
Na Mapuli Kitina Misalaba
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini ambaye pia ni
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe.
Paschal Katambi, amesema Serikali imejipanga kutatua changamoto za miundombinu
ya barabara katika Manispaa ya Shinyanga, na kwamba kazi hiyo itafanyika kwa
viwango vya kisasa ikiwa ni sehemu ya mpango mkubwa wa kuwaletea wananchi
maendeleo.
Akizungumza leo kwenye tamasha la michezo ya jadi
lililofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage, Katambi amesema barabara nyingi
ndani ya manispaa hiyo zitajengwa kwa kiwango cha lami, ikiwemo barabara ya
kuelekea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, ambayo kwa muda mrefu imekuwa
kilio kwa wananchi.
Mbali na kuzungumza kwenye tamasha hilo, Katambi pia
ametumia siku ya leo kutembelea kata 13 kati ya 17 za Jimbo lake la Shinyanga
Mjini, ambapo amekutana na wananchi na kuzungumza nao kuhusu miradi mbalimbali
ya maendeleo. Katika kila kata aliyotembelea, Katambi ametoa zaidi ya shilingi
milioni tatu kwa ajili ya kutatua changamoto, ikiwa ni hatua ya haraka ya
kuharakisha utekelezaji wa miradi midogo ya maendeleo.
“Tunaendelea
kuwahudumia wananchi kwa vitendo. Hatuahidi tu bali tunatoa fedha kusaidia
miradi kwenye kila kata. Kazi yetu ni kuhakikisha kuwa Shinyanga inabadilika
kwa kasi,” amesema Katambi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi
(CCM) Mkoa wa Shinyanga, Mhe. Mabala Mlolwa, amempongeza Mhe. Katambi kwa kazi
kubwa anayoifanya kwenye jimbo lake, huku akimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan kwa kuendelea kuonesha nia ya dhati ya kupeleka maendeleo kwa wananchi
wa Shinyanga.
“Tunajivunia kuwa na Mbunge Katambi. Amekuwa
kiongozi wa vitendo, na tumeshuhudia namna ambavyo Rais wetu Dkt. Samia amekuwa
akivuta maendeleo kwa kasi isiyo na mfano. Tuna imani kubwa na Serikali ya
Awamu ya Sita,” amesema Mlolwa.
Aidha, Mlolwa amewaomba wananchi waendelee kukiunga
mkono Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa kuwa kimeendelea kusimamia utekelezaji wa
miradi ya maendeleo kwa ufanisi mkubwa.
Tamasha hilo la michezo ya jadi limeibua hisia
mbalimbali kutoka kwa wakazi wa Manispaa ya Shinyanga, ambapo wengi wamesema ni
ishara kuwa viongozi wao hawawasahau bali wanajitahidi kurudi kwao na
kusikiliza kero zao moja kwa moja.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini ambaye pia ni Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe. Paschal Katambi, akizungumza kwenye tamasha la michezo ya jadi lililofanyika katika Uwanja wa CCM Kambarage leo Mei 16, 2025.
Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini ambaye pia ni
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu), Mhe.
Paschal Katambi, akizungumza kwenye tamasha la michezo ya jadi lililofanyika
katika Uwanja wa CCM Kambarage leo Mei 16, 2025.
Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga,
Mhe. Mabala Mlolwa, akimpongeza Mhe. Katambi kwa kazi kubwa anayoifanya kwenye
jimbo lake.
Post a Comment