" SERIKALI, WADAU SHINYANGA WAJIPANGA KUPAMBANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

SERIKALI, WADAU SHINYANGA WAJIPANGA KUPAMBANA NA USAFIRISHAJI HARAMU WA BINADAMU

Na Mapuli Kitina Misalaba

Wadau mbalimbali mkoani Shinyanga wametakiwa kuendelea kuimarisha ushirikiano katika kuzuia na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu pamoja na kuhamasisha uhamiaji salama, ili kulinda haki za wanawake, watoto, vijana na makundi mengine yaliyo katika mazingira hatarishi.

Wito huo umetolewa na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Rafael Msela, wakati akifunga semina ya kimkoa kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu (TIP) na Uhamiaji Salama iliyowakutanisha wawakilishi wa taasisi za serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, mahakama, ofisi ya mashtaka, uhamiaji, ustawi wa jamii, maendeleo ya jamii, asasi za kiraia, viongozi wa dini pamoja na vyombo vya habari.

Akizungumza katika hafla ya kufunga semina hiyo, Msela amewashukuru waandaaji ambao ni Shirika la Community of Volunteers for the World (CVM), CHODAWU na Sekretarieti ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Watu (ATS) chini ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa kuandaa mafunzo hayo yaliyolenga kuongeza uelewa kuhusu usafirishaji haramu wa binadamu na uhamiaji salama.

Amesema mada zilizowasilishwa zimewajengea washiriki uwezo wa kutambua mbinu zinazotumiwa na wahalifu, namna ya kuwabaini waathirika pamoja na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika kuzuia, kulinda na kushughulikia matukio ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Msela alisema usafirishaji haramu wa binadamu si tatizo la taasisi moja, bali ni changamoto inayohitaji ushirikiano wa sekta zote kwa kuwa waathirika wake wakubwa ni watoto, wasichana, wanawake na vijana wanaodanganywa kwa ahadi za ajira au maisha bora na baadaye kuingia katika mazingira ya unyonyaji, ukatili na kunyimwa haki zao za msingi.

Ameeleza kuwa katika Mkoa wa Shinyanga bado zipo changamoto zinazohusiana na ajira za watoto katika sekta zisizo rasmi pamoja na hatari zinazotokana na uhamiaji usio salama, hivyo elimu inayotolewa kupitia semina hiyo inapaswa kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Amewataka washiriki kuhakikisha maarifa waliyopata hayaishii ndani ya ukumbi wa mafunzo bali yanatumika katika maeneo yao ya kazi na kwenye jamii kwa kutoa elimu kuhusu viashiria vya usafirishaji haramu wa binadamu, kutambua mapema waathirika na kuchukua hatua za haraka pale viashiria vinapoonekana.

Aidha, ametoa wito kwa Serikali, vyombo vya ulinzi na usalama, mahakama, ofisi ya mashtaka, asasi za kiraia, taasisi za dini, vyombo vya habari pamoja na washirika wa maendeleo kuendelea kuimarisha ushirikiano kwa kubadilishana taarifa kwa wakati, kuimarisha mifumo ya rufaa kwa waathirika na kutekeleza wajibu wa kila mdau katika mapambano dhidi ya uhalifu huo.

Msela pia ameeleza kufurahishwa na kuimarishwa kwa Kikosi Kazi cha Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu (TIP Working Group), akisema kitakuwa jukwaa muhimu la kuratibu utekelezaji wa maazimio yaliyofikiwa wakati wa semina hiyo.

Akitoa mada kuhusu uhamiaji salama, Mrakibu wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Issa Kisiroti, amesema bado wapo baadhi ya wananchi wanaokata hati za kusafiria (paspoti) kwa kufuata taratibu zote za kisheria, lakini wanapofika mipakani huamua kutumia njia zisizo rasmi maarufu kama njia za panya, jambo ambalo ni kosa la kisheria.

Amefafanua kuwa sheria za uhamiaji zinamtaka kila mwenye paspoti kutumia vituo rasmi vya mipakani anapoingia au kutoka nchini, na anayekiuka utaratibu huo anaweza kuchukuliwa hatua za kisheria kama anavyofanyiwa mtu anayejihusisha na biashara ya magendo.

