiajiri au kuajiriwa.

Chuo pia kinaendelea kushirikiana na migodi, makampuni ya ujenzi, karakana binafsi na taasisi za umma katika utoaji wa Mafunzo kwa Vitendo (IPT) na mfumo wa Uanagenzi Pacha (DATS), unaowawezesha wanafunzi kupata uzoefu wa moja kwa moja mahali pa kazi.

Kupitia utaratibu wa Recognition of Prior Learning (RPL), mafundi waliopata ujuzi nje ya mfumo rasmi hupimwa na kuthibitishiwa uwezo wao kwa kupewa vyeti vinavyotambulika kitaifa, hatua inayowawezesha kushiriki zabuni na kupata ajira rasmi.

Serikali kupitia VETA Makao Makuu imeendelea kuboresha karakana, madarasa na kununua vifaa vya kisasa vya kufundishia na kujifunzia ili kuongeza ubora wa mafunzo na idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa.

Mbughuni amesisitiza kuwa dunia ya leo inahitaji zaidi uwezo wa kufanya kazi kuliko vyeti pekee.

“Ujuzi ni mtaji, ujuzi ni ajira, ujuzi ni kujitegemea na ujuzi ni heshima,” amesema.

Ametumia nafasi hiyo kuwahamasisha vijana kujitokeza kujiunga na VETA Shinyanga ili kupata stadi zitakazowawezesha kujenga maisha yao na kuchangia maendeleo ya taifa.

Amesema kupitia uwekezaji wa Serikali ya Awamu ya Sita, VETA imekuwa injini ya kuzalisha ajira na kukuza uchumi shindani.

“Ninawaomba wanahabari muendelee kuwa mabalozi wa kuelimisha jamii kuhusu fursa hizi, ili kila kijana ajue kuwa mustakabali wake uko mikononi mwake. VETA Shinyanga ipo kumwezesha — VETA Shinyanga, Kazi Mkononi,”

Mkuu wa Chuo cha VETA Shinyanga, Abraham Richard Mbughuni akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Machi 2, 2026.




 

  • Wasiliana nasi:
    📍 East African Spirits (T) Ltd
    📞 +255 767 650 806 | +255 652 096 254

Post a Comment

Previous Post Next Post