" KARDINALI PENGO KESHO JUMATATU KUWASILI JIMBO LA SHINYANGA KWA ZIARA YA SIKU NNE

KARDINALI PENGO KESHO JUMATATU KUWASILI JIMBO LA SHINYANGA KWA ZIARA YA SIKU NNE

Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam Mwadhama Polycarp Kardinali Pengo, kesho Jumatatu tarehe 16.12.2024, atawasili Jimboni Shinyanga kwa ziara yake ya siku nne, ambapo pamoja na mambo mengine, atampa daraja takatifu la Ushemasi Frateri Deusdedith Nkandi wa Parokia ya Buhangija Jimbo Katoliki Shinyanga.

Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na uongozi wa jimbo, Kardinali Pengo atapokelewa katika eneo la Nyasamba mpakani mwa Jimbo kuu la Mwanza na Jimbo la Shinyanga, majira ya saa sita mchana, ambapo Mapadre, watawa na waamini wameombwa kujitokeza kwa wingi kumpokea

Akiwa Jimboni Shinyanga, Kardinali Pengo atakutana na kuzungumza na makundi mbalimbali, ambapo siku ya Jumanne tarehe 17.12.2024, saa 4:00 hadi saa 5:30 asubuhi, atakutana na kuzungumza na Mapadre katika makazi mapya ya Askofu huko Ibadakuli ambapo kuanzia saa 6:30 mchana atashiriki chakula cha pamoja na Mapadre na viongozi wa Halmashauri Walei katika Parokia ya Lubaga.

Jumatano tarehe 18.12.2024, kuanzia saa 4:00 hadi saa 6:00 mchana, Kardinali Pengo atakutana na kuzungumza na Mamonsinyori katika Parokia ya Buhangija, na kuanzia saa 6:30 hadi saa 8:00 mchana atashiriki chakula cha pamoja na Mapadre na Shemasi mtarajiwa Deusdedith Nkandi, ambapo saa 9:30 alasiri msafara wake utaelekea katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga kwa maandalizi ya Ibada ya masifu ya jioni, itakayoanza saa 11:00 jioni.

Alhamisi tarehe 19.12.2024, kuanzia saa 4:00 asubuhi hadi saa 8:00 mchana, Kardinali Pengo ataongoza Misa takatifu ya Ushemasi katika Kanisa kuu la Mama mwenye huruma Ngokolo mjini Shinyanga, ambapo kupitia Misa hiyo, atampa Daraja takatifu la Ushemasi Frateri Deusdedith Nkandi.

Kardinali Pengo atarudi Jijini Dar es Salaam siku ya Ijumaa tarehe 20.12.2024, kupitia uwanja wa ndege wa Mwanza.

Post a Comment

Previous Post Next Post