Kisiroti amesema Idara ya Uhamiaji imeendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia kampeni ya "Mjue Jirani Yako", inayolenga kuwahamasisha wananchi kuwafahamu watu wanaoishi katika maeneo yao na kutoa taarifa kwa mamlaka wanapobaini wageni au watu wanaowatilia shaka ili hatua za kisheria zichukuliwe mapema.

Aidha, ameonya kuwa baadhi ya watumishi wasiokuwa waadilifu wamekuwa wakishirikiana na wasafirishaji haramu wa binadamu kwa kupokea rushwa na kuwasaidia kuvuka mipaka kinyume cha sheria, akisisitiza kuwa vitendo hivyo ni makosa yanayochukuliwa hatua kali za kisheria.

Ameongeza kuwa Tanzania imekuwa ikipokea wahamiaji haramu kutoka nchi jirani ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Rwanda, lakini elimu inayoendelea kutolewa imechangia kupungua kwa matukio hayo kutokana na wananchi kuelewa umuhimu wa kutumia nyaraka halali za kusafiria, ikiwemo hati za muda mfupi.

Naye mwezeshaji kutoka Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Providence Simbila, alisema kusafiri si kosa, bali kosa ni kutumia udanganyifu, vitisho au mbinu nyingine haramu kumsafirisha mtu kwa lengo la kumtumikisha au kumnyonya.

Amesema sheria ya Kupambana na Usafirishaji Haramu wa Binadamu inaweka adhabu kwa wahusika, ikiwemo kifungo cha kuanzia miaka mitatu au adhabu nyingine kwa mujibu wa sheria.

Kwa upande wake, mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma Ally, amesema kupitia mradi wa EmPoWedeD II, shirika hilo linaendelea kuwawezesha wasichana wanaofanya kazi za majumbani kutambua haki zao za msingi, kupata mikataba ya ajira na kuboresha mazingira yao ya kazi.

Amesema wasichana wengi wanaofanya kazi za majumbani bado wanakabiliwa na mishahara midogo, ukosefu wa mikataba ya kazi na kutofahamu haki zao kama wafanyakazi, jambo linalowaweka katika hatari ya kunyonywa na kudhurumiwa.

Mwajuma amesema mradi huo utatekelezwa kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2026, ukiwa na shughuli mbalimbali zinazolenga kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu na kuhakikisha wafanyakazi wa majumbani wanalindwa kwa kuzingatia sheria za kazi na haki za binadamu.

Ameongeza kuwa kupitia mradi huo, wafanyakazi wa majumbani wanawezeshwa kupata elimu kuhusu haki zao, mafunzo ya ujuzi kupitia VETA, ajira zenye staha pamoja na elimu ya uhamiaji salama ili kupunguza uwezekano wa kudhurumiwa na kuingia kwenye mazingira ya usafirishaji haramu wa binadamu.

Semina hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali za kuendelea kujenga uwezo wa taasisi na jamii katika kuzuia, kutambua na kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Rafael Msela, akizungumza wakati wa kufunga semina ya kimkoa kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu (TIP) na Uhamiaji Salama leo Julai 8, 2026 mjini Shinyanga.Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, Rafael Msela, akizungumza wakati wa kufunga semina ya kimkoa kuhusu Usafirishaji Haramu wa Binadamu (TIP) na Uhamiaji Salama leo Julai 8, 2026 mjini Shinyanga.Mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma Ally, akiwasilisha mada kuhusu ulinzi wa wafanyakazi wa majumbani, haki za wafanyakazi na juhudi za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu kupitia mradi wa EmPoWedeD II.Mwezeshaji kutoka Shirika la CVM, Mwajuma Ally, akiwasilisha mada kuhusu ulinzi wa wafanyakazi wa majumbani, haki za wafanyakazi na juhudi za kuzuia usafirishaji haramu wa binadamu kupitia mradi wa EmPoWedeD II.Mrakibu wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Issa Kisiroti, akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia njia halali za kusafiri na kuzingatia sheria za uhamiaji.Mrakibu wa Uhamiaji Mkoa wa Shinyanga, Issa Kisiroti, akitoa elimu kuhusu umuhimu wa kutumia njia halali za kusafiri na kuzingatia sheria za uhamiaji.











 

Post a Comment

Previous Post Next Post