Na Mapuli Kitina Misalaba
Mwanaume mmoja anayefahamika kwa jina la Chima
Majiyanguhi Samamba ambaye anakadiliwa kuwa na umri wa Miaka 52, mkazi wa Songambale
Kata ya Salawe Halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga, anadaiwa kumpiga mke wake
hadi kusababisha kifo kisha kumzika kwenye shimo la choo lililopo pembezoni mwa
nyumba yake.
Taarifa za tukio hilo zilianza kusambaa jana jioni
baada ya wananchi kutoa taarifa kwa uongozi wa Kijiji ambapo Mwenyekiti wa
Kijiji cha Songambele, Bwana Lazaro Enock, akizungumza na Misalaba Media leo Oktoba 8, 2025 amethibitisha kupokea taarifa hizo
na kueleza kuwa leo ni siku ya 12 tangu mauaji hayo kufanyika.
Amesema kuwa baada ya kupata taarifa hizo, alichukua
hatua za haraka kutoa taarifa kwa viongozi mbalimbali wa serikali pamoja na
jeshi la polisi. Kwa mujibu wa Enock, awali jeshi la sungusungu lilimhoji
mtuhumiwa ambapo alikanusha kufanya mauaji, lakini baada ya kufikishwa kituo
cha polisi alikiri kuwa alimuua mke wake.
“Baada ya mahojiano, polisi walishirikiana
na wananchi kufukua mwili wa marehemu, na uchunguzi wa kitabibu umefanyika
kabla ya kukabidhi mwili kwa familia kwa ajili ya mazishi,” amesema
Enock.
Kwa upande wake, Mtendaji wa Kijiji cha Songambele, Bi
Evalina Isack, amekiri kupokea taariza hizo na kwamba leo ameshiriki hatua zote za kufukua mwili huo huku akiwashukuru
wananchi kwa kutoa ushirikiano na kutoficha taarifa za tukio hilo.
Ameitaka jamii kuacha kujichukulia sheria mkononi na
badala yake kutumia viongozi wa serikali, dini na vyombo vya sheria kutatua
migogoro.
“Tunawaomba wananchi kuwa na subira pale
wanapokuwa na migogoro. Serikali na vyombo husika vipo kwa ajili ya kutoa
suluhisho, siyo kuchukua sheria mikononi,” amesema Evalina.
Mwili wa marehemu, aliyezaliwa mwaka 1978 ambaye hadi
sasa angekuwa na miaka 47, umekabidhiwa kwa familia kwa ajili ya mazishi ambayo
yanatarajiwa kufanyika leo katika eneo la Ntobo, Halmashauri ya Msalala, Wilaya ya
Kahama, mkoani Shinyanga, hata hivyo majina yake bado hayajafahamika rasmi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Kennedy
Mgani, amesema jeshi la polisi linaendelea na uchunguzi wa tukio hilo, na
kwamba taarifa kamili zitatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.
Post a Comment