Basi la kampuni ya Maning Nice lililopata ajali Kijiji cha Sululu Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara
Mkuu wa Wilaya ya Masasi bi Rechal Kassanda akiwajulia hali majeruhi wa ajali
Na Regina Ndumbaro Masasi-Mtwara
Basi la abiria la kampuni ya Maning Nice lenye namba za usajili 848ELA, linalofanya safari kati ya Tunduru na Dar es Salaam, limepata ajali katika kijiji cha Sululu wilayani Masasi, mkoani Mtwara.
Ajali hiyo imetokea katika barabara ya kuelekea Tunduru, ambapo basi hilo lilihusika katika tukio hilo lililosababisha taharuki kwa wakazi wa eneo hilo na abiria waliokuwemo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Mganga Mkuu wa Hospitali ya Wilaya ya Masasi, Dkt. Gembe, jumla ya abiria 23 wamejeruhiwa katika ajali hiyo na walikimbizwa katika Hospitali ya Mkomaindo kwa ajili ya matibabu.
Dkt. Gembe amethibitisha kuwa hakuna mtu aliyepoteza maisha katika ajali hiyo, na hali za majeruhi zinaendelea vizuri huku wakiendelea kupatiwa matibabu.
Mkuu wa Wilaya ya Masasi, Bi Rachel Kasanda, ametembelea hospitali hiyo mara baada ya ajali ili kuwapa pole na kuwafariji majeruhi waliolazwa.
Bi Kasanda ameeleza kusikitishwa kwake na tukio hilo, na amesisitiza umuhimu wa madereva kuchukua tahadhari barabarani ili kuepusha ajali zisizo za lazima.
Wananchi wameomba mamlaka husika kuhakikisha magari yanakaguliwa mara kwa mara na hatua madhubuti kuchukuliwa dhidi ya uzembe wa madereva.
Serikali imeahidi kufuatilia kwa ukaribu chanzo cha ajali hiyo na kuchukua hatua stahiki.
Post a Comment