Na Mapuli Kitina Misalaba
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Anamringi Macha,
ameipongeza taasisi ya “Nasimama na Mama” kwa malengo yake ya kusaidia wananchi
hususan wanawake, vijana na makundi yenye uhitaji katika jamii kwa kusimamia
haki, kuhamasisha maendeleo na kudhibiti vitendo vya ukatili.
RC Macha ametoa pongezi hizo wakati wa hafla ya
viongozi wa taasisi hiyo kujitambulisha ofisini kwake, ambapo amesema taasisi
hiyo imeonyesha dira nzuri ya kuunga mkono juhudi za serikali katika kulinda
utu, kukuza maadili na kuchochea maendeleo ya kiuchumi kwa wananchi.
“Nawapongeza
kwa kazi mnayofanya ya kusimamia haki za wanawake, watoto, wanaume na watu
wasio na sauti. Ni vyema mkahakikisha kuwa taasisi hii inakuwa msaada wa kweli
kwa jamii kwa kutekeleza majukumu yenu kwa weledi na kwa kuzingatia sheria za
nchi,” amesema RC Macha.
Aidha, amehimiza taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu
kwa vijana kuhusu umuhimu wa kujiepusha na makundi hatarishi na badala yake
wajikite kwenye shughuli halali zitakazowawezesha kiuchumi na kimaadili.
Aidha, RC Macha amehimiza taasisi hiyo pia kushiriki
kikamilifu katika kuhamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kushiriki kikamilifu
kwenye shughuli za maendeleo, ikiwemo uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka
huu.
Akizungumza kwa niaba ya Katibu wa taasisi hiyo Mkoa
wa Shinyanga, Katibu wa Kanda ya Serengeti (Shinyanga, Simiyu na Mara), Renatus
Mzenmo amesema taasisi hiyo itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kufuata
sheria, taratibu na kanuni za nchi.
“Tunaahidi
kutekeleza maelekezo ya Mkuu wa Mkoa kwa vitendo. Tutasimama na mama, kijana,
au mtu yeyote ambaye hana sauti katika jamii kwa ajili ya haki, usawa na
maendeleo,” amesema Mzenmo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Nasimama na
Mama Mkoa wa Shinyanga, Zamda Shaban, amesema taasisi hiyo ni mwamvuli wa
kuisaidia jamii hasa wale wanaonyimwa haki, kufanyiwa ukatili au kutelekezwa.
Ameongeza kuwa pia wanajihusisha na sekta ya
ujasiriamali na wanahamasisha vijana na wanawake kuchangamkia fursa za kiuchumi
na kijamii.
Taasisi ya “Nasimama na Mama Popote Nilipo”
imeanzishwa hivi karibuni kwa lengo la kuwa sauti ya wanyonge, kusimamia haki,
na kuchochea maendeleo jumuishi kwa wanawake, vijana na makundi mengine.
Taasisi ya “Nasimama na Mama Popote Nilipo”
imeanzishwa kwa lengo la kuwainua watu waliokosa sauti katika jamii, kulinda
haki za binadamu, na kuhimiza maendeleo jumuishi kwa ushirikiano na serikali na
wadau wa maendeleo.




Katibu wa Kanda ya Serengeti (Shinyanga, Simiyu na
Mara), Renatus Mzenmo akizungumza kwa niaba ya katibu wa Taasisi hiyo Mkoa wa
Shinyanga.

Katibu wa Kanda ya Serengeti (Shinyanga, Simiyu na
Mara), Renatus Mzenmo akizungumza kwa niaba ya katibu wa Taasisi hiyo Mkoa wa
Shinyanga.


Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Mhe. Anamringi Macha (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa Taasisi ya Nasimama na Mama Mkoa wa Shinyanga leo Aprili 30, 2025.









Post a Comment