" UMEWAHI KUJIULIZA KWAMBA MTU ANAWEZA KUONDOLEWA UVIMBE BILA KUFANYIWA UPASUAJI?

UMEWAHI KUJIULIZA KWAMBA MTU ANAWEZA KUONDOLEWA UVIMBE BILA KUFANYIWA UPASUAJI?

Sekta ya afya nchini Tanzania imepiga hatua kubwa katika matumizi ya sayansi na teknolojia kwa kuanzisha huduma ya kuondoa uvimbe mwilini bila kufanyiwa upasuaji, kwa kutumia mtambo uitwao High Intensity Focused Ultrasound.

Huduma hii ya kipekee inayotolewa na Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni, jijini Dar es Salaam, ni ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, huduma hii inaondoa vimbe bila kuchana, kupasua, kuongezewa damu, wala kupewa dawa za usingizi.

Daktari bingwa wa matumizi ya mtambo huo kutoka Hospitali ya Kairuki, Dokta Fredy Rutachunzibwa, amesema kuwa huduma hii inaondoa vimbe mbalimbali mwilini, ikiwemo vimbe kwenye kizazi na uvimbe wa saratani ya tezi dume.

“Mwishoni mwa mwaka 2023, Hospitali ya Kairuki ilianzisha uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya kwa kutoa huduma hii ya kuondoa uvimbe bila upasuaji, kwa kutumia mtambo tiba uitwao High Intensity Focused Ultrasound. Mtambo huu una uwezo wa kuondoa uvimbe mbalimbali mwilini, ikiwemo uvimbe kwenye kizazi, saratani ya matiti, saratani ya ini na kongosho, saratani ya tezi dume, pamoja na uvimbe mwingine wowote unaoweza kufikiwa na mtambo huu,” amesema Dokta Fredy.

Dokta Fredy amefafanua kuwa, faida za kutumia huduma hii ni kwamba mgonjwa hauguzi kidonda na ndani ya muda mfupi wa uangalizi, anaruhusiwa kuendelea na shughuli zake kama kawaida.

“Faida za kupatiwa huduma hii ya kuondoa uvimbe bila upasuaji ni kwamba hauuguzi kidonda, bali ndani ya siku mbili za uangalizi unaruhusiwa kuendelea na shughuli zako kama kawaida, na mwili unarejea katika hali ya kawaida,” ameongeza.

Huduma hii, inayopatikana katika Hospitali ya Kairuki pekee katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati, itawasaidia Watanzania na nchi jirani kupata huduma hiyo kwa urahisi, tofauti na awali ambapo wagonjwa walilazimika kusafiri hadi Misri, Nigeria, au Afrika Kusini.



Post a Comment

Previous Post Next Post