Na Mapuli Kitina Misalaba
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la
Shinyanga mjini kimeeleza hofu yake juu ya changamoto zinazojitokeza katika
zoezi la uandikishaji wa wapiga kura, kikidai kuwa baadhi ya mawakala wake
wananyimwa takwimu sahihi na wasimamizi wa vituo vya kujiandikisha.
Madai haya yameibua mjadala mzito kuhusu ufanisi na
uwazi wa zoezi hili muhimu katika maandalizi ya uchaguzi wa serikali za mitaa
unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa CHADEMA jimbo la
Shinyanga mjini, Bwana Hamis Ngunila, pamoja na Katibu wa jimbo hilo, Bwana
Sebastian Polepole, matatizo haya yamejitokeza katika vituo kadhaa vya
uandikishaji vilivyopo ndani ya jimbo hilo.
Wakiwa wanazungumza na Misalaba Media, viongozi hao
wameeleza kuwa mawakala wa chama hicho wamekuwa wakinyimwa taarifa muhimu
zinazohusiana na idadi ya wananchi wanaojitokeza kujiandikisha na kuboresha
taarifa zao.
Bwana Ngunila ameongeza kuwa bila kuwa na takwimu
sahihi na zinazolingana, itakuwa vigumu kuhakikisha uwazi na usawa katika
uchaguzi ujao wa serikali za mitaa.
Bwana Polepole naye ameongeza kwa kusema,
"Tunakabiliana na hali ambapo mawakala wetu wanakosa ushirikiano kutoka
kwa wasimamizi wa vituo, hii inazua wasiwasi mkubwa juu ya uwazi wa zoezi hili
na kuleta mashaka juu ya matokeo ya mwisho."
CHADEMA imemwomba msimamizi mkuu wa zoezi hilo jimbo
la Shinyanga mjini kuchukua hatua za haraka na kuhakikisha kuwa mawakala wa
vituo vya uandikishaji wanatoa ushirikiano kwa mawakala wa vyama vyote, ikiwemo
CHADEMA, ili kuhakikisha takwimu zinazopatikana ni sahihi na zinafanana ili kuepuka
mkanganyiko wowote na kuhakikisha kuwa kila kura inahesabika kwa haki.
Mbali na kutoa wito kwa wasimamizi wa vituo vya uandikishaji,
CHADEMA pia imewaomba wananchi wa Shinyanga kujitokeza kwa wingi kushiriki
katika zoezi hili la uandikishaji.
Bwana Hamis Ngunila, amesisitiza umuhimu wa wananchi
kuhakikisha wanajiandikisha na kuboresha taarifa zao, ili wawe na sifa za
kupiga kura katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
"Hii ni haki yenu ya kikatiba. Ni muhimu
kuhakikisha mnashiriki katika mchakato huu kwahiyo tunawaomba mjitokeza kwa
wingi kwenye vituo”. amesema Ngunila
Bwana Ngunila pia amehitimisha kwa kusema kuwa chama
hicho kitaendelea kufuatilia kwa karibu zoezi hili na kuhakikisha kuwa haki
inatendeka.
"Hatutakubali
udanganyifu au ukiukwaji wowote wa haki za wapiga kura, tutaendelea kusimamia
maslahi ya wananchi na kuhakikisha kuwa kila mwananchi anapata fursa ya
kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao," amesema
Ngunila.
Hali hii inakuja wakati ambapo maandalizi ya
uchaguzi wa serikali za mitaa yakiendelea kwa kasi, huku vyama vya siasa
vikijipanga kujiimarisha na kuhakikisha kuwa wapiga kura wao wanakuwa na sifa
stahiki za kushiriki katika uchaguzi huo.
Changamoto zinazodaiwa kujitokeza sasa zinaweza kuwa
na athari kubwa kwenye mchakato wa uchaguzi, na hivyo ni muhimu kwa mamlaka
husika kuchukua hatua za haraka kurekebisha hali hiyo.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume ya
Uchaguzi, mchakato wa kuchukua fomu za kugombea utafanyika kuanzia tarehe 01
Novemba 2024, na utafuatiwa na kampeni za uchaguzi ambazo zitaanza tarehe 20
hadi 26 Novemba 2024.
Siku ya
kupiga kura imepangwa kuwa tarehe 27 Novemba 2024, ambapo wananchi watajitokeza
kuchagua viongozi wao katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Katika mwendelezo wa ufuatiliaji wa zoezi hili,
Misalaba Media itaendelea kukuletea habari za kina na za kipekee kuhusu
maendeleo ya uandikishaji wapiga kura na matukio mengine muhimu yanayoendelea
jimboni Shinyanga.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo
(CHADEMA) jimbo la Shinyanga mjini, Bwana Hamis Ngunila, akielezea sheria na
kanuni za uchaguzi leo Agosti 22,2024.
Katibu wa Chama
cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jimbo la Shinyanga mjini Bwana Sebastian
Polepole, akizungumza leo Agosti 22,2024.
Post a Comment